Farisi

(Elekezwa kutoka Perseus)

Farisi (kwa Kigiriki: Περσεύς Perseus) ni shujaa katika hadithi za Mitholojia za Kiigiriki. Alitajwa kama mwanzilishi wa mji wa Mikene akiwa pia maarufu kwa kumuua dubwana Madusa. Katika masimulizi ya Wagiriki alitazamwa kama nusu-mungu, yaani mtoto wa mungu mkuu Zeu na wa binti wa kibinadamu Danaë. Alikumbukwa kuwa pamoja na mke wake Andromeda, binti mfalme wa Ethiopia, na wanao Perses, Alkaios, Sthenelos, Elektryon, na binti Gorgophone. Katika masimulizi hayo, Farisi pia ni babu-mkubwa wa Herakles.

Farisi - Perseus akishika kichwa cha Madusa, na Antonio Canova, alikamilisha 1801 ( Makumbusho ya Vatikani)

Asili ya jina haieleweki vema. Ni jina la kale sana: kuna maelezo ya kwamba lilimaanisha "askari, mharibifu". Kutokana na kutoeleweka Wagiriki wa baadaye waliichukua kumaanisha "mtu kutoka Persia" (Iran), yaani Mwajemi. Jina la Kigiriki "Perseus" lilifika Afrika ya Mashariki kupitia masimulizi ya Waarabu waliopokea maana inayomtaja mtu wa "Fars", yaani Iran, hivyo lilipata umbo la "Farisi" pale linapotajwa ketika mapokeo ya Waswahili, kwa mfano katika kundinyota Farisi[1].

Alivyozaliwa

hariri

Babu wa Farisi, mfalme Akrisio wa Argos aliambiwa na mwaguzi kuwa angeweza kuuawa na mjukuu wake. Kwa sababu hiyo alimfunga binti yake Danaë katika mnara ambao hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia, ili asiweze kupata mimba. Lakini mungu Zeu aliweza kuingia kwa kuchukua umbo la mvua ya dhahabu, na mtoto wake alikuwa Farisi.

Akrisio kisha akamweka Danaë na mtoto wake Farisi ndani ya sanduku na kuwatupa baharini. Lakini Zeu alimwagiza mungu wa bahari Poseidoni awasaidie, na kwa hiyo Danaë na mtoto wake walifika kwenye kisiwa cha Seriphos. Huko wanapatikana na mvuvi Diktys, anayewaokoa na kuishi nao.

Miaka mingi baada ya hapo, Farisi anashiriki katika michezo kwa heshima ya mazishi fulani. Akrisios yuko pia kati ya wageni, Wakati wa michezo, Perseus anatupa diski, ambayo kwa bahati mbaya humpiga Akrisios ambaye akafa; kwa njia hiyo utabiri ulitimizwa.

Farisi na Medusa

hariri

Farisi alitumwa na Mfalme Polidektes achukue kichwa cha Madusa, maana huyu Polidektes alitaka kumwoa mama yake Farisi lakini kijana alimzuia. Kwa kutoa ombi hili Polidektes alifikiri haiwezekani na Farisi angekufa maana wote waliowahi kumwona Madusa walibadilishwa kuwa jiwe.

Katika mpango wake, Farisi alipata msaada na ushauri wa miungu mbalimbali waliomheshimu akiwa mwana wa Zeu. Athena alimtuma kwa masista ya kijivu, mabibi watatu wazee waliochanga jicho moja, ambao mwanzoni walisita kumwambia kitu; lakini Farisi alinyanganya jicho kutoka kwao mpaka walimjibu. Walimpeleka kwa mapepo ya Hesperidi waliompatia mfuko wa kubeba salama kichwa cha Madusa; Zeu alimpa upanga wa almasi, mungu wa kizimu Hades alimkopesha kofia yake ya giza iliyoweza kumficha kabisa, na Hermes alimwachia kwa muda viatu vyake aweze kuruka. Hatimaye Athena alimpa ngao iliyong'arishwa ili aweze kumwangalia Madusa kupitia kioo, asimwangalie mmoja kwa moja, kwani kila mtu aliyemtazama machoni angegeuka kuwa jiwe.

Kwa msaada wa vifaa hivyo vyote, Farisi aliweza kufika katika pango la Madusa na kukata kichwa chake.

 
Farisi alivyomokoa Andromeda; uchoraji kwenye chungu ya Ugirikiy a Kale

Farisi na Andromeda

hariri

Akiwa njiani kurudi nyumbani, alipita katika Ethiopia. Kwenye mwambao wa nchi hiyo alimkuta Andromeda, binti wa mfalme, aliyefungwa hapa kama kafara kwa dubwana wa baharini Ketusi. Akamwua Ketusi akamweka Andromeda huru na kumwoa, akirudi naye nyumbani.

Baada ya kutumiza maisha yao, Athena aliweka Farisi pamoja na Andromeda kati nyota ya anga, ambako wanaonekana hadi leo kama makundinyota ya Farisi na Mara.

Marejeo

hariri
  1. Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331

Viungo vya Nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: