Wagweno
Wagweno ni kabila la watu wenye asili ya Kenya wanaoishi Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro, upande wa Kaskazini wa Milima ya Ugweno.
Lugha yao ni Kigweno. Utamaduni wao ni mchanganyiko wa tamaduni za Kipare na Kichaga. Wagweno wanajishughulisha na kilimo na ufugaji. Wanalima ndizi, mahindi, kahawa na maharage. Pia Ugweno kuna kilimo cha matunda kama parachichi, maembe na mapensheni.
Shughuli za ufugaji zinahusisha ufugaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo.
Asili
haririKiasili Wagweno ni katika jamii zilizotoka Uhabeshi ya kale na ndiyo maana ukiangalia kwa makini utamaduni wao utaona kwamba hazifanani sana na Wabantu, bali na Wahamitiki. Tazama hata katika ngoma ya Kigweno ambayo wanaiita mrangi [mwanzi] hawatumii ngoma kama Wabantu.
Sababu ya kukimbia Kenya na kuhamia Tanzania ya leo
haririInasemekana asili yao wametoka maeneo ya Taita na Voi nchini Kenya.
Kilichowakimbiza Kenya ya kale na kuhamia eneo linalojulikana kama milima ya Ugweno kwa sasa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Taita na Voi.
Lakini kuna nadharia moja inayosema kwamba kabla Wagweno hawajahamia rasmi katika milima hiyo ya Upare walituma wapelelezi kwanza; walifika eneo husika na kisha wakarudisha taarifa yao wakasema, "Mringa ua khona" (yaani mito ya huko inatoa sauti katika kutiririka kwake) na hapo jina Ugweno likazaliwa, yaani kughona ni muungurumo.
Kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwamba Mgweno ni yeyote aliyekuja na kufanya makazi yake katika milima hiyo mizuri ya ugweno. Ndiyo kusema kwamba wahenga walitoka Taita, Voi, Uchaga na hata Upare: ndiyo maana unaweza kukuta hata koo za Wasangi, Wanzava, nk.
Mfano mzuri ni mzee Modongo na wenzake ambao waliitwa na Wasuya kutoka Usangi ili kuja kuzuia vita visiingie Ugweno. Ukoo huu mpaka leo unapatikana maeneo ya Chanjale kwa Mkuti njia ya kwenda Mangio na Vuchama, tena kuna mzee maarufu wa ukoo huo aitwaye Kiogwe Msangi ambaye alifariki dunia mwaka 1995.
Mila na desturi
haririKwa asili Wagweno hapo kale walikuwa Wapagani wanaoabudu mungu jua [RUBHA], pamwe na mwandani wake MWIRI [MWEZI], mkewe jua, sanjari na watoto wao nyota.
Ibada hii ya kuelekea jua iliambatana na kuabudu mizimu na ndiyo maana kuhani wa Kigweno alipochinja mnyama na kumchuna ngozi yake aliweza kutazama maini kupiga ramli kwa kutumia viungo kwenye tumbo la mnyama.
Tena wanyama hao walichinjwa kwenye eneo maalumu liitwalo kwa Kigweno Ngondinyi. Mara nyingi eneo hili walihusika wanaume bighairi wanawake kwa sababu kwa mila ya Kigweno wanaume ndio makuhani. Mara nyingi katika eneo la kuzunguka Ngondinyi kulipandwa mimea maalum iitwayo Mathale, ambayo kwa mujibu wa mapokeo ya Wagweno ni mimea mitakatifu.
Mnyama anapochinjwa kuhani hukata vipande vidogovidogo na kuviweka eneo husika, kisha huchukua pombe ama mbege au dengelua kisha atatazama mbinguni huku ameshika mkononi pombe kama ishara ya tambiko na kusema RUBHA KAGHU NGOMA MBAI; yaani, naamini mungu yuko juu, lakini chini kuna mizimu. Kisha humwaga pombe na kusema anachokusudia, kama anataka mvua inyeshe au anakusudia kuondosha MSINYANYO [mkosi].
Kwa maana kwa mujibu wa mapokeo ya Wagweno mkosi kwao ulikuwa jambo kubwa sana na ndiyo maana hata mtoto aliyezaliwa na ulemavu wa aina yoyote alitolewa kafara kwenye jiwe la watoto, kwa Kigweno IGHWE YA BHANA.
Mhanga alikuwa anachukuliwa kwenye jiwe husika, mamaye humbembeleza, akiisha kulala hulazwa kwenye kilele cha jiwe na anapoamka ghafla huporomoka na kufa na watakuwa wameondoa mkosi katika jamii na kumfurahisha mahoka.
Kuna kisa kimoja cha kale juu ya bwana mkubwa mmoja aliyeitwa Kindobhai wakati anafukuzwa na maadui kunako eneo ambalo kwa sasa kuna hifadhi ya wanyama ya Tsavo karibia na ziwa Jipe. Inasemekana alipiga fimbo yake kwenye maji na yeye, mifugo na wafuasi wake wakavuka salama!
Masimulizi juu ya Wagweno ni mengi sana, kiasi kwamba unaweza ukastaajabu. Mpaka leo kuna mawe ya ajabu ambayo yako mithili ya watu; inasemekana maadui hapo kale walikuwa wanakuja kuiba mifugo huko, lakini kulingana na ujuzi wa wazee wakageuzwa mawe kwa njia ya miujiza.