Rhodesia ya Kusini

Rhodesia ya Kusini ilikuwa koloni la Uingereza katika nchi ya Kusini mwa Afrika iliyopata uhuru kwa jina la "Zimbabwe" tangu mwaka 1980.

Mahali pa Rhodesia Kusini (=Zimbabwe) katika Afrika.
Bendera ya Rhodesia Kusini.
Ugawaji wa kimbari wa ardhi katika Rhodesia Kusini mnamo 1965
nyeupe: ardhi ya walowezi wazungu
buluu:ardhi chini ya mamlaka ya makabila ya Kiafrika
nyekundu:ardhi ya binafsi ya Waafrika
kijani: ardhi ya serikali

Kuundwa na Cecil Rhodes

hariri

Koloni liliundwa na Cecil Rhodes aliyetwaa eneo hili pamoja na "Rhodesia ya Kaskazini" au Zambia na kuliweka chini ya Kampuni ya Kiingereza ya Afrika Kusini (British South Africa Company).

Rhodes aliwahi kujaribu kupata mapatano na mfalme Lobengula wa Wandebele kuhusu haki za kuchimba madini katika Matabeleland. Mfalme alikataa hadi mwaka 1888 alipokubali mapatano ya Rudd. Lobengula alidanganywa na Charles Rudd kwa njia ya mkataba huo uliokuwa msingi wa kutwaliwa kwa eneo lake kwanza na baadaye Zimbabwe yote.

Uvamizi

hariri

Mwaka 1890 kikosi cha askari 500 wa kampuni kiliingia kutoka Afrika Kusini na kutwaa nchi. 180 kati yao walikuwa walowezi walioapishwa kama askari wa "Pioneer Column" na kupewa ardhi baadaye. 300 walikuwa askari wa Polisi ya Kiingereza kwa Afrika ya Kusini (British South Africa Police) ilikuwa kiini cha polisi na jeshi la koloni ya baadaye.

Kwa silaha zao za kisasa, hasa bunduki za Maxim, walishinda wenyeji. Vita ya Matabele ya 1893-1894 ilikuwa vita ya kwanza iliyoona matumizi ya bunduki ya mtombo ya kisasa duniani. Waingereza 50 waliweza kushinda Wandebele 5,000.

Hadi mwaka 1897 kampuni iliweza kupambana na upinzani wa kijeshi wa Wandebele na pia Washona ikawashinda.

Serikali ya Uingereza ilikubali kampuni itawale koloni lote (pamoja na Rhodesia ya Kaskazini) kwa niaba ya Ufalme wa Muungano wa Britania na Eire ya Kaskazini.

Hadi vita ya kwanza ya dunia idadi ya walowezi ikaongezeka wakaanza kudai madaraka ya kujitawala kama makoloni kadhaa ya Uingereza yenye walowezi Wazungu, kwa mfano Afrika Kusini, Kanada au Australia.

Koloni la kujitawala

hariri

Mwaka 1922 wawakilishi wa walowezi walidai madaraka ya kujitawala. Wengine walipendelea kuunganishwa na Afrika Kusini. Kura ilipigwa kati ya walowezi 34,000 juu ya swali la kuwa koloni la Uingrgeza lenye madaraka ya kujitawala au kuwa jimbo la tano la Afrika Kusini. Walio wengi walipendelea kuwa koloni lenye madaraka ya kujitawala.

Tangu 12 Septemba 1923 serikali ya Uingereza ilichukua utawala juu ya Rhodesia moja kwa moja ikawa koloni ya Uingereza na kampuni ilibaki na shughuli za kiuchumi. Wazungu walipewa serikali yao pamoja na kiwango cha kujitawala katika mambo ya ndani. Waziri mkuu wa kwanza alikuwa Charles Patrick John Coghlan tangu 1923 akifuatwa 1927 na Howard Unwin Moffat. Idadi ya walowezi wazungu ikaongezeka hasa baada ya vita kuu ya pili ya dunia na kufikia 270,000 mwaka 1970.

Hali ya Waafrika

hariri

Hali ya wenyeji Waafrika ilikuwa ya duni tangu uvamizi. Maeneo mapana yenye rutuba yalitawaliwa na walowezi. Wenyeji wa sehemu zile walipaswa ama kukubali kama wafanyakazi kwenye mashamba ya Wazungu au kuhamia katika Rizavu za Waafrika. Hata hivyo umoja wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi zilionyesha pia maendeleo fulani upande wa Waafrika wenyeji kwa kuondoa vita za mara kwa mara na kuleta huduma za kwanza za afya na za elimu. Viongozi wa Wazungu Warhodesia waliamini ya kwamba wakati ujao lakini si karibuni sehemu ya Waafrika wangeanza kushirikiana nao katika uongozi wa koloni. Isipokuwa waliamini ni sharti wenyewe walipaswa kuamua ni lini Waafrika wangekuwa tayari kuanza kushirikana nao.

Wakati huohuo wanasiasa wazungu waliendelea kukaza sheria zilizoongeza uguma kwa Waafrika wengi. Sheria ya ardhi ya 1931 iligawa nchi katika maeneo ya wazungu na Waafrika lakini Waafrika walipata theluthi moja ya ardhi tu. Tangu 1936 kila Mwafrika wa kiume alipaswa kutembea na kitambulisho wakati wa kuzuru nje ya rizavu. Sheria ya 1951 (Native Land Husbandry Act) iliamua ya kwamba Waafrika wangekuwa na kiwango fulani cha ardhi na cha mifugo iliyotegemea mazingira hasa rutuba ya eneo. Lakini matokeo ya sheria yalibana uwezo wa Waafrika wengi kuendelea na kujenga maisha yao hivyo wakaongeza upinzani.

Mapambano ya uhuru kuanza

hariri

Baada ya vita kuu ya pili wazungu wa Rhodesia waliona maendeleo mengi lakini Waafrika walianza kusikitika zaidi. ANC ya Afrika Kusini ilienea hadi Rhodesia. Mwenyekiti wake nchini tangu 1957 alikuwa kijana Joshua Nkomo. ANC ilipopigwa marufuku 1959 Nkomo akaenda Uingereza akarudi 1960 na kuunda National Democratic Party of Zimbabwe (NDP) iliyopigwa marufuku 1961 akaunda ZAPU. Chama hiki kilifarakana mwaka 1963 ilhali ZANU ilijitenga chini ya Ndabaningi Sithole, na Robert Nugabe alijiunga baadaye na ZANU.

Rhodesia ya Wazungu

hariri

Mwaka 1965 serikali chini ya walowezi Wazungu ilitangaza uhuru wa nchi kutoka Uingereza kwa jina la Rhodesia. Hii ilikuwa chanzo cha vita ya msituni ya Rhodesia ambako majeshi ya ZIPRA (jeshi la ZAPU) na ZANLA (jeshi la ZANU) yalipigana na jeshi la Rhodesia.

Rhodesia haikutambuliwa na Ufalme wa Maungano (Uingereza) na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola hivyo ilitangaza kuwa jamhuri na kujitenga kabisa na Uingereza. Nchi za nje zilianza kuweka vikwazo vya kiuchumi (sanctions) dhidi ya Rhodesia.

Vita ya msituni iliendelea. Majeshi ya ZIPRA na ZANLA yalikosa uwezo wa kushinda jeshi la Rhodesia lakini yalikuwa na nafasi ya kushambulia na kurudi baadaye katika makambi yao Zambia, Msumbiji na Angola. Kwa njia hii walilazimisha serikali ya Rhodesia kutumia pesa nyingi na kuita wanaume kati ya Wazungu kuhudumia jeshini kwa wiki kadhaa kila mwaka. Idadi kubwa zaidi ya askari wa Rhodesia walikuwa Waafrika waliojitolea. Vijana Wazungu wote walipaswa kuhudumua jeshini kwa mwaka mmoja halafu kuwa tayari kuitwa kwa wiki kadhaa kila mwaka.

Rhodesia-Zimbabwe na kushirikishwa kwa Waafrika wa ndani

hariri

Kuanzia 1976 Afrika Kusini (iliyotawaliwa bado ba serikali ya Apartheid) ilipunguza misaada yake kwa Rhodesia na serikali chini ya Ian Smith ilipaswa kujadiliana 1978 na viongozi Waafrika ndani ya Rhodesia ambao hawakushiriki katika vita ya msituni, walioongozwa na askofu Abel Muzorewa. Walipatana katiba mpya ambako wananchi wote walipewa haki ya kupiga kura, ilhali robo moja ya nafasi kwenye bunge na katika serikali zilitengwa kwa wawakilishi wa Wazungu wa Rhodesia.

Katika uchaguzi wa Machi 1979 Waafrika wote waliruhusiwa kushiriki mara ya kwanza. ZANU na ZAPU walikaribishwa kushiriki kwa mashariti ya kuacha mapambano ya vita, walikataa wakaita Waafrika wote kutoshiriki wakatangaza watashambulia hao watakaoshiriki. Hata hivyo zaidi ya asilimia 64 ya wanachi walishiriki, chama cha Muzorewa "United African National Congress " kilishinda. Muzorewa alikuwa waziri mkuu, Josiah Gumede alichaguliwa kuwa rais. Jina la nchi ikabadilika kuwa "Rhodesia-Zimbabwe".

Mapatano ya Lancaster House na mwisho wa Rhodesia

hariri

ZANU na ZAPU pamoja na nchi nyingi wa nje walikataa kukubali uhalali wa uchaguzi huu na mashambulio ya majeshi ya ZIPRA na ZANLA yaliendelea. Serikali za Marekani na Uingereza zilishawishi Muzorewa kutafuta maelewano na Mugabe na Nkomo. Katika hali hii serikali ya iliamua kuitikia wito wa Ufalme wa Maungano wa kukutana na wawakilishi wa ZANU na ZAPU pale Lancaster House, Uingereza. Mapatano ya Lancaster House yalileta mwisho wa Rhodesia-Zimbabwe.

Mapatano haya yalisema - pande zote zitasimamisha matendo ya kivita - misingi ya katiba mpya ilikubaliwa - Zimbabwe-Rhodesia itarudi chini ya mamlaka ya Uingereza na kuitwa tena "Southern Rhodesia" - serikali itakuwa mkononi mwa gavana Mwingereza - uchaguzi mpya utatokea katika miezi ya kwanza ya 1980

Baada ya uchaguzi kwenye Februari 1980, Rhodesia Kusini ilikuwa jamhuri huru ya Zimbabwe.

Tanbihi

hariri


Viungo vya Nje

hariri
Jua habari zaidi kuhusu Rhodesia kwa kutafuta kupitia mradi wa Wikipedia Sister
  Uchambuzi wa kamusi kutoka Wikamusi
  Vitabu kutoka Wikitabu
  Dondoo kutoka Wikidondoa
  Matini za vyanzo kutoka Wikichanzo
  Picha na media kutoka Commons
  Habari kutoka Wikihabari
  Vyanzo vya elimu kutoka Wikichuo