Mto Brahmaputra
Brahmaputra (Tsangpo ndani ya China) ni jina la mto unaoanza nchini Tibet (China) na kupita Uhindi. Nchini Bangla Desh unaungana na mto Ganges kilomita 150 kabla ya mdomo wa pamoja inapoishia katika Ghuba ya Bengali. Ni kati ya mito mikubwa ya Asia ukiwa na urefu wa kilomita 2,900.
Chanzo cha Brahmaputra ni barafuto ya Chemayungdung kwenye mitelemko ya Himalaya katika nchi ya Tibet[1].
Sehemu ya kwanza ya njia yake iko katika nyanda za juu za Tibet inapoelekea kutoka mashariki kwenda magharibi. Hapa inaitwa Tsangpo au Zangpo. Baada ya kilomita 1,500 hivi njia inapinda kwenda kusini. Inapita safu za Himalaya kupitia mabonde makali na kuingia katika jimbo la Arunachal Pradesh nchini Uhindi.
Njia yake inapinda tena kuelekea magharibi katika bonde la Assam. Baada ya kilomita 600 hivi inapinda tena na kuelekea kusini inapoingia Bangla Desh. Hapa mto unajigawa; mkono mkubwa unaitwa Padma na kuungana na mto Ganges. Mkono mdogo zaidi unaendelea kuitwa Brahmaputra (kwa Kibengali: Brommoputro) na kuishia katika Mto Meghna unaoendelea kujiunga baadaye na Padma. Mto wote unaishia kwenye Ghuba ya Bengali (sehemu ya Bahari Hindi) kupitia delta kubwa. Delta hiyo huitwa mara nyingi delta ya Ganges au delta ya Brahmaputra-Ganges.
Mkondo wa Brahmaputra unasafirisha kiasi kikubwa cha maji kinachopitiwa tu na Amazonas na Kongo. Kwa wastani ni mita ya mjazo 19,800 kwa sekunde lakini baada ya kuyeyuka kwa theluji kwenye milima ya Himalaya mkondo unaweza kuongezeka hadi 100,000 m3/s. Hii inasababisha mara kwa mara mafuriko makubwa hasa nchini Bangla Desh.
Tanbihi
hariri- ↑ "The Course of River Brahmaputra (Tsangpo-Brahmaputra)". ImportantIndia.com. 21 Agosti 2013. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-07-27. Iliwekwa mnamo 2019-09-18.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)
Viungo vya Nje
hariri- http://www.mapsofindia.com/maps/rivers/brahmaputra.html - Brahmaputra River Map