Pietro Paolo Savorgnan di Brazzà (aliyejulikana pia kwa jina la Kifaransa Pierre Paul François Camille Savorgnan de Brazza; 26 Januari 1852 - 14 Septemba 1905) alikuwa mpelelezi aliyeanzisha Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo. Alizaliwa Mwitalia na kuchukua baadaye uraia wa Ufaransa.

Pietro S. di Brazza katika mavazi ya safari

Utoto katika Italia na kuhamia Ufaransa

hariri

Brazza alizaliwa mjini Roma (Italia) katika familia ya kikabaila akasomeshwa Paris. Akajiunga na chuo cha kijeshi cha wanamaji na kuingia katika jeshi la maji la Ufaransa. Safari za kwanza zilimfikisha mwambanoni wa Amerika ya Kusini na Afrika ya Magharibi. Mwaka 1874 alifika mara ya kwanza mdomoni wa mto Gabon akajitolea kufanya safari za kupeleleza mwendo wa mto huu.

Safari za upelelezi

hariri

Akarudi Ufaransa akajipatia pesa za kufanya safari kubwa ya kugundua mwendo wa mto Ogowe. 1875-1878 alifuata mwendo wa mto huu na kuchora ramani yake hadi ndani ya eneo la Jamhuri ya Kongo ya leo. Akaongozana na kikundi kidogo pamoja na daktari mmoja, mtaalamu mmoja wa mimea na askari 12 Wasenegal.

Miaka 1879-1882 alitumwa na serikali ya Ufaransa kwa safari ya pili kwa shabaha ya kupeleleza mto wa Kongo. Wafaransa walitaka kuanzisha biashara na beseni ya Kongo na kujiandaa nafasi ya kuanzisha koloni. Hapo Brazza alifahamiana na mfalme Makoko wa Wabateke na kununua kutoka kwake ardhi kwa ajili ya kituo kilichokuwa baadaye mji wa Brazzaville. Alifanya pia mikataba ya ulinzi na Makoko na machifu wengine.

Gavana Mkuu wa Kongo ya Kifaransa

hariri

1886 - 1890 alipewa cheo cha gavana mkuu wa koloni mpya ya Kongo ya Kifaransa.

Mkoloni mpole

hariri

Brazza ametajwa mara nyingi kama mtu wa pekee kati ya wakoloni wa siku zile. Kuna taarifa ya kwamba alichukizwa na mbinu za kinyama alizoona zilivyotumiwa na Wafaransa walipokandamiza ghasia katika Algeria alipotembelea huko mara ya kwanza. Brazza mwenyewe alisemekana alifanya safari zake zote bila kuua watu au kutumia mbinu za mabavu akibeba naye vifaa alivyotumia kwa kulipia huduma alizohitaji badala ya kulazimisha wenyeji kumpatia chakula au misaada mingine.

Katika kipindi chake kama gavana wa kwanza wa koloni ya Kongo ya Kifaransa kuna taarifa ya wanahabari waliotembelea ya kuwa na tofauti kubwa kulingana na hali katika Kongo ya Ubelgiji ambako wakati uleule mfalme Leopold alijenga dola lake la binafsi kwa unyama. Inasemekana mishahara ililipwa na unyama kutokuwepo.

Matatizo na serikali ya Ufaransa na kuondolewa kwake

hariri

Mtindo wake ulimweka katika matatizo na serikali ya Paris baada ya muda mfupi. Waziri wa koloni André Lebon aliamua mwa. 1887 kukodi maeneo makubwa ya koloni kwa makampuni ya kibiashara. Shabaha ilikuwa kufaidia na malighafi ya koloni kwa kukabidhi eneo mkononi mwa kampuni iliyopewa haki ya kukusanya malighafi pamoja na madaraka ya kutawala wenyeji.

Brazza aliona ubaya wa utaratibu huu katika eneo jirani la Kongo ya Ubelgiji ambako wenyeji walifanywa kuwa kama watumwa waliolazimishwa kukusanya mpira wa miti au meno ya tembo badala ya kodi waliyodaiwa; lakini makampuni yaliwalazimisha bila huruma na kutoa adhabu kali kama idadi ya mpira n.k. haikutosha kwa mahitaji ya kampuni, tena kwa kuongeza kisai kilichotakiwa kukusanywa mara kwa mara. Upinzani wowote ulikandamizwa kinyama.

Brazza alikataa kutekeleza maagizo. Makampuni na matajiri waliotaka kujitayarisha katika koloni walipiga kempeni dhidi yake. Magazeti ya Paris yalichapisha habari za kasoro za gavana Brazza. Katika Januari 1898 aliambiwa kuondoka Kongo. Brazza alijiuzulu katika utumishi wa serikali akaenda kukaa maisha ya mapumziko Algiers iliyokuwa koloni ya Ufaransa siku zile.

Safari ya mwisho

hariri

Alirudi tena Kongo mwaka 1905 kwa sababu aliteuliwa kufanya utafiti juu ya matatizo katika koloni. Palikuwa na taarifa ya kwamba wenyeji walilazimishwa kwa unyama kukusanya mpira wa miti. Brazza aliweza kuthebitisha madai haya katika taarifa aliyoandika kwa urefu kwa ajili ya serikali ya Ufaransa.

Kwenye safari ya kurudi Brazza aliugua akafa tar. 14 Septemba 1905 huko Dakar (Senegal). Taarifa yake ilifichwa na serikali ya Ufaransa kama siri kufuatana na azimio la kamati ya bunge iliyoona ilikuwa ya aibu mno.

Kujengwa kwa kaburi Brazzaville

hariri

Majivu yake yalizikwa huko Algiers. Jiwe la kaburi lasema "une mémoire pure de sang humain" ('kumbukumbu isiyochafuliwa na damu ya wanadamu').

Mwaka 2006 serikali ya Kongo iliamua kumheshimu Brazza kwa kumjengea kaburi mjini Brazzaville. Tarehe 3 Oktoba 2006 majivu yake yakapelekwa Kongo kutoka Algiers.

Vitabu

hariri

Viungo vya Nje

hariri