Wingu Kubwa la Magellan

Wingu Kubwa la Magellan (ing. Large Magellanic Cloud, kifupi LMC) ni galaksi ndogo iliyo karibu na galaksi yetu ya Njia Nyeupe na sehemu ya kundi janibu letu. Inakadiriwa kuwa na nyota mnamo bilioni 10 - 15. Umbali wake na Dunia yetu ni takriban miakanuru 160,000.

Njia Nyeupe na Mawingu ya Magellan jinsi inavyoonekana katika jangwa la Atacama, Chile; nyota angavu ni Suheili

Kwenye usiku wa giza sana pasipo ukungu hewani inaonekana kama wingu au doa kubwa linalong'aa. Linaonekana pamoja na doa jeupe la pili lililo karibu linaloitwa Wingu Dogo la Magellan na kwa pamoja hujulikana kama Mawingu ya Magellan.

Ilhali linaonekana vema kwenye anga ya nusutufe ya kusini kwa macho matupu mataifa na makabila mengi yana majina kwa ajili ya mawingu ya Magellan.

Jina la kimataifa linatokana na nahodha na mpelelezi Mreno Ferdinand Magellan aliyekuwa mtu wa kwanza kuleta habari zake Ulaya.

Ushuhuda wa kwanza wa kimaandishi unaojulikana ni "Kitabu cha Nyota" cha Mwajemi Abd-al-Rahman Al Sufi aliyetaja "Ng'ombe Dume Mweupe" inayoonekana kwa Waarabu wa kusini ilhali wingu halikuonekana katika kaskazini mwa Uarabuni[1].

Amerigo Vespucci aliyetembelea pwani za Amerika mnamo mwaka 1500 alitaja sehemu mbili angavu alizozitazama kwenye anga la kusini na inaaminiwa ya kwamba alitaja hivyo mawingu ya Magellan.

Maelezo ya kwanza yaliyoeleweka yalitolewa na Ferdinand Magellan aliyekuwa mtu wa kwanza kuzunguka Dunia yote katika safari ya miaka 1519 - 1522. Hapo alichora pia ramani za nyota na kufanya vipimo vya kwanza vya mawingu angavu ya anga yaliyopokea baadaye jina lake.

Tabia zake

hariri

Wingu Kubwa la Magellan linaonekana katika eneo la makundinyota ya Panji (Dorado) na Meza (Mensa) kwenye angakusi la Dunia. Halionekani kwa watazamaji wanaokaa upande wa latitudo ya 20° ya kaskazini.

Zamani makadirio ya umbali wake yalitofautiana sana. Tangu mwaka 2013 umbali wa kitovu chake uliweza kupimwa kwa hakika kubwa kuwa parsek 49,970 (49.97 kpc)[2] au miakanuru 162,902.

Masi ya Wingu Kubwa ya Magellan ni takriban sehemu ya kumi ya Njia Nyeupe (galaksi yetu). Kipenyo chake ni takriban miakanuru 14,000 (Njia Nyeupe ni zaidi ya 100,000). Umbo lake halifuati muundo maalumu sana kama galaksi nyingi. Kuna mkusanyiko wa nyota na mata nyingi katika kitovu chake [3] na mkono mmoja tu wenye umbo la parafujo[4]. Umbo lake ni dalili ya kwamba athari ya graviti ya Njia Nyeupe na Wingu Ndogo kwa pamoja zilivurugisha mfumo wa awali wa Wingu Kubwa ambao labda ilikuwa la parafujo.[5]

Wingu Kubwa linasogea kwenye anga-nje kwa kasi ya kilomita 378 kwa sekunde, pamoja na Wingu Dogo lenye kasi ya 302 km/sec. Hapa wataalamu hawana uhakika kama mawingu yote mawili ni sehemu ya mfumo wa Njia Nyeupe zikishikwa na graviti yake na kuizunguka, au kama ni galaksi geni zinazopita tu karibu na Njia Nyeupe.[6]

Tanbihi

hariri
  1. Abd-al-Rahman Al Sufi , tovuti ya Messier Catalogue, iliangaliwa Oktoba 2017
  2. An eclipsing binary distance to the Large Magellanic Cloud accurate to 2 per cent, G. Pietrzynski et al. 7 Machi 2013 , tovuti ya European Southern Observatory, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. A Cosmic Zoo in the Large Magellanic Cloud, tovuti ya European Southern Observatory, tar. 1 Juni 2010, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. [linganisha http://adsabs.harvard.edu/full/1955AJ.....60..126D de Vaucouleurs, G. (1955), Diemsnsions and Structure of the Large Cloud], Astronomical Journal Vol 60, p 126ff, tovuti ya harvard.edu, iliangaliwa Oktoba 2017
  5. Besla. G. et al: "Low Surface Brightness Imaging of the Magellanic System: Imprints of Tidal Interactions between the Clouds in the Stellar Periphery", (2016). The Astrophysical Journal. 825 (1): 20, tovuti ya Institute of Physics IOP science publishing, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Magellanic Clouds May Be Just Passing Through, tovuti ya Harvard-Smithsonian Center for Astrophysics, release Release No.: 2007-02 / January 9, 2007; iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wingu Kubwa la Magellan kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.