Rhodesia ya Kaskazini

Rhodesia ya Kaskazini (kwa Kiingereza: Northern Rhodesia) ilikuwa jina la koloni halafu eneo lindwa la Uingereza katika Afrika ya Kusini lilipopata uhuru wake kwa jina la Zambia tarehe 24 Oktoba 1964.

Bendera ya Rhodesia ya Kaskazini (1939-1953).

Upanuzi wa kampuni ya Cecil Rhodes

hariri

Jina lilitokana na Cecil Rhodes aliyetwaa eneo hili pamoja na "Rhodesia ya Kusini" au Zimbabwe na kuliweka chini ya Kampuni ya Kiingereza ya Afrika Kusini (British South Africa Company).

Kampuni ya Rhodes iliwahi kutwaa maeneo ya Zimbabwe kuanzia 1885 na kupanua kaskazini ya mto Zambezi kuanzia 1890. Nia ya Rhodes ilikuwa kuunganisha kanda la Afrika kati ya Afrika Kusini ("rasi ya Tumaini Jema") hadi Misri ("Cape to Cairo") chini ya bendera ya Uingereza.

Wakati wa Rhodes utajiri wa madini katika "kanda la shaba" haukujulikana bado, hivyo kampuni ya Rhodes ililenga hasa kuupanua utawala wake kuelekea kaskazini na kujenga reli hadi migodi ya Katanga katika Kongo ya Kibelgiji.

Uenezi kaskazini ya Zambezi

hariri

Rhodes alifaulu kutwaa nchi kaskazini ya mto Zambezi bila matatizo makubwa.

Mfalme wa Walozi katika magharibi alifanya mkataba wa ulinzi na Waingereza mwaka 1890 kwa imani ya kwamba ushirikiano na kampuni ya Rhodes ungehifadhi ufalme wake dhidi ya Wareno na Wangoni. Wabemba waligawanyika kati yao wakakosa wakati ule uwezo wa upinzani. Magharibi ilitawaliwa kama "North Western Rhodesia".

Watu wa pekee waliompinga kijeshi walikuwa Wangoni katika mashariki ya nchi lakini walishindwa na silaha za kisasa za jeshi la kampuni mwaka 1897. Eneo lao lilitawaliwa kama "North-Eastern Rhodesia".

Pande zote mbili ziliunganishwa chini ya kampuni kama "Northern Rhodesia" mwaka 1911.

Nchi lindwa ya Uingereza

hariri

Mwaka 1923 serikali ya Uingereza iliamua kuchukua utawala mikononi mwake. Rhodesia ya Kusini ikawa koloni lenye kiwango cha kujitawala kwa ajili ya walowezi Wazungu wa huko. Rhodesia ya Kaskazini lilikuwa na walowezi wachache tu, ikawekwa chini ya idara ya makoloni ya Uingereza kama nchi lindwa kuanzia 1924 hadi uhuru mwaka 1964. Kampuni ya Kiingereza ya Afrika Kusini iliendelea kibiashara hasa kuchimba madini kwenye migodi ya kanda la shaba hadi uhuru uliolazimishwa kukabidhiwa mali yake kwa serikali ya nchi huru.