Mshumaa wa Pasaka au Mshumaa mkuu ni mshumaa maalumu unaotumika katika liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa magharibi kama kiwakilishi cha Yesu mfufuka.

Shemasi akiimba mbiu ya Pasaka Exultet karibu na mshumaa wa Pasaka.
Mishumaa mbalimbali ya Pasaka huko Uholanzi.

Mshumaa mpya wa namna hiyo unabarikiwa na kuwashwa kila mwaka katika kesha la usiku wa Pasaka, halafu unawashwa wakati wa maadhimisho mbalimbali, kama vile yale muhimu zaidi ya Kipindi cha Pasaka (hadi Pentekoste) na hata nje yake, kwa mfano wakati wa ubatizo na mazishi ya Kikristo.

Unatakiwa kuwa mkubwa kuliko mishumaa ya kawaida na uweze kudumu hadi Pasaka ya mwaka unaofuata.

Kwa kawaida unachorwa alama mbalimbali, hasa msalaba wa Yesu na herufi za Kigiriki Alfa na Omega, ambazo ni ya kwanza na ya mwisho katika alfabeti ya lugha hiyo ya Agano Jipya, na hivyo zinamaanisha kuwa Kristo ni mwanzo (asili) na mwisho (lengo) wa ulimwengu wote.

Baada ya kuwashwa kwenye moto wa Pasaka, mshumaa huo unapelekwa kwa maandamano hadi mimbarini, na wakati huo waamini wanawasha kwake mishumaa yao binafsi ili kumaanisha kwamba wameshirikishwa mwanga wa Kristo na kumfuata.

Viungo vya nje

hariri

  "Paschal Candle". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.