Mpaka ni sehemu ambako kitu kinafikia mwisho wake. Mara nyingi neno hutumiwa kutaja mwisho wa eneo fulani, kama vile kiwanja, shamba au nchi.

Geti la kuvuka mpaka baina ya Togo na Benin.
Mpaka baina ya Berlin Mashariki na Berlin Magharibi hadi mwaka 1990.
Mpaka usio na vizuizi baina ya Austria na Ujerumani ndani ya Umoja wa Ulaya.

Vieneo vya hisabati huwa pia na mpaka, kama vile maumbo ya kijiometria (mraba, duara) au seti. Vipindi vya wakati huwa na mpaka vilevile.

Mpaka wa nchi

hariri

Katika karne zilizopita eneo lote la Dunia (isipokuwa Antaktiki) limegawiwa kati ya nchi zinazotenganishwa kwa mipaka inayofafanuliwa. Hali hii haikuwa kawaida katika sehemu kubwa ya historia ya binadamu.

Mipaka inaweza kufuata vizuizi asilia kama vile mito, safu za milima, jangwa au bahari. Katika nchi nyingi kuna tatizo kwamba mipaka ilikubaliwa kisiasa bila kujali hali ya watu katika eneo fulani; hivyo makabila mengi katika Afrika yametenganishwa kwa mipaka iiyochorwa wakati wa ukoloni. Lakini tatizo hili linapatikana pia Ulaya, Asia na Amerika.

Kwa mipaka mingi kuna masharti fulani kama watu wanataka kuipita kama vile kuwa na pasipoti au kibali cha viza.