Wamatengo ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga mashariki.[1][2][3][4][5]

Jiografia ya makazi hariri

Kabila hilo linasifika kwa ukarimu na uhodari wa kazi.

Kwa mujibu wa Egino Ndunguru, ambaye ameandika kwa kina kuhusu historia, mila na desturi za kabila hilo, Wamatengo wanapenda kuishi sehemu za milimani katika eneo lenye hali ya hewa nzuri na rutuba inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kilimo cha mazao kama mahindi, maharage na mihogo, na hasa cha mazao ya biashara (kahawa) na shughuli za ufugaji.

Pia wanafuga wanyama mbalimbali kwa madhumuni tofauti. Kondoo, ng’ombe na sungura wanafuga kwa ajili ya kitoweo, kuku kwa ajili ya tambiko na mahoka, lakini kila familia inalazimika kufuga mbuzi kwa sababu zama hizo alitolewa kama sadaka na mahari. Katika mgawanyo wa kazi, wanawake wanashughulika na kilimo, lakini wanaume na vijana wa kiume kwa asili shughuli yao kubwa ni kuchunga wanyama mchanganyiko.

Chakula hariri

Chakula cha asili cha Wamatengo ni ugali wa mahindi na mboga za majani au maharage. Pia wanakula maboga na viazi vitamu. Mihogo na ulezi wanatumia kutengenezea pombe, hususan wakati wa njaa.

Katika mfumo wa maisha ya zamani, Wamatengo hawakupenda vyakula vya ngano na kahawa kwa kuamini kwamba vimeletwa na wakoloni, lakini sasa mfumo wa maisha umebadilika na wanatumia kama wanavyotumia vyakula vingine.

Nyumba hariri

Baadhi ya Wamatengo waliishi mapangoni hasa wakati wa vita, lakini sasa wamejenga nyumba za miundo na ukubwa tofauti sehemu za milimani ambapo baba, mama na watoto huishi nyumba moja na mifugo wakajengewa banda lao. Kiasili nyumba zao ni za miti ambazo hukandikwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi.

Ni nyumba zenye kuezekwa paa pande mbili tu, maarufu kama mgongo wa tembo na pia hujenga nyumba za msonge.

Nguo hariri

Nguo za asili za Wamatengo huitwa mbinda na zilitengenezwa kwa kutumia miti inayoitwa mitawa. Miti hiyo ilikatwa kisha kutolewa magamba ambayo yalipondwapondwa kisha yakalowekwa mtoni kwenye maji yenye matope meusi kwa muda wa siku moja hivi.

Yalitolewa yakaanikwa juani na yalipokauka yalikuwa tayari kuvaliwa. Magamba hayo yalibadilika rangi yake kutoka hudhurungi na kuwa nyeusi kabisa. Vazi la asili la wanawake liliitwa mpati. Walilifunga kiunoni kisha wakachukua kipande cha vazi lililotengenezwa kwa magome ya miti na kulipitisha katikati ya miguu ili kufunika makalio na sehemu ya siri.

Wanaume pia walivaa vazi hilo kwa kufunika sehemu nyeti pekee.

Ukarimu hariri

Wamatengo ni wakarimu kwa kupokea na kumpa mgeni malazi na chakula. Ikiwa mgeni ni ndugu hukalishwa mkekani, huchinjiwa kuku na hupewa nyama yote na ugali kama heshima. Mgeni akishindwa kumaliza nyama ‘yake’ huzichukua na kupeleka nyumbani kwake.

Baadhi ya wageni hasa wakwe (wayemba) walipewa heshima ya kipekee kwani walitengenezewa pombe na kuchinjiwa mbuzi. Wamatengo hawampi mgeni yeyote chakula chochote kabla hawajaonja wenyewe kwanza. Wakati wa kumkaribisha mgeni chakula, mathalani ugali, mwenyeji humega tonge moja na kula kama ishara ya kumhakikishia mgeni kuwa chakula ni salama kisha humkaribisha na kumwacha aendelee kula peke yake.

Pia wana desturi ya kuonja kinywaji kabla ya kumpa mgeni. Ingawa wajibu wa kupika kwa asili ni wanawake, lakini wanaume wa Kimatengo hadi leo hupenda ama tuseme si ajabu kushirikiana na wake zao kupika. Asilimia kubwa ya Wamatengo wa siku hizi wameachana na utamaduni huo ingawa bado upo kwa baadhi ya wanafamilia walioshika mila hasa sehemu za vijijini.

Mungu hariri

Egino Ndunguru katika kitabu chake anaonesha kwamba kama ilivyo kwa makabila mengine ya Afrika, Wamatengo wa kale waliamini kuna Mungu na walitumia njia mbalimbali kuwasiliana naye. Walimjua na kumwamini Mungu mweza wa yote aliyeumba vitu vyote.

Pia walitegemea msaada kwa ndugu zao marehemu (mahoka) kwa kuwa waliamini baada ya kuaga dunia wafu walikwenda kukaa karibu na Mungu na hivyo ingekuwa rahisi kwao kumfikishia mola ujumbe kuhusu matatizo yanayowakabili watu waliobaki duniani. Waliamini kuwa Mungu ni muweza wa yote, hivyo ni vyema kumtegemea hasa wakati wa shida ili kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kumtia mtu majaribuni.

Waliapa kwa kutumia jina la Mungu ili kudhihirisha wanachosema ni kweli mbele za haki.

Jando na uchumba hariri

Kijana wa kiume anapobalehe wazazi humshawishi atafute mwenza, humwambia kwa Kimatengo namu henu mpali mwotu gwiono, wakiwa na maana sasa tafuta jiko lako, wewe sasa ni mkubwa kutosha kuoa.

Zama hizo ilikuwa sio rahisi kumpata mchumba kwa sababu wasichana walikuwa hawaruhusiwi kwenda shule wala kukusanyika katika matamasha kama ilivyo sasa.

Hivyo kijana akimwona msichana anayempenda alilazimika kwenda kumwinda kwenye shughuli za matanga, michezo ya ngoma maarufu kwa jina la mhambo na wakati mwingine kijana alilazimika kumtembelea msichana nyumbani kwao na kumwelezea lengo lake.

Kijana wa kiume humpa msichana unyasi, udodi au ushanga kama ishara ya kuomba uchumba, hivyo msichana alikuwa na hiari ya kupokea ama kukataa. Endapo atapokea naye humpa mvulana mojawapo akikubali vitu hivyo kama ishara ya kutokuvunja ahadi ya uchumba huo.

Vijana wanapoingia kwenye kipindi cha uchumba hupata heshima ya kipekee na hivyo ilikuwa mwiko kusalimiana kwa kuwashika mikono, kukaribiana uso kwa uso na walitengwa na kupewa sehemu maalumu ya kukaa kila mmoja sehemu yake hadi siku watakaporuhusiwa kuanza maisha ya ndoa.

Mahari yaliyotolewa kwa familia ya binti ni jembe moja, mbuzi watano na kipande cha nguo cha (mbinda) kwa ajili ya mama mzazi, nguo ambayo hivi sasa inajulikana kama mkaja wa mama. Tofauti na makabila mengine, Wamatengo hawafanyi sherehe yoyote wakati wa kushika uchumba wala siku ya harusi.

Baada ya bwana harusi kukamilisha mahari, shangazi wa bibi harusi humpeleka mwali kwa mchumba wake na kumkabidhi bwana harusi na kuwaruhusu kuanza maisha ya ndoa.

Shangazi alipaswa kuishi na wanandoa hao na kuwaelekeza mambo muhimu katika ndoa. Shangazi alilala chumba kimoja na wanandoa hao na kufuatilia mwenendo wa wanandoa hao wapya ili aweze kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa kama bibi harusi alikutwa na bikira au la.

Hata mabadiliko ya mfumo wa maisha yameondoa baadhi ya vipengele kwani Wamatengo wanafanya sherehe ya harusi na shangazi wa bibi haruhusiwi kuingia chumbani kwa maharusi.

Ikiwa mvulana atamchukua msichana bila kufuata utaratibu kwa Kimatengo (makunja) washenga hupeleka kuku au mbuzi kwa wazazi wa msichana kuwataarifu na baadaye hulipa mahari kwani bila kufanya hivyo mvulana na msichana wanabaki kuwa wachumba na kama mtoto akizaliwa kipindi hicho huwa mali ya wazazi wa msichana.

Wanaume wa Kimatengo walioa mke zaidi ya mmoja kwa kuwa wanapenda kuwa na watoto wengi. Katika tamaduni za Wamatengo mama akiwa mjamzito wa miezi mitatu hutengwa na hukaa nyumba ya peke yake hadi atakapojifungua. Walifanya hivyo kama ishara ya kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kuwa waliamini kuwa mjamzito akijumuika na watu wengine anaweza kupatwa na magonjwa ambukizi, kuangaliwa vibaya na watu au kumkasirisha mama mjamzito.

Mara baada ya kujifungua mama mzazi alitunzwa na mkwe mpaka kitovu cha mtoto kipone. Akishapona hufanyiwa tambiko maalum. Kwanza huogeshwa kwa maji yaliyochanganywa na dawa maarufu kwa jina la mbatabata, kisha hunyolewa na kusubiri taratibu za kutolewa nje.

Siku ya mtoto kutolewa nje mama wa baba wa mtoto hulowanisha mbatabata kisha huchukua dawa nyingine iiitwayo luhamu na kuichomeka juu ya paa la nyasi sehemu ya mlangoni na kusubiri jua lichomoze. Jua linapochomoza mama na mwanae husimama mlangoni kisha mama mkwe humimina maji ya mbatabata juu ya mlango katika nyasi ili matone ya maji hayo yadondoke kwenye utosi wa mtoto.

Wakiwa hapo mlangoni mtoto huelekezwa upande wa mashariki na kisha mzee wa jadi humuombea baraka na kumpatanisha na mwanga wa jua kwa kusema “gutogulanee na lyoba” maana yake upatane na jua kisha huelekezwa magharibi kisha mzee husema “gutogulanee na mwezi” maana yake upatane na mwezi.

Kipindi za uzazi mke hujitenga na mumewe kitendo kinachojulikana kama masegati kwa lugha ya Kimatengo. Mtoto anapofikisha miezi sita hupewa uji maarufu kama ukoba ambao hutengenezwa kwa unga wa ulezi na kinywaji kiiwatcho nimbi ambacho ni togwa ya watoto wachanga. Mtoto akishaanza kula vyakula tofauti ndipo mama yake huruhusiwa kuendelea kukaa chumba kimoja na mumewe.

Malezi hariri

Wamatengo wanawalea watoto katika maadili na kazi, mama kumfunza binti kazi mbalimbali za kilimo pamoja na za nyumbani kama kupika, kuokota kuni, kufua na kufinyanga vyungu. Wanaume wanakutana sehemu inayoitwa pasengu kupeana mawaidha na mafunzo kama jinsi kuchunga na kuwinda.

Msichana anapofikia umri wa kuvunja ungo anamwambia shangazi yake na shangazi huwafikishia wazazi taarifa na kumweka binti ndani kwa muda wa mwezi hadi miezi sita. Baada ya binti kukaa ndani hatua inayofuata anatolewa na kupelekwa porini na wanawake wazee kuchezwa unyago.

Huko anaelezwa maana ya kuvunja ungo, maumbile yake, kuzaa na kulea, heshima kwa watu, kujisitiri kwa mavazi ya heshima na jinsi ya kuishi na mume. Baadaye binti hunyolewa nywele na kubebwa mgongoni kurudishwa nyumbani kwa shangwe, vigelegele na vifijo, akifika nyumbani huketishwa uwanjani ili kila mtu amwone.

Anaimbiwa nyimbo za mafunzo kama huu usemao: na jwakakema ndongu jojo, gwitamaa pahe wakiwa na maana utakapoitwa na mumeo itika kwa adabu. Hupewa zawadi na wale waliofika kumpokea na hufanya sikukuu kubwa ya watu kula na kunywa. Pia wavulana wanapopevuka hukaa kwenye mabweni tofauti yanayoitwa mabwalu ambako husimuliana hadithi na kucheza michezo kama mbila, kinyita, nzengu na unyilii.

Wamatengo wanaamini mtu akifa roho yake huchukuliwa ahera kuishi maisha mengine. Roho hizo huitwa mahoka na huwa na uhusiano na watu wanaoishi duniani. Pia mahoka wasipoheshimiwa hukasirika na kuleta maafa duniani. Kwa kila mwanadamu kifo ni hatua ya mwisho ya maisha ya hapa duniani.Wamatengo kabla ya mauti wanasamehe, kupatana na wagomvi na kulipa madeni.

Burudani za jadi hariri

Kuanzia mwezi Juni mpaka Novemba Wamatengo hujiburudisha na ngoma za asili. Wanaume hupendelea kucheza ngoma ya mganda na mhambo na wanawake hupenda kucheza ngoma aina ya kioda.

Tanbihi hariri

  1. Kurosaki, p.20
  2. Kurosaki, p. 21
  3. "Languages of Tanzania". Ethnologue:Languages of the World. Iliwekwa mnamo 25 Oktoba 2010.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. "Matengo". Joshua Project: A ministry of the U.S. Center for World Mission. Iliwekwa mnamo 2010-10-25.
  5. Kurosaki, p.19
  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wamatengo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.