Transparency International
Transparency International (kifupi: TI) ni Shirika Lisilo la Kiserikali la kimataifa lenye shabaha ya kupambana dhidi ya rushwa na hongo kote duniani. Makao makuu yako Berlin (Ujerumani).
Shirika liliundwa mwaka 1993 huko Berlin na Peter Eigen na marafiki zake. Eigner aliwahi kuwa mkurugenzi wa Benki ya Dunia akaanzisha TI kutokana na maarifa yake kazini.
Chanzo cha TI
haririEigen alipata wazo la kuanzisha TI alipoongoza kamati ya ukaguzi wa miradi iliyolipiwa na msaada wa kimataifa nchini Kenya. Alitambua ya kwamba mara nyingi miradi yenye gharama kubwa zilipewa kipaumbele na mashirika yanayotoa misaada lakini pia na serikali za nchi zinazopokea misaada, hata kama miradi hiyo haina faida kubwa kwa watu wanaolengwa na miradi, tena hata kama miradi hiyo inaongeza madeni ya nchi inayopokea. Kamati ilitambua ya kwamba maafisa wa pande zote mbili, yaani upande wa kutoa na upande wa kupokea fedha, mara nyingi walipendelea miradi ghali kwa sababu ya faida zao binafsi. Hasara ilikuwa wazi kwa nchi zinazopokea misaada kwa sababu madeni yao huongezeka yanayopaswa kulipwa baadaye. Hasara ilionekana pia upande wa nchi zinazotoa pesa ya misaada kwa sababu pesa ya umma hutumiwa kwa faida za binafsi ya makampuni makubwa yanayouza bidhaa na huduma kwa bei ya juu wakizuia msaada kufika kwa watu maskini wanaotakiwa kufaidika na msaada ule.
Kamati ilijifunza pia ya kwamba rushwa ilikubaliwa kwa namna fulani katika nchi ambako sheria za kodi zilikubali gharama za "kusahalisha" na kuwezesha makampuni kukata gharama hizo katika deni la kodi, hivyo kuruhusu hali halisi rushwa kufidiwa na idara ya kodi.
Hivyo kundi la watu wa siasa na biashara kutoka nchi za Ulaya na kutoka Afrika na Asia walianzisha shirika la TI. Walifaulu kuamsha serikali nyingi pamoja na mashirika makubwa zya kimataifa kuhusu maovu ya rushwa. TI imesababisha mabadiliko ya sheria katika nchi mbalimbali.
Taarifa ya kimataifa kuhusu rushwa (Corruptions Perceptions Index)
haririTI imejulikana hasa kutokana na taarifa zake za kila mwaka kuhusu kiwango cha rushwa katika nchi za dunia (Corruptions Perceptions Index). Taarifa hii hutolewa kutokana na maoni ya wataalamu na wafanyabiashara wanaoulizwa jinsi wanavyoona kiwango cha rushwa katika nchi fulani.
Taarifa hizo hupingwa mara nyingi kwa sababu hazitumii takwimu halisi bali mawazo na maoni ya watu wanaochaguliwa na TI. Ila tu hadi sasa hakuna njia bora inayojaribu kupima kiwango cha rushwa. Kwa hiyo wengi wameikubali kama onyo au mshale (indiketa) ya tatizo hilo.
Viungo vya Nje
hariri- Official site | TI's mission statement Archived 4 Julai 2008 at the Wayback Machine.
- List of TI National Chapters Archived 15 Oktoba 2008 at the Wayback Machine.
- TI's Global Corruption Report Archived 13 Machi 2020 at the Wayback Machine.
- International Anti-Corruption Conference Archived 6 Septemba 2008 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Transparency International kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |