Ho Chi Minh
Ho Chi Minh, aliyezaliwa kwa jina Nguyễn Sinh Cung, (19 Mei 1890 - 2 Septemba 1969 [1]) alikuwa mwanasiasa wa chama cha Kikomunisti na kiongozi (waziri mkuu kutoka mwaka 1945 hadi 1955, na rais kutoka 1945 hadi 1969) wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Vietnam (Vietnam Kaskazini).
Maisha ya awali
haririJina la 'Hồ Chí Minh' alianza kulitumia wakati wa mapinduzi ya Agosti 1945. Alipozaliwa aliitwa Nguyễn Sinh Cung. Kulingana na desturi za Ukonfusio alibadilisha jina kuwa Nguyễn Tất Thành alipofikia umri wa miaka kumi. Baadaye alitumia majina bandia mbalimbali hasa kutokana na kazi yake ya kisiasa. Watu wa Vietnam mara nyingi humtaja kama Bác Hồ (Mjomba Ho)[2].
Nguyen alizaliwa katika kijiji cha Kim Liên, kaskazini mwa Vietnam, wakati ule sehemu ya Annam iliyokuwa eneo la koloni la Ufaransa. Baba yake alikuwa hakimu. Nguyen alipokea mafunzo ya Kikonfusio akasoma baadaye kwenye shule ya Kifaransa.
Kuanzia mwaka 1911 hadi 1917 Nguyen alisafiri duniani akifanya kazi mbalimbali kwenye meli kama mpishi. Kwa vipindi vifupi alipata pia kazi katika miji ya Ufaransa, Marekani na Uingereza[3]. Katika miaka 1919 hadi 1923 aliishi Paris ambako alijiunga na Wavietnam wengine katika kundi lililojadili madai ya uhuru kwa nchi yao[4]. Alishiriki pia katika mikutano ya chama cha Kisoshalisti. Mwaka 1920 alijiunga na chama cha kikomunisti kilipojitenga na Wasoshalisti.
Mwaka 1923 alihamia Urusi alipoajiriwa na Komintern na kusoma kwenye chuo cha kikomunisti mjini Moscow.[5][6]
Kati ya miaka 1924 hadi 1941 alitumwa na Komintern mara kadhaa kwenda China alipohusika kujenga chama cha Kikomunisti[7].
Kuunda Vietnam huru kwa vita dhidi ya Ufaransa
haririMwaka 1941 Ho alirudi Vietnam iliyowahi kuvamiwa na Japani ingawa Wajapani waliruhusu Wafaransa kuendelea kutawala chini yao. Ufaransa iliyoshindwa na Ujerumani huko Ulaya ilidhoofishwa, na Wakomunisti Wavietnam walichukua nafasi kupigania uhuru. Ho aliunda vikosi vya wanamgambo wa Vietminh walioshambulia Wajapani na Wafaransa[8]. Wakati Japani ilipaswa kusalimu amri kwenye mwaka 1945 na jeshi la Jamhuri ya China lilichukua nafasi ya Wajapani, wanamgambo wa Vietminh walitwaa mji wa Hanoi na kutangaza Jamhuri ya Vietnam na serikali iliyoongozwa na Ho Chi Minh[9].
Hata hivyo, kaskazini mwa Vietnam ilikuwa chini ya Jamhuri ya China iliyovumilia kuwepo kwa serikali ya Ho Chi Minh ambayo ilibaki bila mamlaka halisi.
Wakati Wafaransa waliporudi baada ya kupatana na China, Ho Chi Minh alikubali kubaki na Vietnam iliyojitawala chini ya ulezi wa Ufaransa. Lakini mwaka 1946 kulikuwa na mapigano kati ya wanajeshi wa Vietminh na Wafaransa. Hapo Wafaransa walijaribu kurudisha hali ya kikoloni kamili. Hivyo vita ya Indochina ilianza.
Iliendelea hadi 1954 ambako jeshi la Vietminh ilishinda Wafaransa. Mapatano ya amani yaliacha kaskazini mwa Vietnam chini ya serikali ya Ho Chi Minh ilhali kusini kulikuwa chini ya serikali ya kaizari Bao Dai aliyesaidiwa na Marekani na Wafaransa waliokubali kumaliza utawala wao.
Vita ya Vietnam
haririMatokeo ya Vita ya Vietnam yalikuwa mgawanyiko wa nchi. Ho Chi Minh alitawala sasa sehemu ya kaskazini, ilhali Vietnam Kusini ilikuwa chini ya serikali iliyopinga Ukomunisti.
Hapo Ho pamoja na chama cha Kikomunisti waliamua kuanzisha makundi ya wanamgambo huko kusini ambao waliitwa Vietkong. Hao Vietkong walishambulia polisi na maafisa wa serikali ya kusini.
Marekani iliunga mkono Vietnam Kusini kwa msaada wa kijeshi, na Umoja wa Kisovyeti (ukiongozwa na Nikita Krushchev na kisha Leonid Brezhnev) na Jamuhuri ya Watu wa China (iliyoongozwa na Mao Zedong) iliendelea kuunga mkono juhudi za vita za Vietnam Kaskazini hadi ushindi wake.
Kifo
haririAkisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na shida ya moyo, Hồ Chí Minh alijiuzulu na uongozi wa serikali na chama mnamo mwaka 1965. Kwenye asubuhi ya 2 Septemba 1969 alifariki baada ya shtuko la moyo.
Katika wosia wake aliandika alitamani kuchomwa na majivu yake yatawanywe kaskazini, katikati, na kusini mwa Vietnam. Walakini, chama kiliamua kuhifadhi mwili wake na kuuweka ndani ya kaburi ambapo unaoonyeshwa kwa wananchi na watalii wanaopewa nafasi kupita na kumwangalia.
Mnamo 1976, baada ya ushindi katika kusini, mji mkuu wa Vietnam Kusini, Saigon, ulipewa jina la Ho Chi Minh City kwa heshima ya kiongozi huyo.
Marejeo
hariri- ↑ "Ho Chi Minh". Random House Webster's Unabridged Dictionary.
- ↑ Yen Son. "Nguyen Ai Quoc, the Brilliant Champion of the Revolution." Thuong Tin Hanoi. 30 August 1945.
- ↑ Tucker, Spencer C. (1999). Vietnam. UCL Press. ISBN 9781857289220.
- ↑ Huynh, Kim Kháhn, Vietnamese Communism, 1925–1945. Ithaca, NY: Cornell University Press, 1982; pg. 60.
- ↑ Duiker, William J. Ho Chi Minh: A Life. New York: Hyperion, 2000.
- ↑ "The Learning Network".
- ↑ Quinn-Judge, Sophie (2002). Ho Chi Minh: The Missing Years 1919 - 1941. University of California Press. ISBN 978-0520235335.
- ↑ https://web.archive.org/web/20150510160521/http://www.vietquoc.com/hcm-04.htm
- ↑ Davidson, Phillip B., Vietnam at War: The History: 1946–1975 (1991), p. 4.
Viungo vya Nje
haririAngalia mengine kuhusu Ho Chi Minh kwenye miradi mingine ya Wikimedia: | |
Fafanuzi za Kiingereza kutoka Wiktionary | |
picha na media kutoka Commons | |
misaada ya kujisomea kwa Kiingereza kutoka Wikiversity | |
nukuu kutoka Wikiquote | |
matini za ushuhuda na vyanzo kutoka Wikisource | |
vitabu kutoka Wikibooks |
- Chi Minh Ho (1890–1969) kwenye Internet Movie Database
- The Drayton Court Hotel
- Hồ Chí Minh obituary, The New York Times, 4 September 1969
- TIME 100: Hồ Chí Minh
- Ho Chi Minh Selected Writings in PDF format
- Hồ Chí Minh's biography
- Satellite photo of the mausoleum on Google Maps
- Bibliography: Writings by and about Hồ Chí Minh