Prussia ya Magharibi
Prussia ya Magharibi ilikuwa jimbo la kihistoria kwenye dola la Prussia katika Ujerumani kuanzia mwaka 1772 hadi mwaka 1945. Leo hii eneo lake ni sehemu ya mkoa wa Pomerania katika Poland.
Hadi mwaka 1772 maeneo ya Prussia ya Magharibi yalikuwa chini ya Milki ya Poland. Yalikuwa na katiba ya pekee; wakazi wa miji walikuwa hasa wenyeji wenye lugha ya Kijerumani wakifuata madhehebu ya Uprotestanti lakini wakazi wengi wa vijiji walitumia lugha ya Kipoland wakifuata Ukatoliki.
Mwaka 1776 Poland iligawiwa mara ya kwanza baina ya Urusi, Austria na Prussia. Sehemu zilizowekwa chini ya Prussia ziliitwa sasa "Prussia Magharibi", tofauti na Prussia asili iliyoitwa sasa "Prussia Mashariki". Wakati wa ugawaji wa Poland kwenye mwaka 1793 maeneo mengine yalitwaliwa na Prussia na kuongezwa katika jimbo la Prussia Magharibi.
Wakati wa Napoleon sehemu za kusini za Prussia Magharibi zilitengwa tena na kuingizwa katika Utemi wa Warshawa uliokuwa tena dola la Kipolandi chini ya usimamizi wa Ufaransa. Baada ya kushindwa kwa Napoleon mkutano wa Vienna uliamua mwaka 1815 kurudisha sehemu hizi kwa Prussia ilhali maeneo mengine yaliwekwa chini ya Urusi.
Serikali ya Prussia ilifuata siasa ya kuimarisha utamaduni wa Kijerumani katika jimbo hili pamoja na kuingiza walowezi Wajerumani kwa shabaha ya kupunguza idadi ya wakazi waliojisikia Wapolandi. Mnamo mwaka 1910 Prussia Magharibi ilikuwa na wakazi milioni 1.7 na asilimia 65 walikuwa na Kijerumani kama lugha ya kwanza, asilimia 28 na Kipoland na asilimia 7 na Kikashubi.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Ujerumani (pamoja na Prussia) ilishindwa na Polandi ikaundwa upya. Kwenye Mkataba wa Versailles sehemu kubwa ya Prussia Magharibi iliingizwa katika Polandi na maeneo ya kaskazini yalikuwa Dola-mji wa Danzig. Wakazi hawakuulizwa kuhusu ugawaji huu kwa sababu washindi wa vita waliona ya kwamba Polandi ilihitaji mawasiliano na bandari kwenye pwani ya Bahari Baltiki. Maeneo madogo upande wa magharibi yalibaki upande wa Ujerumani; wilaya kadhaa upande wa mashariki yalipewa nafasi ya kupiga kura na wakazi walichagua kuwa sehemu za Ujerumani; sehemu zilikuwa Mkoa wa Prussia Magharibi katika Jimbo la Prussia Mashariki baina ya 1920 hadi 1945.
Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia Polandi ilishindwa na Ujerumani mwaka 1939. Maeneo ya Prussia Magharibi yaliingizwa tena katika muundo wa Dola la Ujerumani. Katika miaka michache ya utawala wa Kijerumani uliokuwa mikononi wa chama cha Nazi wakazi Wapolandi waliteswa na hasa wakazi Wayahudi walitafutwa na kuuawa katika maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya.
Mwaka 1945 maeneo yake yalitwaliwa na Jeshi la Kisovyeti na kuingizwa katika Polandi. Wakazi Wajerumani walifukuzwa na kuhamishwa katika sehemu nyingine za Ujerumani.