Vietnam Kusini au Jamhuri ya Vietnam (kwa Kivietnam: Việt Nam Cộng Hòa) ilikuwa nchi katika nusu ya kusini ya Vietnam ya leo kati ya miaka 1954 na 1976. Mji mkuu ulikuwa Saigon (leo: Mji wa Ho-Chi-Minh).

Nembo (1967 - 1975)
Ramani ya Vietnam Kusini
Wanajeshi wa Marekani katika Vietnam Kusini

Uhuru wa koloni ya Kifaransa

hariri

Koloni la Kifaransa la Vietnam liligawiwa mwaka 1954 wakati wa kuondoka kwa Wafaransa. Katika kaskazini ya nchi wanamgambo Wakomunisti chini ya Ho Chi Minh waliwahi kuwafukuza Wafaransa katika vita ya Indochina. Wakimbizi wengi waliohofia Wakomunisti walikimbilia kusini.

Wafaransa waliwahi kuunda serikali ya kienyeji na kumkabidhi madaraka Kaisari Bao Dai kwa sehemu ya kusini walipobaki na uwezo. Mkutano wa Geneva juu ya Indochina ya mwaka 1954 uliomaliza vita uliamua ya kwamba serikali ya Bao Dai itawale kusini na kanda la eneo lisilo na jeshi ligawanye sehemu mbili za nchi.

Udikteta wa Diem

hariri

Wakati wa kundoka kwa Wafaransa Bao Dai alipinduliwa na waziri mkuu Ngô Đình Diệm. Diem alikataza uchaguzi kwa Vietnam yote uliopangwa kwa mwaka 1956. Akaendesha vikali utawala kama rais akawa dikteta. Mwenyewe alikuwa Mkatoliki akashindwa kujenga uhusiano na Wabuddha waliokuwa wengi kati ya wakazi. Farakano hili kati ya Wakristo na Wabuddha lilisaidia upanuzi wa Wakomunisti.

Vita ya Vietnam

hariri

Mwaka 1963 Diem alipinduliwa na jeshi na nchi iliendelea chini ya kamati za kijeshi. Wakomunisti kutoka kaskazini walipeleka silaha kusini na kuanzisha maeneo waliotawala kwa umbo la chama cha Vietkong. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipanuka. Marekani ilijiunga katika vita hii kwa kutuma wanajeshi kwanza kama washauri na wasaidizi wa jeshi la Vietnam Kusini na baadaye pia kwa vikosi vilivyoshiriki katika vita ya msituni dhidi ya Wakomunisti wa Vietkong.

Kuingilia kwa Marekani

hariri

Jeshi la Vietnam Kusini liliongozwa vibaya na viongozi wake walijishughulisha zaidi na ufisadi kuliko vita. Wanajeshi wa kawaida hawakuwa na hamu kuwafuata wakubwa ambao walijali pesa kuliko maisha ya watu wao. Hivyo Marekani ilichukua sehemu kubwa zaidi za mapigano na mwaka 1968 wanajeshi 543,000 Wamarekani walikuwepo Vietnam Kusini.

Huko Marekani watu wengi walianza kupinga mchango wa nchi yao katika vita hii na serikali ilianza kupunguza idadi ya wanajeshi wake ikijaribu kuimarisha jeshi la Vietnam Kusini.

Kwa jumla majaribio hayo yalishindikana. Vietnam Kaskazini iliendelea kutuma wanajeshi wengi kupitia Laos na Marekani ilishindwa kuwazuia.

Mwisho wa Vietnam Kusini

hariri

Mwaka 1975 Vietkong pamoja na jeshi la Vietnam Kaskazini iliteka mji mkuu Saigon. Kwa mwaka moja serikali ya kikomunisti ilitawala kusini na mwaka 1976 sehemu mbili za Vietnam ziliunganishwa.

Takriban milioni na nusu ya wakazi wa kusini walikimbia baada ya 1976 wakitumia maboti na mashua ya kila aina wakajaribu kuvuka bahari na kufikia nchi pasipo Ukomunisti. Wengi wao walikufa njiani.