Ndembezi (Igunga)
Ndembezi ni kata ya Wilaya ya Igunga katika Mkoa wa Tabora, Tanzania yenye postikodi namba 45621.
Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa 7,961 [1]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 12,724 waishio humo.[2]
Wakazi wengi wa kata hii ni Wanyamwezi na Wasukuma, pia kuna makabila ya Wanyiramba, Wanyaturu na Waarabu wachache.
Utamaduni
haririWenyeji wa kata hii ni waumini wa dini ya Kikristo, Kiislamu na dini za jadi. Kuna misikiti mitatu, makanisa tisa ya madhehebu tofauti ya Kikristo na maeneo matatu ya matambiko ya dini yajulikanayo kama Mazimbo.
Ndembezi ni maarufu kwa uzalishaji wa zao la mpunga. Wakazi wake ni hodari kwa kilimo, ufugaji, uvuvi na upakuaji asali.
Wenyeji ni wakarimu sana ambapo katika kipindi cha mavuno hupenda kubadilishana zawadi, hasa maboga, karanga, kunde na mboga za majani aina ya mlenda, mswalu, na mgagani.
Chakula kikuu cha wakazi wa kata hii ni ugali ukiambatana na mboga tofautitofauti kama vile dagaa, nyama, kisamvu, mlenda, na mboga nyinginezo zinazopendelewa mkoani Tabora.
Burudani
haririMara baada ya msimu wa mavuno kwisha, wakazi wa kata hii huingia katika msimu wa burudani kuanzia mwezi Juni hadi Septemba ambapo burudani kuu huwa ngoma za jadi maarufu kwa jina la Pubha (Beni) na Hiyali. Ngoma hizo hushirikisha pande mbili pinzani ambapo kila upande huimba na kucheza huku Manju wao akifanya michezo mbalimbali juu ya uchanja ili kuvutia watazamaji upande wake. Pande hizo pinzani huitwa Wazubha na Wagika; wakati mwingine pia hushirikisha ngoma ya tatu ijulikanayo kama Wayeye. Upande utakaovutia watu wengi ndio huwa mshindi na hupata zawadi mbalimbali hasa ng'ombe na mazao. Ndembezi ina wasanii wengi wa ngoma za jadi, miongoni mwao wapo Gwesa, Ng'wanidako na Tuma.
Ndembezi pia kuna timu za mpira wa miguu kama vile Ndembezi Rangers, Ndembezi Stars na timu za shule za msingi na sekondari. Miongoni mwa wachezaji waliopata kuwika katani hapo ni: Rajabu Bakari, Juma Bakari, Ramadhani Ndolaga, Abdallah Abu na Fundi Hamisi.
Wazee maarufu katika kata hii ni pamoja na Maalim Shaabani Abdallah, Mzee Athumani Sollo Nguku, Mzee Majid Nassor, Mzee Hussein Simbachai, Mzee Salum Sauji Kigabho, Mzee Mwananhanzagila na wengineo wengi ambao wameshafariki dunia.
Historia
haririKijiji cha Ndembezi kina historia ndefu sana, ikirudi nyuma katika kipindi cha kabla ya kuingia wakoloni. Kilikuwa makao ya Msaidizi wa Mtawala wa nchi ya Nyawa ambapo makao makuu yake yalikuwa katika kijiji cha Ulaya.
Ndembezi ilitawaliwa na watawala kama Chifu Ndambile, Ntinginya na Kabeho.
Kijiji na kata hii vitaendelea kukumbukwa kwa kutoa waziri wa Elimu na Mbunge wa Igunga Charles Shija Kabeho, mtoto wa Chifu Kabeho aliyekuwa mtawala wa mwisho wa Ndembezi kabla ya uchifu kufutwa katika kipindi cha utawala wa rais Julius Kambarage Nyerere.
Ndembezi pia ni maarufu kwa kukaliwa na idadi kubwa ya Waarabu wafanyabiashara kabla na baada ya ukoloni. Waarabu maarufu waliowahi kuishi Ndembezi ni pamoja na Nassor Majid Seif, babu yake na Abdallah Majid Nassor alifika Tabora mwaka 1897 akitokea Zanzibar ambapo alihamia Nzega, akaenda kuishi Izimba Bhusu (Ussongo) na hatimaye akahamia Ndembezi. Kabla ya kifo chake alihamia tena Izimba Bhusu alikofia na kuzikwa huko. Wafanyabiashara wengine wa Kiarabu waliokaa Ndembezi ni Ally bin Salum na Mohamed Saidi Kinanda.
Ndembezi ina majengo ya kihistoria yaliyojengwa na Waarabu katika karne ya 18; baadhi ya magofu hayo yanapatikana hadi leo kijiji cha Ndembezi, Ntigu na Kitangiri.
Viongozi wazawa
haririKata ya Ndembezi iliongozwa na diwani wao kijana mwenye ukomavu wa kisiasa toka Chama cha Mapinduzi Abubakar Shaabani Abdallah ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga kuanzia mwaka 2000 hadi 2020. Diwani huyo amechangia mambo mengi katani hapo ikiwa ni pamoja na kumalizia ujenzi wa zahanati ya Ndembezi, ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Ndembezi na uchangiaji wa huduma za kijamii hasa wakati wa majanga mbalimbali kama ugawaji wa chakula wakati wa njaa.
Marejeo
haririKata za Wilaya ya Igunga - Mkoa wa Tabora - Tanzania | ||
---|---|---|
Bukoko | Chabutwa | Chomachankola | Iborogelo | Igoweko | Igunga | Igurubi | Isakamaliwa | Itumba | Itunduru | Kining'ila | Kinungu | Kitangili | Lugubu | Mbutu | Mtunguru | Mwamakona | Mwamala | Mwamashiga | Mwamashimba | Mwashikumbili | Mwisi | Nanga | Ndembezi | Ngulu | Nguvumoja | Nkinga | Ntobo | Nyandekwa | Simbo | Sungwizi | Tambalale | Ugaka | Uswaya | Ziba |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tabora bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Ndembezi (Igunga) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |