V-2
V-2 (kifupi cha Kijerumani Vergeltungswaffe 2, yaani "silaha ya kulipiza kisasi namba mbili") ilikuwa roketi ya kijeshi ya Ujerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ilikuwa chombo cha kwanza kilichotengenezwa na binadamu kilichofikia anga-nje.
Roketi zote za kisasa hufuata kimsingi mfano wa V-2. Ilibuniwa na wahandisi wa kijeshi na wanasayansi chini ya uongozi wa Werner von Braun kwenye kituo cha kijeshi cha Peenemünde kwenye mwambao wa Bahari Baltiki. Ikarushwa mara ya kwanza tarehe 3 Oktoba 1942 ikifikia kimo cha kilomita 84.5. Tarehe 20 Juni 1944 ilifikia kimo cha kilomita 174.6 na kuvuka mpaka wa anga-nje uliopo kwa kilomita 100.
Kusudi la kubuni V-2 lilikuwa kubeba mabomu kwa miji ya Ulaya, hasa Uingereza, ambako jeshi la anga la Ujerumani lilikutana na upinzani mkali wa Waingereza. V-2 za kwanza zilizotumiwa kama silaha zilipiga Paris na London tarehe 8 Septemba 1944. Zaidi ya V-2 3000 zilirushwa na jeshi la Kijerumani dhidi ya shabaha za wapinzani wake zikaua takriban watu 7,200.
Baada ya vita Wamarekani na Warusi walikamata wataalamu wa Peenemünde na kuwatumia kuanzisha miradi ya roketi kwao. Kwa njia hii Werner von Braun aliendelea kuwa mkurugenzi wa kituo cha Marshall Space Flight Center akaitwa "Baba wa miradi ya anga-nje".
Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |