Kikosi cha wapagazi

Kikosi cha wapagazi (kwa Kiingereza Carrier Corps) kilikuwa kitengo cha jeshi la Uingereza wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Kiliujumuisha wapagazi Waafrika walioajiriwa au kulazimishwa kubeba mizigo ya jeshi la Uingereza kwenye mapigano ya Vita Kuu ya Kwanza katika Afrika ya Mashariki dhidi jeshi la Wajerumani lililoongozwa na Paul von Lettow-Vorbeck.

Kumbukumbu ya wapagazi Waingereza kwenye Sanamu ya Askari, Dar es Salaam
Wapagazi Waafrika upande wa jeshi la Schutztruppe

Waingereza walikuwa na tatizo kusafirisha chakula, risasi na mahitaji mengine kwa ajili ya jeshi kubwa katika maeneo pasipo barabara wala reli.

Jeshi la kikoloni la Uingereza lilitumia wanejeshi Waingereza, Wahindi na Wazungu wa Afrika Kusini hasa miaka ya kwanza ya vita. Wanajeshi hao walizoea kusafiri na kiwango cha mzigo wa binafsi.

Kinyume chake kamanda Mjerumani von Lettow-Vorbeck aliwahi kuandaa jeshi la askari Waafrika walioweza kutumia vyakula vilivyopatikana hata porini na wasiozoea kuwa na mizigo mingi. Hao askari wazalendo walikuwa sehemu kubwa ya jeshi la Schutztruppe la Wajerumani katika Afrika ya Mashariki. Kwa hiyo Wajerumani walitumia wapagazi wachache kuliko Waingereza ingawa hata wao waliajiri au kulazimisha Waafrika kufanya kazi hii kwa ajili ya mahitaji yao.

Upande wa Waingereza wanajeshi wao hawakuzoea vyakula vya mahali. Kwa hiyo kazi ya kusafirisha kilogramu 1 ya mchele kutoka bandari za pwani hadi kufikia wanajeshi barani ilihitaji mara nyingi kilogramu 50 za mchele zilizohitajika kulisha wapagazi waliobeba akiba.

Kwa kazi hii kubwa utawala wa kikoloni wa Waingereza ulianzisha kitengo cha pekee kilichoitwa "Carrier Corps". Ilitumia takriban wanaume 400,000 Waafrika kwa kazi zake, na katika muda wa vita kwa jumla Waafrika takriban milioni 1 walikuwa sehemu ya kikosi cha wapagazi upande wa Uingereza.

Imekadiriwa ya kwamba angalau 95,000 kati ya hao walikufa, wengi kutokana na njaa na magonjwa[1]. Usimamizi wa kazi ya kujenga kikosi hiki kilikuwa chini ya Mwingereza Oscar Ferris Watkins aliyewahi kufika Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (yaani Kenya) kama mtawala wa kikoloni mwenye cheo cha mkuu wa wilaya.

Kuna kumbukumbu ya wapagazi mahali mbalimbali kama vile

Miji mingi ya Afrika Mashariki ina sehemu zinazoitwa kwa majina kama "Kariakoo" kama Dar es Salaam na Dodoma au "Kariakor" huko Nairobi. Ni mahali ambapo wapagazi waliostaafu katika kikosi cha wapagazi walijenga nyumba zao.

Marejeo hariri

  1. "World war casualties were colossal, na Batumuraki Musingizi, East African Friday, March 13  2015". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-03-21. Iliwekwa mnamo 2015-03-27. 

Tazama pia hariri

Kujisomea hariri