Samakimagamba

(Elekezwa kutoka Polypteridae)
Samakimagamba
Samakimagamba kijivu (Polypterus senegalus)
Samakimagamba kijivu (Polypterus senegalus)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Nusufaila: Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo)
Ngeli: Actinopterygii (Samaki walio na mapezi yenye tindi)
Oda: Polypteriformes (Samaki kama samakimagamba)
Familia: Polypteridae (Samaki walio na mnasaba na samakimagamba)
Bonaparte, 1835
Ngazi za chini

Jenasi 2, spishi 14:

Samakimagamba ni samaki wa kizamani wa maji matamu wa familia Polypteridae, familia pekee ya oda Polypteriformes. Mwili wao umefunikika kwa magamba manene yafananao na mifupa. Badala ya pezimgongo moja wana vipezimgongo vingi. Wanatokea Afrika tu, hususa katika vinamasi vya delta (mdomo wa mto) na nyanda zinazofurikika mara kwa mara.

Maelezo

hariri

Samaki hawa wamerefushwa wenye urefu wa upeo wa sm 25 hadi zaidi ya sm 100 kulingana na spishi. Wana mfululizo wa kipekee wa vipezimgongo vinavyotofautiana kwa idadi kutoka 7 hadi 18 badala ya pezimgongo moja. Kila kimoja cha vipezimgongo kina ncha mbili na mwiba mbele yake. Mwili umefunikika kwa magamba manene kama mifupa yenye umbo la almasi. Muundo wa taya zao unafanana kwa karibu zaidi na ule wa tetrapodi kuliko ule wa samaki wa aina ya teleosti. Samakimagamba wana idadi ya sifa nyingine za msingi, pamoja na mapeziubavu yenye nyama yanayofanana kijuujuu na yale ya samaki wenye mapezindewe (Sarcopterygii)[1]. Pia wana jozi ya matundu kama mipasuko (spirakuli) juu ya vichwa vyao ambayo hutumiwa kuvuta pumzi[2], sahani mbili za koo na mapafu yaliyounganishwa kwa tumbo (pafu la kushoto ni fupi kuliko lile la kulia)[3]. Jozi nne za matao ya matamvua zipo[4].

Chakula na sifa

hariri

Samakimagamba hukiakia usiku na kujlisha na vertebrata wadogo, gegereka na wadudu[1]. Chakula chao cha kawaida katika tangisamaki ni pamoja na minyoo ya damu (lava wa Chironomidae). Wanajulikana kuwa na uwezo wa ajabu wa kunusa. Uzazi unafanyika kwa jike kutaga mayai 100 hadi 300 kwa muda wa siku chache na utungisho na dume[5].

Upumuaji wa hewa

hariri

Samakimagamba huwa na jozi ya mapafu yaliyounganisha na umio kupitia mwanya. Hupumua hewa kwa hiari na huipata wakati maji wanamokaa yana oksijeni duni[6]. Mapafu yao yana mishipa mingi ili kuwezesha ubadilishaji wa gesi. Damu ya ateri isiyo na oksijeni huletwa kwenye mapafu na jozi ya ateri za mapafu zilizo matawi ya ateri za matamvua ya nne na damu yenye oksijeni huondoka mapafu kwenye vena za mapafu. Tofauti na kambaremamba na tetrapodi wengi, mapafu yao ni mifuko laini badala ya tishu zilizo na vifuko vya hewa (alveoli). Samakimagamba ni wa kipekee kwa kuwa wanapumua kwa kutumia uvutaji wa pumzi bila kutumia misuli[6]. Wakishusha pumzi magamba ya kidari huvutwa ndani, kisha hurudi kama mtambo na kuvuta pumzi. Wanaonekana kupendelea kuvuta pumzi kupitia spirakuli zao wakati hawasumbuliwi au katika maji ya kina kifupi sana ambapo hawawezi kuweka mwili wao katika ukao wa kutosha ili kuvuta pumzi kupitia mdomo wao[2].

Spishi

hariri

Marejeo

hariri
  1. 1.0 1.1 Wiley, Edward G. (1998). Paxton, J.R.; Eschmeyer, W.N. (whr.). Encyclopedia of Fishes. San Diego: Academic Press. ku. 75–76. ISBN 978-0-12-547665-2.
  2. 2.0 2.1 Graham, Jeffrey (2014). "Spiracular air breathing in polypterid fishes and its implications for aerial respiration in stem tetrapods". Nature Communications. 5: 3022. Bibcode:2014NatCo...5.3022G. doi:10.1038/ncomms4022. PMID 24451680.
  3. Berra, Tim M. (2001). Freshwater Fish Distribution. San Diego: Academic Press.
  4. AccessScience | Encyclopedia Article | Polypteriformes
  5. "Breeding Bichirs". www.aquaticcommunity.com. Iliwekwa mnamo 2021-08-27.
  6. 6.0 6.1 Graham, J.B. 1997. Air-breathing Fishes: Evolution, diversity, and adaptation. San Diego: Academic Press. 299 p.