Izyira ni kata ya Wilaya ya Mbeya Vijijini katika Mkoa wa Mbeya, Tanzania yenye msimbo wa posta namba 53229 [1].

Katika sensa iliyofanyika mwaka 2022 wakazi walihesabika kuwa 6,260 [2]. Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, idadi ya wakazi wa kata ilikadiriwa kuwa watu 6,620.[3]

Kijiji cha Izyira kimepewa hadhi ya kuwa kata inayojitegemea mwaka 2014 baada ya kugawa kata ya Iwiji. Kata ya Izyira ina jumla ya vitongoji vinne ambavyo ni Izyira, Masewe, Inuka na Mapita ikiwa ni kijiji kilichotokea baada ya kugawa kijiji cha Izyira.

Jiografia hariri

Kijiji hicho kinapakana na Ibezya, kijiji cha wilaya ya Ileje kusini mashariki, huku kusini kikipakana na Wilaya ya Mbozi, vijiji vya Hezya na Namwangwa, na kuendelea mpaka magharibi kijiji cha Haraka na Idiwili; magharibi kuna Mlima Mwira; kaskazini kuna kijiji cha Iwiji na safu ya milima Mbeye na kaskazini magharibi mlima Makungulu iliyoambatana na msitu Mang'onga na msitu Mbogho. Misitu hiyo minene ni muhimu kwa kuwa ndicho chanzo kikuu cha mito mitatu ambayo ni Mto Magole, Mto Salaga na Mto Mafumbo. Mito hiyo inashikilia asilimia 85 ya kilimo cha umwagiliaji wa ukanda wa vijiji vyote vilivyovitajwa hapo juu kuwa jirani ya Izyira.

Mito hiyo mitatu hupitia kijiji hicho: mto Magole upo mashariki, sambamba na kijito kidogo kiitwacho Itaga, katikati kuna kijito kingine Salaga, magharibi kuna mto mkubwa Mafumbo na magharibi kuna kijito kingine Shongo. Mito yote hii ndiyo chanzo kikuu cha uzalishaji wa chakula cha wakazi wa kijiji cha Izyira na vijiji vya jirani. Mito hiyo mkubwa miwili, yaani Magole na Mafumbo, ikisaidiana na vijito hivyo hutiririsha maji mwaka mzima. Muungano wa mito hiyo miwili hufanya mto mmoja unaokwenda kusini kupitia karibu sana na Itumba kuungana na mto Songwe ulio kama mpaka wa Tanzania na Malawi.

Kutokana na ongezeko la watu katika misitu hiyo miaka ya karibuni kumekuwa na uharibifu mkubwa na kusababisha mito hii kupungua sana tena sana kwa ujazo wa maji na kusababisha kupungua kwa kiwango cha unyeshaji wa mvua. Kama hakutakuwa na mkakati wa kuzuia uharibifu huu wa misitu hiyo upo uwezekano wa mito kukauka na kusababisha hali mbaya kwa vijiji vyote vinavyopata huduma ya maji ya mito hiyo.

Izyira inahudumiwa na barabara kuu kutoka Mbalizi ikipitia vijiji vifuatavyo: Mbalizi, Izumbwe I, Mganjo, Isangati Santilya, Shipongo, Ilembo, Italazya, Shigamba, Izumbwe II. Iwiji barabara inagawanyika, kushoto inakwenda makao makuu ya Wilaya ya Ileje yaani Itumba na kulia barabara hii ndiyo inakwenda moja kwa moja Izyira hatimaye huendelea Wilaya ya Mbozi kupitia vijiji vya Hezya, Nyimbili, Ilengo, Shumba, Hasamba na kuungana tena na barabara kuu ya Dar es Salaam mpaka Zambia pale makao mkuu ya Wilaya ya Mbozi.


Watu hariri

Izyira hukaliwa na makabila matatu ya Wanyiha, Wandali na Wamalila. Kijiji hicho kina mila na desturi zake kikiongozwa na mila za jadi. Kiongozi akiitwa mwene wa ukoo wa Mwazembe.

Chakula chao kikuu kinatokana na mazao yaani mahindi, ndizi na viazi vitamu. Zao la biashara ni kahawa.

Kati ya Wakristo kuna hasa madhehebu yaliyo kwenye jumuiya ya CCT.

Huduma za kijamii hariri

Kijiji hiki kina shule tatu. Izyira ni shule mama iliyoanzishwa mnamo 1957 kwa mfumo wa shule za TAPA iliyoanza na mwalimu mzawa Winfred Mtindo Mwazembe; baadaye zilianzishwa shule mbili kutokana na ongezeko la watu ambazo ni Mwenge na shule ya msingi Masewe. Pia wananchi katika mfumo wa kila kata kujenga shule ya sekondari kijiji kama kijiji walijenga shule ya sekondari ya kijiji kwa mpango wa kujitolea pamoja na kuwa na shule ya sekondari ya kata ambayo ipo makao ya kata pale Iwiji; pia tarehe 29 Arili 2009 shule ya sekondari ilifunguliwa katika kijiji cha Izyira chini ya mkuu wa shule Godlove Ngonde.

Kijiji hiki, pamoja na kuwa na vitongoji kumi, kinahudumiwa na zahanati moja tu. Uongozi wa wilaya ya Mbeya umeona kuwa ni vyema kujenga kituo cha afya katika kata hii; kama ujenzi huu utakamilika utakuwa msaada mkubwa kwa ukanda huu wa kusini mwa wilaya ya Mbeya vijijini kwa sababu kata hii wananchi wake walikuwa wanapata shida sana, hasa akina mama na watoto wanapohitaji huduma ya matibabu ilikuwa inawalazimu kusafiri umbali mrefu kwani iliwalazimu kwenda wilaya ya Ileje, ama kwenda hospitali ya Mkoa wa Songwe ambayo zamani ilikuwa hospitali ya wilaya ya Mbozi katika mji wa Vwawa ama hospitali ya binafsi ya Mbozi mission.

Kituo hiki kinajengwa kwa nguvu za wananchi na mpaka sasa kipo hatua ya kujenga msingi asilimia kubwa ya ujenzi wa kituo hiki ni nguvu za wananchi kwa kuwa hujitolea matofali, mawe, mchanga na mafundi. Kituo hiki kinajengwa katika eneo la kitongoji cha Inuka ambalo lina historia yake, pamoja na kuwa katikati ya kata ya Izyira. Eneo hili ndipo ilipoanzishwa shule ya kwanza kabisa kabla hata nchi hii haijapata uhuru yapata miaka 70 iliyopita, hivyo ni jambo la busara kwa uamuzi uliotolewa kulienzi eneo hilo japo watu wengi hawajui nini maana ya kujenga kituo katika eneo hilo.

Marejeo hariri

  Kata za Wilaya ya Mbeya VijijiniMkoa wa Mbeya - Tanzania  

Bonde la Songwe | Igale | Igoma | Ihango | Ijombe | Ikukwa | Ilembo | Ilungu | Inyala | Isuto | Itawa | Itewe | Iwiji | Iwindi | Iyunga Mapinduzi | Izyira | Lwanjilo | Maendeleo | Mjele | Masoko | Mshewe | Nsalala | Santilya | Shizuvi | Swaya | Tembela | Ulenje | Utengule/Usongwe


  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mbeya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Izyira kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.