Bungo-mavi

(Elekezwa kutoka Aphodiinae)
Bungo-mavi
Bungo-mavi akifingirikisha bonge la mavi (Scarabaeus laticollis)
Bungo-mavi akifingirikisha bonge la mavi (Scarabaeus laticollis)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Scarabaeoidea
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Familia 2, nusufamilia 2 za bungo-mavi:

Bungo-mavi au viviringamavi ni mbawakawa wa familia mbili za familia ya juu Scarabaeoidea katika oda Coleoptera: Scarabaeidae na Geotrupidae, ambao hula mavi ya wanyama. Familia hii ya juu ina familia nyingine pia, lakini familia hizi hazina bungo-mavi. Hata Scarabaeidae na Geotrupidae zina spishi zisizo bungo-mavi na zinazokula mizoga, matunda au ubao inayooza.

Maelezo

hariri

Bungo-mavi ni imara wenye mabawa magumu sana ya mbele. Miguu ya mbele ina nguvu mara nyingi na imetoholeka kwa kuchimba. Spishi za nusufamilia Scarabaeinae ni kubwa hadi kubwa sana, mpaka zaidi ya sm 5. Zile za Aphodiinae ni ndogo sana, kwa kawaida china ya sm 1, ilhali zile za Geotrupidae ni katikati.

Lava wa mbawakawa hawa au mabuu ni weupe na wana miguu mifupi. Mwili wao ni mwororo wenye fumbatio nono. Kichwa chao ni ngumu chenye rangi ya nyeusi hadi kahawianyekundu. Hutumia maisha yao ndani ya mavi wanayokula. Kuna hatua tatu za lava zinazofuatwa na bundo.

Ekolojia na mwenendo

hariri

Bungo-mavi huishi katika makazi mengi pamoja na mbuga, savana, jangwa, mashamba na misitu asilia na iliyopandwa. Wanaathiriwa sana na muktadha wa mazingira na hawapendi hali ya hewa baridi au kavu sana. Wanapatikana kwenye mabara yote isipokuwa Antaktiki. Hula mavi ya walamani na ya walachochote na hupendelea yanayotolewa na wale wa mwishoni. Wengi wao pia hula nyoga na majani na matunda yanayooza. Spishi moja inayoishi Amerika ya Kati, Deltochilum valgum, ni mgwizi anayewinda majongoo. Siyo lazima bungo-mavi wakule au kunywa kitu kingine chochote, kwa sababu mavi hupeana virutubishi vyote muhimu.

Bungo-mavi wanaainishwa katika aina tatu za kazi kulingana na mikakati yao ya kujilisha na kutaga kama vile “wafingirikishaji”, “wachimbaji” na “wakazi”. Wafingirikishaji hufingirikisha na kuzika bonge la mavi au kwa uhifadhi wa chakula ama kwa kutengeneza bonge la kutagia. Wachimbaji huchimba vishimo chini ya pedi ya mavi, kuvuta mavi chini na kutaga ndani yake. Kwa upande mwingine, wakazi hawachimbi lakini wanaishi na kutaga ndani ya pedi ya mavi.

Kwa kisa cha wafingirikishaji, bungo mmoja wa kiume na mmoja wa kike hukaa karibu na bonge la mavi wakati wa mchakato wa kufingirikisha. Kwa kawaida ni dume anayefingirikisha bonge, wakati jike huchukua lifti au kufuata nyuma tu. Kwa visa vingine dume na jike hufingirikisha pamoja. Wakipata mahali penye udongo laini, wanasimama na kuzika bonge, kisha wanapandana chini ya ardhi. Baadaye, jike hutaga mayai ndani yake, aina ya uandalizi kwa wengi. Spishi fulani haziondoki baada ya hatua hii, lakini zinabaki kulinda uzao wao.

Bungo-mavi wengi hutafuta mavi kwa kutumia hisi yao nyeti ya harufu. Spishi fulani ndogo hujinata kwa watoa mavi na kuyangoja. Baada ya kutengeneza bonge bungo hulifingirikisha akifuatia mstari nyofu licha ya vikwazo vyote. Wakati mwingine, bungo-mavi hujaribu kuibia bungo mwingine bonge la mavi lake. Kwa hivyo bungo-mavi hulazimika kuhama haraka kutoka kwa rundo la mavi mara tu wamesokota bonge lao ili kuzuia lisiibwe. Bungo-mavi wanaweza kufingirikisha hadi mara 10 uzito wao. Madume ya bungo Onthophagus taurus wanaweza kuvuta mara 1,141 uzito wao wenyewe wa mwili: sawa na mtu wa kawaida akivuta mabasi sita ya ghorofa yaliyojaa watu.

Spishi moja ya bungo-mavi, Scarabaeus zambesianus wa Afrika, huabiri kwa ruwaza ya mbinikizo katika mwanga wa mwezi, mnyama wa kwanza anayejulikana kufanya hivyo. Bungo-mavi pia wanaweza kuabiri wakati Njia Nyeupe au vishada vya nyota nyangavu zinaonekana tu, ambayo inawafanya wadudu wa pekee wanaojulikana ambao wanajua wapo wapi kwa njia ya Njia Nyeupe.

Manufaa na utumiaji

hariri

Bungo-mavi huwa na daraka katika kilimo na misitu ya kitropiki. Kwa kuzika na kula mavi, huboresha urejelezaji wa virutubishi na muundo wa udongo. Bungo-mavi wameonyeshwa aidha kuboresha hali ya udongo na ukuaji wa mimea kwenye migodi ya makaa mawe iliyorekebishwa nchini Afrika Kusini. Wao ni muhimu pia kwa utawanyaji wa mbegu zilizopo kwenye mavi ya wanyama, wakiathiri kuzikwa kwa mbegu na ugavi wa miche katika misitu ya kitropiki. Wanaweza kukinga mifugo, kama vile ng'ombe, kwa kuondoa mavi ambayo, yakiachwa, yanaweza kuwapatia wadudu kama nzi makazi. Katika nchi zinazoendelea bungo hawa ni muhimu mno kama kiambatisho cha kuboresha viwango vya afya. Na hata huko Marekani, Taasisi ya Marekani ya Sayansi ya Biolojia (American Institute of Biological Sciences) inaripoti kwamba bungo-mavi huokoa tasnia ya ng'ombe takriban dola milioni 380 za Kimarekani kila mwaka kwa kuzika mavi ya mifugo yaliyopo juu ya ardhi.

Huko Australia, Shirika la Utafiti wa Kisayansi na wa Kiwanda wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Scientific and Industrial Research Organization au CSIRO) iliagiza Mradi wa Bungo-mavi wa Australia (1965-1985) ambao ulitaka kuingiza spishi za bungo-mavi kutoka Afrika Kusini na Ulaya. Spishi 23 ziliingizwa kwa ufanisi, haswa Digitonthophagus gazella na Euoniticellus intermedius, ambayo imesababisha uboreshaji wa ubora na rutuba ya machungani ya ng'ombe ya Australia, pamoja na upungufu wa idadi ya nzi wasumbufu wa porini kwa karibu na asilimia 90.

D. gazella aliingizwa katika maeneo kadhaa ya Amerika ya Kaskazini na ya Kusini na ameongeza msambao wake kwenye maeneo mengine kwa fumukano asilia na usafirishaji kwa bahati mbaya, na labda amekuwa kawaida katika karibu nchi zote kati ya Meksiko na Argentina. Spishi za kigeni zinaweza kuwa muhimu kwa kudhibiti magonjwa ya mifugo katika maeneo ya biashara, na zinaweza kuweka kando spishi za asili katika maeneo yaliyobadilishwa. Hata hivyo data si kamili juu ya athari yao kwa spishi za asili katika mazingira asilia na ufuatiliaji zaidi inahitajika.

Bungo-mavi wa Bahari ya Mediteranea (Bubas bison) wametumiwa pamoja na lishe ya bio-makaa ili kupunguza utoaji wa oksidi nitrasi na oksidi kaboni, ambazo zote mbili ni gesijoto. Bungo huzika mavi yaliyoimarishwa kwa bio-makaa ndani ya udongo bila kutumia mashine.

Spishi zilizochaguliwa za Afrika ya Mashariki

hariri
  • Allogymnopleurus indigaceous
  • Catharsius heros
  • Copris denticulatus
  • Euoniticellus parvus
  • Gymnopleurus laevicollis
  • Gymnopleurus reichei
  • Heliocopris dilloni
  • Kheper aegyptiorum
  • Kheper platynotus
  • Oniticellus egregius
  • Oniticellus pseudoplanatus
  • Onthophagus gibbus
  • Onthophagus graphicus
  • Scarabaeus catenatus
  • Scarabaeus laevistriatus
  • Sisyphus tibialis