Wangurimi

kabila kutoka Mkoa wa Mara nchini Tanzania

Wangurimi (au Wangoreme) ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika Mkoa wa Mara, wilaya ya Serengeti.

Lugha yao ni Kingurimi ambayo waliweza kutambua miezi yote kumi na mbili kwa majina yake kama vile mwezi 1-Kyero kembele (Januari), 2-Itaturi (Februari), 3-Kimagha (Machi), 4-Etwigho (Aprili), 5-Kyero ghekaphere (Mei), 6-Kimagha ghekaphere (Juni), 7-Nyamapheho (Julai), 8-Ringura masaringi (Agosti), 9-Nyasahi (Septemba), 10-Kemwamu (Oktoba), 11-Rughaka (Novemba), 12-Kemwamu kemwisho (Desemba).

Historia hariri

Inasemekana walitokea katika tambarare za hifadhi ya Krugger iliyopo Afrika Kusini mwaka 1320 hivi wakanzaa harakati za kuhama taratibu kutokana na ongezeko kubwa la wadudu aina ya mbung'o walioshambulia mifugo yao na wao wenyewe. Mwaka 1740 baadhi yao walikuwa wameishafika bonde la Ufa la Ngorongoro na baadaye mwaka 1889 wakafika hifadhi ya Serengeti kusini mashariki nyika ya Loliondo. Walishabiana na wenyeji wa nyika ya Loliondo waliotambulika kama Wasonjo ambao walishabiana kwa kila kitu mfano misamiati ya lugha husika, tamaduni na kaliba.

Ilipofika miaka 1919-1932 walianza kusumbuana na kabila la Wamasai kwa kunyang'anywa mifugo yao kila itwapo leo ikawalazimu kuanza kuhama ili wasiendelee kusumbuana na Wamasai kwa kufuata tambarare za mbuga ya Serengeti na ilipofika 1945 wakawa wamefika sehemu mbalimbali za Serengeti wakiwa ni waanzilishi wa mji wa Mugumu wakiongozwa na kiongozi wao aliyeitwa Sabayaya na mdogo wake aitwaye Ikoma; hapo waliishi vizuri huku wakijishughulisha na kilimo, ufugaji maeneo ya Mangwesi na walianza kuzaliana kwa kasi kubwa iliyopelekea kutapakaa sehemu nyingi za Serengeti.

Mwaka 1970 vita vikali kati ya Wangoreme na Wakuriya vikapamba moto maeneo ya Kibaso wakati Wakuriya walipoiba ng'ombe za mzee Mokena na inakadiriwa kuwa vita hivyo vilikuwa vibaya sana kwani takribani watu 86 waliaga Dunia kwenye vita hivyo akiwemo Mgaya-Nyamori wa Majimoto Mwita-Maro wa Kisaka na wengineo wengi.

Mwaka 1989 vita vya pili kati ya Wakuriya na Wangoreme vikapamba moto baada ya Wakuriya kuiba ng'ombe za mzee Mgaya (Nyarokweli) na Motondi waliokuwa wanaishi maeneo ya tambarare za nyika za Kemgesi: inakadiriwa watu wapatao 34 walipoteza maisha.

Wangoreme wanapatikana kwa wingi huko Iramba (Ngoreme), Majimoto, Busawe, Gantamome, Kisaka Nyiboko, Nyansurumunti, Gantamome, Busawe, Mesaga, Kenyamonta, Remung'oroli, Maburi, Gusuhi, Kemgesi, Masinki, Magange, Ring'wani, Kenyana, Nyamatoke, Mosongo, Nyamitita na Bolenga.

Utamaduni hariri

Ni wafugaji wa ng'ombe, mbuzi, kondoo, mbwa kwa ulinzi wa mifugo, paka na punda: hiyo ndiyo asili yao.

Chakula cha asili ni ugali wa ulezi, mtama, mhogo, mahindi, pia kunde, njugumawe, maboga, karanga.

Watani wa Wangurimi ni Wanyiramba na Wamasai. Vilevile Wangoreme wamepakana na kabila la Wakuriya, jamii ya Wanyabasi, Wakira, Wairenge, Wakenye upande wa kaskazini-mashariki wa Serengeti.

Wangoreme ni wakarimu na wanapenda maendeleo, pia ni watu ambao wanapenda sana siasa. Kuna ushindani mkubwa, hasa kati ya vyama viwili: CCM na CHADEMA.

Ni watu wanaopenda kufuata mila na desturi za Kingoreme, kwa mfano jando na unyago kwa vijana waliofikia rika la kuwa na majukumu ya kifamilia (Saro).[1]

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wangurimi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Unknown (2013-08-12). NGOREME KWETU: SERENGETI ILIVYOVAMIWA VIJIJI VYAKE. NGOREME KWETU. Iliwekwa mnamo 2024-01-13.