Kidubini

(Elekezwa kutoka Vidubini)

Vidubini (kwa Kiingereza: microorganism au microbe) ni jina la kundi la viumbehai vidogo sana. Kidubini hakionekani kwa macho bali kwa msaada wa kitambo kama hadubini pekee.

Kundi la bakteria za Escherichia coli zikikuzwa mara 10,000

Vidubini ni kundi lenye tabia tofauti sana kati yao. Vingi vyao vina seli moja pekee lakini kuna pia vidubini vyenye seli kadhaa kama vile kuvu na algae. Tabia ya pamoja ni udogo pekee.

Euglena mutabilis.

Aina za vidubini hariri

Kati ya vidubini kuna

Aina nne za kwanza zinaweza kuishi peke yao au ndani ya miili ya viumbehai wengine. Virusi huongezeka ndani ya viumbehai hao pekee. [1][2][3]

Wataalamu wengine hawahesabu virusi kati ya vidubini kwa sababu si viumbehai kweli.

Upatikanaji wa vidubini hariri

Vidubini ni muhimu sana katika mchakato wa uhai; algae ya diatomi zinatekeleza sehemu kubwa ya usanisinuru duniani ambayo ni msingi wa lishe ya mimea na wanyama wengi.

Vidubini vingine ni vidusia au pathojeni za magonjwa ya kuambukiza.

Kwa jumla idadi ya vidubini ni kubwa kabisa kuliko viumbehai wote wengine na asilimia 70 za biomasi duniani ni vidubini. Maana yake ni kwamba kwa pamoja viumbe hivi vidogo visivyoonekana kwa macho ni vizito kushinda wanyama na mimea yote ya dunia.

Vidubini vinapatikana kila mahali pa dunia hata kwenye tako la bahari, ndani ya miamba ya ganda la dunia au kwenye ncha za milima marefu hata zikielea katika hewa.

Vidubini ni muhimu katika lishe ya viumbe vingine; vinatekeleza kazi ya kuozesha mata hai iliyokufa (mimea, maiti, mizoga) na kuibadilisha katika hali inayoweza kutumiwa na mimea.

Vidubini vinavyoishi peke yao hariri

Vidubini visivyoishi ndani ya miili ya viumbehai wengine vinapata nishati yao kwa njia mbalimbali.

Vingi hutumia nishati ya nuru kwa njia ya usanisinuru, sawa na mimea. Vingine vinatumia kemikali asilia katika mazingira yao na vikitumia nishati inayopatikana kwa kuvunja muungo kemia wa kampaundi.

Vingine vinaishi kwa kuozesha mata hai iliyokufa kama majani yaliyoanguka, maiti na mizoga ya wanyama. Katika mazingira asilia mata iliyooza inachanganywa tena na udongo na hivyo kwa njia hii vinarudisha virutubishi katika ardhi ambavyo vingepungua mno bila mchakato wa kuoza na kurudisha virutubisho.

Vidubini kama hamira ni muhimu kwa kutengeneza vyakula kama mkate, jibini, divai na bia. Vinakula sukari iliyopo katika nafaka, matunda au maziwa na kuvipa vyakula hivyo tabia na ladha za pekee.[4]

Vidubini vinavyoishi ndani ya viumbehai wengine hariri

Vidubini vingi vinapatikana ndani ya viumbehai wengine na kupata nishati yao kutokana na lishe ya viumbehai hao au kutokana na miili yao.

Hasa vidubini ndani ya utumbo vinasaidia kumega vyakula na kutoa virutubisho kwa ajili ya miili yetu.[5]

Vingine ni pathojeni vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza kwa sababu vinaongezeka ndani ya mwili na kupita kutoka mtu mmoja kwa mtu mwingine. Kuoza kwa meno kunasababishwa na bakteria zinazokula sukari mdomoni na kutoa asidi inayoharibu gamba la jino.

Inawezekana kujikinga kwa kutunza chakula vizuri, kusafisha meno na mikono na kuepukana kuwa karibu sana na baadhi ya wagonjwa.

Marejeo hariri

  1. Rybicki E.P. 1990. The classification of organisms at the edge of life, or problems with virus systematics. S African J Sci 86: 182–6.  Missing or empty |title= (help)
  2. Lwoff A. 1957. The concept of virus. J. Gen. Microbiol. 17 (2): 239–53. PMID 13481308.  Missing or empty |title= (help)
  3. Forterre P. 2010. Defining life: the virus viewpoint. Orig Life Evol Biosph. 40(2):151-60. [1]
  4. Dinorah Pous (2003). Blue Planet. McGrawHill. 
  5. Sears C.L. 2005. A dynamic partnership: celebrating our gut flora. Anaerobe 11 (5): 247–51. PMID 16701579. doi:10.1016/j.anaerobe.2005.05.001.  Missing or empty |title= (help)

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kidubini kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.