Mbozi

(Elekezwa kutoka Wilaya ya Mbozi)

Wilaya ya Mbozi ni wilaya mojawapo ya Mkoa wa Songwe. Eneo la wilaya ni kilomita za mraba 3440.

Mahali pa Mbozi (kijani) katika mkoa wa Mbeya.

Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 515,270. Baada ya kutenga maeneo ya wilaya mpya ya Momba ambayo ina Halmashauri za miji ya Tunduma na Momba 2012/13, Mbozi kwa sasa kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya 2022 ina jumla ya watu 510,599 hii ikiwa ni sawa na asilimia 40% ya wakazi wote wa mkoa wa Songwe ambao kwa takwimu hizo ni 1,344,687.

WakaziEdit

Wakazi ni hasa Wanyiha, Wakinga, Wanyakyusa, Wandali na Wanyamwanga. Wanyiha ni takriban nusu ya wakazi wa wilaya wakikalia nyanda za juu. Wanyamwanga ni takriban asilimia 10 za wakazi wakikaa kwenye ukanda wa chini kata za Nambinzo, Isalalo na Ipunga. Makabila mengine ni pamoja na Wawanda, Walambya, Wamalila na Wasafwa. Katika miaka ya mwisho Wamasai na Wasukuma wamehamia wilayani. Pato la wananchi wa mkoa wa Songwe kwa sehemu kubwa linabebwa na Halmashauri ya Mbozi kupitia zao la Kahawa ambalo kwa mwaka huuingizia mkoa zaidi ya Trilioni 1.3 na pato kwa mtu mmoja mmoja kwa mkoa wa Songwe ni 2.23Milioni ukiwa mkoa wa 19 kitaifa, kwa wilaya ya Mbozi pato lake ni wastani wa 2.5 Milioni

EneoEdit

 
Kimondo cha Mbozi

Eneo la wilaya liko katika kimo cha mita 1500-2750 juu ya usawa wa bahari. Nyanda za juu ni maeneo ya Iyula, Vwawa, Igamba na Ndalambo, yana ardhi nyekundu.

Kimondo cha Mbozi, ambacho ni maarufu duniani kama kimondo kikubwa cha chuma, si mbali na misioni ya Mbozi. Kimondo hicho kina uzito unaokadiriwa kuwa tani 12.

Mbozi Mission ndipo mche wa kwanza wa zao la kahawa ulipopandwa mwaka 1902 na wamisionari Wamoravian kutoka Ujerumani na baadaye kuenea katika maeneo mengi ya nyanda za juu za wilaya ya Mbozi, kituo cha kwanza cha ununuzi wa kahawa kilijengwa eneo la Igamba jirani na ilipo mahakama ya Mjerumani kwenye eneo la mwene Nzowa.

Maliasili na visukuku katika eneo la MagambaEdit

Katika kijiji cha Magamba, kilichopo kata ya Isansa, kumegunduliwa makaa ya mawe hazina ya zaidi ya tani milioni 52, ambapo wakoloni Waingereza walifanya majaribio ya makaa hayo mwaka 1934 kuendeshea garimoshi na katika kufua umeme kwenye kituo cha umeme Mombasa mwaka 1935.

Eneo hilo limepata umaarufu zaidi baada ya kupatikana kwa visukuku vya mifupa ya mijusi mikubwa ya kale (dinosauri) kando ya kijito Mahoma. Profesa Patrick O'Connor wa Chuo kikuu cha Ohio nchini Marekani amekuwa akifanya utafiti tangu mwaka 2002 ambapo ameweza kugundua mabaki hayo.

O'Connor anasema baadhi ya mifupa aliyogundua inadhihirisha kuwepo kwa dinosauri wadogo chini ya futi moja walioishi duniani hapa miaka milioni 100 iliyopita. Mifupa ya dinosauri inaonesha mnyama huyo alikuwa mkubwa na uzito wa zaidi ya tani 40. (Hayo yamo katika mahojiano kati ya Kenneth Mwazembe na Prof. O'Connor yaliyofanyika Julai 2008 kijijini Magamba)

Katika kijiji cha Nkangamo kata ya Nkangamo tarafa ya Ndalambo kuna miamba yenye michoro ya kale inayokadiriwa kuchorwa miaka 3000 iliyopita. Katika eneo hilo pia kuna jiwe au mwamba wenye wayo wa binadamu unaoonekana kukanyagwa kabla jiwe halijawa gumu. Kwa bahati mbaya Idara ya Mambo ya Kale haijafuatilia habari hizo.

Katika Wilaya ya Mbozi imegunduliwa kuwepo kwa dhahabu maeneo ya Idiwili na Shidunda, jirani na kimondo cha Mbozi. Pia eneo la Magamba inapopakana na wilaya ya Chunya ni ukanda wa dhahabu unaohitaji wataalamu kufanya utafiti zaidi ili kujua wingi wa dhahabu iliyopo katika maeneo hayo.

Kwa upande wa kijiji cha Magamba mpakani na Chunya kumeonekana dalili za kuwepo kwa mafuta ya petroli hasa kwenye machimbo ya mkaa wa mawe ambao upo kiasi cha mita moja kutoka usawa wa ardhi. Kwa sasa kampuni ya Magamba Coal Mine au Troll Mining Company inayomilikiwa na jenerali mstaafu Robert Mboma inawekeza/kuvuna makaa hayo. Hao wawekezaji wanapaswa kujenga mitambo ya kufua umeme wa makaa ili uwepo wao huko uwe kwa faida ya Watanzania wote.

MijiEdit

Miji wilayani ni Mlowo, penye viwanda vya kahawa vitatu vya GDM, Mbozi MCCO na LIMA (watu 37,000-50,000). Aidha Vwawa ndiko makao makuu ya wilaya ambapo idadi ya wakazi wake ni zaidi ya 60,000. Miji mingine miwili iko kando ya barabara kuu ya TANZAM kutoka Dar es Salaam kupitia Mbeya kwenda Zambia.

Reli ya TAZARA inapita vilevile wilayani na kuna vituo huko Vwawa na Tunduma.

UtawalaEdit

Katika wilaya hii kuna kata 29 za Vwawa, Mlowo, Ihanda, Ukwile, Ipunga, Kilimampimbi, Isalalo, Msia, Ruanda, Mahenje, Nanyala, Iyula, Hezya na Nyimbili. Nyingine ni Ichenjezya, Ilolo, Hasanga, Igamba, Nambinzo, Itaka Halungu, Isansa, Itumpi, Shiwinga, Mlowo, Magamba, Mlangali na Bara.

Misioni ya Moravian MboziEdit

Kitovu cha kihistoria kilikuwa kijiji cha Mbozi penye kituo cha misioni cha Moravian pamoja na hospitali na shule ya sekondari. Kituo kilianzishwa mwaka 1899 na mmisionari Mjerumani, Traugott Bachmann. Bachmann aliyejipa jina la wenyeji la Mwalwizi alichagua mahali pa misioni kwa sababu palikuwa mpakani wa maeneo ya Nzova na Mwasenga waliokuwa machifu muhimu wa Wanyiha.

Asili ya jina la MboziEdit

Asili ya jina Mbozi linatokana na dawa za asili zilizotengenezwa yaani majani ya miti yanachumwa kisha hutwanga kwenye kinu na kuongezewa maji kidogo kisha huchujwa na kupewa mgonjwa. Wanyiha huita dawa hiyo Mbozyo lakini Wazungu walishindwa kutamka Mbozyo wakasema Mbozi.

Viungo vya NjeEdit

  Kata za Wilaya ya Mbozi - Mkoa wa Songwe - Tanzania  

Bara | Halungu | Hasamba | Hasanga | Hezya | Ichenjezya | Idiwili | Igamba | Ihanda | Ilolo | Ipunga | Isandula | Isansa | Itaka | Itumpi | Iyula | Kilimampimbi | Magamba | Mlangali | Mlowo | Msia | Myovizi | Nambinzo | Nanyala | Nyimbili | Ruanda | Shiwinga | Vwawa | Wasa


  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Songwe bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mbozi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari .
Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno