Msikiti wa Sultan Ahmed
Msikiti wa Sultan Ahmed ni msikiti mashuhuri mjini Istanbul katika nchi ya Uturuki. Inajulikana pia kwa jina la "msikiti buluu" kutokana na rangi ya vigae vinavyopamba undani wake.
Msikiti huu ulijengwa kuanzia mwaka 1609 - 1616 kwa maagizo ya Sultani Ahmed I aliyetawala milki ya Osmani.
Ni msikiti mkuu wa Istanbul ukihesabiwa kati ya majengo mazuri na muhimu ya usanifu wa Kiosmani.
Muundo wa jengo
haririMsanifu wake Mehmet Agha alikuwa mwanafunzi wa Mimar Sinan. Aliiga mfumo wake wa kimsingi akifunika ukumbi mkuu wa kati kwa kuba kubwa, na kando yake akaongeza kuba ndogo 6.
Ukumbi mkuu una umbo ambalo unakaribia mraba akiwa na mita 53 x 51. Kuba kubwa una kipenyo cha mita 23.5 na kufikia kina cha mita 43. Kuba kubwa linashikwa kwa tao nne zinazolala juu ya nguzo nene nne zenye kipenyo cha mita 5.
Ukumbi unapokea mwanga kwa madirisha 260 yenye vioo vya rangi.
Msikiti huo, yaani jengo la ibada, ulijengwa pamoja na majengo ya kando kama vile madrasa, hospitali na kaburi la sultani Ahmed I.
Geti kuu upande wa magharibi lina nyororo nzito juu ya nafasi ya kuingia. Kusudi lake lilikuwa kumlazimisha sultani kuinama kichwa chini akiingia msikitini juu ya farasi yake. Nyororo hii ilikuwa na kazi ya kuonyesha ya kwamba Mungu ni mkubwa kuliko mtawala.
Minara
haririMsikiti huu una minara sita. Wakati wa ujenzi hii ilileta matatizo maana wakati ule msikiti wa Kaaba mjini Makka pekee ulikuwa na minara sita. Kwa hiyo sultani alishtakiwa kuonyesha majivuno makubwa mno akiupa msikiti wake minara sawa na Makka. Kwa hiyo sultani Ahmed I aliagiza mnara wa saba uongezwe huko Makk.[1]
Historia ya ujenzi
haririSultan Ahmed I aliamua kujenga msikiti huu kama jengo la toba baada ya kushindwa katika vita dhidi ya Dola Takatifu la Roma (Ujerumani-Austria). Mwaka 1606 Milki ya Osmani ilipaswa kukubali amani iliyomaliza malipo ya kila mwaka yaliyowahi kutolewa na kaisari wa Vienna.
Vita dhidi ya Uajemi iliyoanza baadaye ilienda pia vibaya na mwaka 1612 Waosmani walipaswa kurudishwa maeneo ya Kaukazi kwa Waajemi.
Ahmed aliamua kujenga msikiti wake karibu na Hagia Sofia (maabadi yaliyowahi kuwa kanisa kuu la Konstantinopoli na kubadilishwa kuwa msikiti baada ya uvamizi wa Waturuki) na juu ya mabaki ya ikulu ya makaisari wa Bizanti na pia juu ya sehemu ya uwanja wa shindano la farasi wa Bizanti.[2]
Picha
hariri-
Filamu fupi ionyeshayo msikiti buluu.
-
The Blue Mosque.
-
Msikiti wa Sultan Ahmed jinsi inavyoonekana kutoka upande wa Hagia Sofia
-
Uwanja mbele ya geti
-
Sala ndani ya msikiti
-
Vigae vya buluu
-
GEti kwenda uwanja wa ndani
-
Uwanja wa ndani
-
sehemu pa kusali
-
Kuba kuu lenye vigae vya buluu
-
Tao za uwanja wa ndani
-
Watalii wakitazama msikiti
-
Undani wa jengo
-
Msikiti
Tanbihi
hariri- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-10-13. Iliwekwa mnamo 2014-07-29.
- ↑ http://www.bluemosque.co/history.html
Marejeo
hariri- Goodwin G., "A History of Ottoman Architecture"; Thames & Hudson Ltd., London, reprinted 2003; ISBN 0-500-27429-0
- Turner, J. (ed.) - Grove Dictionary of Art - Oxford University Press, USA; New edition (January 2, 1996); ISBN 0-19-517068-7
- Sheila S. Blair, Jonathan M. Bloom - "The Art and Architecture of Islam, 1250-1800", Yale University Press, 1994; ISBN 0-300-05888-8
Viungo vya Nje
hariri- http://www.bluemosque.co / Website About Blue Mosque - Istanbul
- Virtual tour inside Sultan Ahmed Mosque Ilihifadhiwa 23 Juni 2012 kwenye Wayback Machine.
- Virtual tour inside Sultan Ahmed Mosque (3D panoramas)
- Video of Sultan Ahmend Mosque at dawn call to prayer Ilihifadhiwa 13 Juni 2011 kwenye Wayback Machine.
Makala kuhusu msikiti au sehemu nyingine za kuabudia Waislamu bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |