Ukanda wa Van Allen

Ukanda wa Van Allen (kwa Kiingereza Van Allen belt, Van Allen radiation belt) ni eneo linaloviringisha Dunia katika anga-nje (yaani nje ya angahewa). Unafanywa na chembe atomia hasa protoni na elektroni zilizoshikwa na uga sumaku wa Dunia.

Ukanda wa Van Allen.
Uga sumaku wa Dunia ni kinga dhidi ya mnururisho wa upepo wa Jua.

Jina linatokana na mwanafizikia James Van Allen kutoka Marekani aliyeongoza utafiti wa ukanda huu wa mnururisho katika miaka ya 1950.

Ukanda wa Van Allen una sehemu mbili:

  • ukanda wa ndani uko hasa juu ya latitudo za kati, yaani karibu na ikweta, kwenye kimo cha kilomita 700 hadi 2000 juu ya uso wa ardhi ukishikwa hasa na protoni
  • ukanda wa nje ni mpana zaidi, kwenye kimo cha kilomita 15,000 hadi 25,000 ukifanywa hasa na elektroni

Chembe hizo huwa na chaji ya umeme hasi wala chanya. Hivyo vinavutwa na nguvu ya usumaku wa Dunia baina ya ncha mbili za uga wake. Kwa njia hii ugasumaku wa Dunia unazuia sehemu kubwa ya chembe hizi kufika kwenye uso wa ardhi na hii ni kinga dhidi ya mnururisho unaoweza kuhatarisha viumbehai duniani kutokana na nishati kubwa inayoshikwa nazo.

Asili ya chembe hizo ni: kwa upande mmoja upepo wa Jua (mkondo wa chembe kutoka Jua) na kwa upande mwingine atomi zinazopigwa na miale ya mnunurisho wa mialimwengu (ing. cosmic rays) na kupasuliwa.

Sayari nyingine kama Mshtarii (Jupiter) na Zohali (Saturn) huwa pia na ukanda wa mnururisho wa kufanana.

Ilhali uga sumaku ni dhaifu zaidi karibu na ncha za Dunia, basi chembe zenye chaji vinaweza kuingia katika angahewa na kusababisha hapa mianga ya aurora.

Kiwango cha mnururisho ndani ya ukanda wa Van Allen ni hatari kwa watu na pia mitambo, hivyo satelaiti nyingi na pia vituo vya angani kama MIR na Kituo cha Anga cha Kimataifa ISS vinazunguka dunia kwa obiti zinazobaki chini ya ukanda huu.

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ukanda wa Van Allen kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.