Ring'wani
Ring'wani ni kata ya Wilaya ya Serengeti lakini pia kijiji katika wilaya ya Serengeti katika Mkoa wa Mara, Tanzania yenye postikodi namba 31614[1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 8,785 waishio humo.[2]'
Kata ya Ring'wani inaundwa na vijiji vya Remung'orori, Maghange, Masinki, Ring'wani Nyamitita na Kenyana ambacho ni kitovu na mhimili mkubwa kwa eneo la Ngoreme kwani ndicho kijiji kinachopakana na koo tata za Kabila la Wakurya wanaojihusisha sana na uporaji wa mifugo wilayani Serengeti na hasa katika eneo la Ngoreme. Historia ya watu na maeneo kama ilivyo jamii ya Ring'wani hujengwa na mafanikio au wasifu wa jamii husika hasa watu wake mashuhuri katika maisha ya kisisasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii, hasa kwa watu wale waliofanya mabadiriko chanya katika jamii, kata ya Ring'wani Kijijini Kenyana ndiko alikoishi mzee maarufu miongoni mwa wazee waasisi wa TANU na baadaye Chama cha Mapinduzi (CCM) Mzee Nsaho Maro. Mzee huyo alikuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya Mkoa wa Mara, hasa Wilaya ya Serengeti na kijiji cha Kenyana kwa kuchangia ujenzi wa shule, zahanati, mahakama, na kituo cha polisi nia yake ilikuwa kuasisi kijiji cha kisasa chenye miundombinu yote muhimu. Nsaho ahlikua na ushawishi mkubwa katika jamii ya Ngoreme sambamba na wazee wenzake kutoka vijiji vingine vya Ngoreme kama James Baker (Bega) Ruge, Masiko Moghita, Maro Sosera, Hitler, Chacha Mangari, Mwita King'orori (Masase), James Makenge Ruge, Masosota Ighonga, Pius Maghoko Makongo, Maisori Tumbo, Herman, Petro Maswe, January Waisariro, Chacha Soghora, Wambura Bhwana, Nyambabhe, Renterenge, Maro Kyariga, Nyarukobha na baadae kijana waliyemlea na kumwingiza katika siasa za Ngoreme Mzee Faustine Maro Ruge, wazee hawa walihusika sana katika kuendeleza amani na mshikamano baina ya koo za Waikoma, Wangoreme, Wanyabasi, Wakira na koo nyingine za kabila la Wakurya.
Historia Edit
Kijiji cha Ring'wani kilianza baada ya familia kadhaa za ukoo wa Ruge kuhamia katika eneo lao la asili tangu jadi, wakitokea pande za Roghoro na Majimoto walikokuwa Wakiishi uhamishoni tangu miaka ya 1940 wazee wao walihama maeneo ya Ring'wani ya sasa wakati huo kutokana na mbung'o waliosababisha magonjwa ya mifugo na uvamizi wa mara kwa mara wa Wamasai.
Hizi familia ambazo zilikuwa ni za ukoo wa Ruge, wafugaji wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa tajiri mfugaji Mzee James Makenge Ruge aliyekuwa kiongozi wa ukoo huo, aliambatana na ndugu zake wakina Mahiti Chacha Bhayayi, Mtongori Mhoni, Ghiraita Ruge, Maro Muhoni na Hakimu wa kwanza Mongoreme kuwahi kuhudumu katika mahakama ya mwanzo kwa kutumia lugha ya Kiswahili Mzee Ferdinand Makore Ruge, na baadaye wakahamia William Moremi Ruge na mwanasiasa mashuhuri Kepteni Faustine Maro Ruge, mdogo wake James Makenge Ruge, wazee wengine walihamia baadae kama familia ya Nyaruchowa, Nyanduku, Kiroche, Nyamarasa, Ighonga,Temweni na wengineo.
Kijiji kilianzishwa rasmi mwaka 1977 baada ya kumeguka kutoka katika kijiji cha Ujamaa Kemghesi. Katika kijiji hiki ndiko asili ya ukoo maarufu wa Ruge unaofahamika kwa kuwa na wasomi wengi waliobobea katika nyanja mbalimbali.
Kijiji cha Ringwani, kisiasa kina sifa ya kutoa wanasiasa mashuhuri kwani kiliwahi kutoa mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Serengeti 1982-1992 na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Kepteni Faustine Maro Ruge ambaye pia aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Ring'wani kati ya miaka 2000 na 2005. aliyechangia sana maendeleo ya kielimu wilayani Serengeti kwani ndiye mwasisi wa ujenzi shule za Sekondari za kwanza wilayani humo yaani, shule za sekondari Ngoreme, Serengeti, Issenye Nyabhehore, na Kambarage, ambazo zilijengwa kwa nguvu na ushawishi mkubwa wa mwanasiasa huyo aliyehakikisha zinajengwa kwa nguvu ya wananchi na kusajiriwa kinyume cha sera ya serikali wakati huo.
Baadaye kijiji hiki kilimpata mbunge wa jimbo la Serengeti Dr. Deogratias Mwita kuanzia mwaka 1991 mpaka 2000, ambaye alifanikiwa kuwa Naibu Waziri wa Serikali za mitaa katika serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa na baadae Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Wilayani Serengeti Kijiji cha Ring'wani kinafahamika kwa kutoa wanasiasa mahiri katika wilaya ya Serengeti, na katika medani ya kitaifa Wakiwa wazaliwa Wa Ring'wani, Kepteni Faustine Maro Ruge na aliyekuwa rafiki yake mkubwa Dr. Deogratias Mwita wote ni wenyeji wa kijiji hicho. Ruge ndiye aliyemwingiza kwenye siasa Deogratias Mwita, na baadaye inasemekana ugomvi baina yao ulisababisha kuanguka na kufutika kabisa kisiasa kwa Dr. Mwita aliyejaribu mara kadhaa kurudi kwenye uringo wa siasa bila mafanikio. Ruge ni mwanajeshi mstaafu wa JWTZ akiwa amewahi kuwa kamanda mwandamizi na mkuu wa vikosi mbalimbali nchini Tanzania. Tanzania ikiwa moja ya nchi za mstari wa mbele Ruge alipata fursa ya kushiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika akihusika katika kufundisha wapigania uhuru hasa wa FRELIMO na ZANU PF na hata kushiriki na kuongoza harakati za siri za kijeshi na mapambano katika mataifa mbalimbali yakiwamo Msumbiji, Angola, Afrika Kusini, Komoro, Shelisheli, Namibia, Zimbabwe na Uganda aliposhiriki kwa nguvu katika harakati za kumwondoa madarakani aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo Idd Amin Dada, ambapo pia alibaki katika kazi maalumu ya kuilinda nchi hiyo hadi mwaka 1982. Ruge ametunukiwa medani mbalimbali za utumishi uliotukuka ikiwamo nishani ya vita (Medal for Victory in Uganda), Nishani ya Kagera, Nishani ya Zimbabwe, Nishani ya Ujasiri na nyingine kadhaa. Ruge ni mmoja kati ya askari wawili wa kwanza wakati wa vita vya Kagera walioshuhudia na kuthibitisha kuwa daraja la Kagera llimevunjwa na askari wa Idd Amin, Ruge ndiye kamanda aliyeongoza zoezi la kufungua vyumba vya mateso vya dikteta Idd Amin na kuachilia huru wafungwa wengi wa kisiasa mara baada ya kuiokomboa Uganda na baadaye Ruge alipewa kazi maalum ya kulinda kituo cha kurushia matangazo cha Radio Uganda (Radio Uganda Transmitting Station). Baade Ruge alirudishwa Ikulu ya Entebbe kwa kazi ya kulinda Ikulu ya nchi hiyo na kuhakikisha usalama wa marais Godfrey Lukongwa Binaisa, Yusuf Kironde Lule na Paul Muwanga, baadae yeye na wenzake walisimamia uchaguzi wa kwanza nchini Uganda baada ya kumwondoa madarakani Dikteta Idd Amin, uchaguzi huo ambao ulifanyika mwaka 1980 ulikuwa na ushindani mkali kati ya Bwana Paul Ssemogerere na Sir. Milton Obote, uchaguzi huo uligubikwa na utata ulioepelekea machafuko baada ya Sir. Milton Apollo Obote aliyekuwa Rafiki mkubwa wa Nyerere kutangazwa mshindi, machafuko hayo yalisababisha vifo vingi vya askari wa Tanzania hali iliyopelekea Ruge kupewa kazi maalum ya kutuliza na kukomesha maasi hayo katika jiji la Kampala na Entebbe.
Kijiji cha Ring'wani kilibahatika kupata wanasiasa wenye maono ya mbali sana mfano Deogratius Mwita huyu alifanikiwa kukomesha wizi sugu wa mifugo kwa kudumisha urafiki maalum wa kimila baina ya Wangoreme na koo za Wakurya wilayani Serengeti sambamba na rafiki yake Ruge. Mwita anafahamika kwa umahiri wake wa kutumia lugha ya Kengoreme jukwaani ukimlinganisha na Ruge, Ruge akiwa ameanza siasa tangu mwaka 1982 ambapo wanajeshi walikuwa wanaruhusiwa kushiriki siasa, anafahamika kwa umahiri wake wa kuzungumza jukwaani na ushawishi mkubwa katika siasa za wilaya hiyo, anaheshimika kwa kuasisi na kusimamia ujenzi wa shule ya msingi Kemalambo iliyoko kijijini kwake Ring'wani, na ujenzi wa shule za Sekondari Serengeti, Kambarage Nyerere na Ngoreme, aliasisi pia ujenzi wa shule za sekondari Nyabehore na Isenye ambazo baadae zilikabidhiwa kwa taasisi za kidini kutokana na uwezo mdogo wa Serikali na wananchi wakati huo (kwa vipindi tofauti alikuwa mwenyekiti wa bodi za shule hizo). kitendo cha ujenzi wa shule hizo kwa wakati mmoja mwanzoni na katikati ya miaka ya 1980 kilimsababishia maswali mengi kutoka kwa Baba wa Taifa la Tanzania Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeamini zaidi katika uboreshaji wa Shule za Misingi wakati huo, Nyerere akiwa Mwenyekiti Wa CCM Taifa alimshauri Ruge kujikita zaidi katika katika elimu ya msingi kwani ndio elimu iliyopatikana kwa wengi vijijini lakini Ruge aliamini katika maendeleo ya mapema katika jamii yake endapo vijana wangesoma elimu ya juu kwanza.
Baadaye, wageni walizidi kuhamia kwa ajili ya uchimbaji mdogomdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Kemalambo kwani pia Kijiji cha Ringwani kimekuwa ni eneo linalovutia sana kwa kuwa kipo njia panda ya kijiji kikubwa cha Kemgesi na njia panda ya kijiji cha Maburi na pia kijiji hiki kimepitiwa na barabara ya mkoa kutoka Musoma kwenda Mugumu hadi Arusha. kwa siku za karibuni Ring'wani kuna vuguvugu la wananchi kujiletea maendeleo mfano katika ujenzi wa Zahanati kwa kutumia nguvu zao wenyewe, kwani richa ya kuwa na wanasiasa mashuhuli hakukuwahi kuwa na kituo cha afya, kwani kijiji cha Ring'wani kina matatizo makubwa ya misuguano baina ya koo za Waireghe na Wabhwiro msuguano ambao umekwamisha baadhi ya maamuzi muhimu ya maendeleo kwa miaka mingi. uharibifu wa misitu na uchomaji hovyo wa majani Ring'wani ni vitendo viliyopelekea uharibu wa vyanzo asili vya maji na ukame uliokithiri.
Ni katika kijiji hiki ndiko anakotoka Mwanasiasa machachari wa mlengo wa upinzani (CHADEMA) na Mbunge Dr. Catherine Ruge akitokea katika ukoo wa kisiasa na wasomi wa Ruge ni binti wa Hakimu Mzee Ferdinand Makore Ruge, Bi. Ruge ni mwanafunzi wa kisiasa wa Kepeteni Ruge (Mwana CCM na Baba yake mdogo) na inasadikiwa anafuata nyayo zake, anasifika kwa michango yake adhimu bungeni hasa katika nyanja za mazingira na haki za wanawake na watoto wa kike, ni mwanadada wa kipekee kwani ni wa kwanza katika kijiji hicho kumaliza kidato cha sita na wa kwanza kupata shahada ya Chuo Kikuu, shahada ya Uzamiri na Uzamivu pia, mwanaharakati huyu wa haki za binadamu hasa za wanawake na watoto wa kike alikataa kukeketwa kama ilivyokuwa jadi ya jamii katika usichana wake, vita anayoiendesha mpaka hivi sasa kupinga unyanyasaji na ukeketaji, kwa jitihada zake alijenga bweni la kisasa katika Sekondari ya Ring'wani kwa ajiri ya watoto wa kike walio katika mazingira magumu, anafahamika kwa kutoa misaada ya mahitaji maalum mashuleni wilayani Serengeti hasa kwa watoto wanaotoka katika kaya masikini, Mbunge huyu kijana amaevunja rekodi kwa kujenga nyumba ya kisasa zaidi ya orofa moja hapo kijijini kwake Ring'wani.
Katika kijiji hiki ndipo zinapopatikana familia za wazee wa zamani kama Wichoka Masancha, Chacha Masabhi, Mahemba Changure, Machota Witocho, Nyabhunya, Ndeghe Temweni, mwanasiasa mkongwe kigogo na nguri Cleophas Maighe Mohogo, Chacha Soghora, Maro Ghesimba, Maro Monyi, George Mato, Ghesusu, King’orori na Mghaya Keghuku.
Kijiji cha Ring’wani kina historia ya kuwa na familia za mifugo mingi na pia wafugaji mahiri waliowahi kutokea wakiongozwa na Nyamarasa Masiko Nyangogho aliyekadiriwa kuwa na idadi ya ng’ombe wapatao 14000 mpaka wakati wa kifo chake, pia waliwahi kuwapo wazee matajiri wa mifugo kama Masosota Ighonga na nduguye Edward Ghaghuri Ighonga, Mzee Nyanduku Maheri “Tip Tip" Masiko Moghita na Chacha Nyaruchowa waliofahamika kwa idadi kubwa ya mifugo katika historia ya kijiji cha Ring’wani.
Matajiri hawa wa mifugo Wazee James Makenge Ruge, Edward Ghaghuri Ighonga, Nyamarasa Masiko na Masosota Ighonga wanakumbukwa kwa busara na moyo wao wa kutoa misaada katika jamii hasa wakati wa shida kama njaa, ugonjwa, misiba, ada za shule na hata mahali kwa ajiri vijana ya kuolea pale mtu alipopungukiwa kwani walitumia mali zao kusaidia wengine. mfano wakati fulani baraka hii ya mifugo mingi ilisaidia sana katika kijiji cha Ring’wani kwani karibu asilimia kubwa vijana waliochipukia maisha na zile familia duni kwa miaka mingi zilitegemea mifugo ya matajiri hawa kwani mfano karibu asilimia 20 ya kaya katika kijiji cha Ring’wani na vijiji vingine vya jirani zilikuwa na ng’ombe wa Nyamarasa wakiwatumia kwa maziwa na kilimo.
Kijiji cha Ring’wani kina sifa ya kutoa wasomi wengi pia, kwani waliwahi kuwapo wasomi kama Marehemu Dr. Caroly Maro Nyanduku, msomi, mtaalamu na dakatari aliyebobea katika kilimo, Genchwere Makenge Ruge Mongoreme wa kwanza kuwa Certified Public Accountant akiwa msomi na mtaalamu wa uhasibu, wapo pia wasomi kama Mwanasheria wa siku nyingi Flavian Makore Ruge, Mtaalamu wa mazao ya maziwa Richard Makenge Ruge (Expert in Dairy and Milk Products Management), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dr. Genchwere Makenge Ruge, Dr. Magori Makenge Ruge, Bwana Kilimo Dr. Genchwere Makenge Ruge, Dr. Nicodemus Masosota Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda na pia aliwahi kutokea mtaalamu wa ramani za ujenzi Kabhori Chacha Matara.
Kijiji hiki kina wasomi vijana wengi sana mfano kutoka katika familia ya Mwalimu Aloyce na nduguye King’orori, pia katika kijiji hiki ndipo anapotokea kamanda mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Kupambana na na Kuzuia Rushwa nchini Ndugu James Ghenchwere Maro Ruge, kuna wasomi wengine kama Mwalimu Sangi Makenge Ruge ambae anatambulika kwa jina la Matare - yeye amekuwa Mkufunzi wa vyuo mbalimbali nchini, Afisa Elimu Taaluma Sec wilaya na Mshauri wa Baraza la Mitihani NECTA kwa miaka 9, Bigeso Makenge Ruge pamoja ma kuwa mjasiriamali hodari lakini pia amefanya kazi katika sekta ya afya binafsi kwa takribani miaka nane sasa ambapo ni mshauri wa maswali ya uendeshaji wa biashara katika sekta ya afya binafsi Tanzania, Ruge Makore Ruge, Matara Kabhori, Nyamase Masosota, Sangi Makenge Ruge, Ruge Maro Mhoni, Sangi Maro Mhoni, Dr. Stephen Maro Muhoni na nduguye Vedastus Maro Mhoni, aliwahi kuwepo Nyanchoghu Masosota na nduguye Nyamase Masosota, wapo wasomi Sabhai Nicholaus, Mantoye Mahende Nyanduku, Mtaalamu wa Sayansi ya Uchunguzi Maalum Manyere Maro Ruge na nduguye mwanasiasa hodari Mhasibu Mapinduzi Maro Ruge na wengineo wengi, wanawake pia hawako nyuma katika shule wakiongozwa na mwanasiasa msomi Dr. Catherine Nyakaho Makore Ruge (CPA) (Mbunge), pia wapo vijana wasomi na wataalamu wa uhasibu kama Mhasibu Sangi Maro Ruge (CPA ) Afisa Mapato Denis Maro Ruge (CPA)
Wapo pia wanasheria mahiri akiwamo Mwanasheria Sabhai Chrispin Nyanduku na Wakili Msomi Pius Maro Ruge huyu ni Mwanasheria mtaalamu Wa Sheria za Kimatifa na Mwanaharakati Wa Haki za Binadamu, na nduguye Mwanasheria chipukizi Ferdinand Makore Ruge.
Kijiji hiki pia kina wakimbiaji mahiri waliowahi kutokea katika historia ya kijiji wakiongozwa na Motibha “Rotwewe” Nyanduku, Daudi Mahende Nyanduku n.k
Pia kijiji hiki kina wasanii na wachekeshaji mahiri katika historia ya kijiji kama Kirabhari Nyamhanga Mataratora ambaye hivi sasa ni mchungaji mwenye kanisa lake, Ghiteghe Matoka na Saghaswe Motibha.
Pia kijiji hiki kina historia ya mafundi waliowahi kufahamika sana kwa ujenzi wa nyumba za jadi na za kisasa wakiongozwa na Marehemu Mzee Rohuro Masiko, Marehemu Mzee Nyamarori Machoghu, Mzee Matoka na wengineo, vipaji hivi vimerithiwa na vijana wao ambao waliviendeleza vipaji hivo kama alivyokuwa mfanya biashara fundi Nyambeta Nyamarori na vijana wa Rohuro kama Maro na Sarighoko.
Kijiji hiki pia kina wazee vijana maarufu wanaofahamika sana na wenye busara mfano Mzee Abas Mresi, Bhoke Nyaruchowa, Simoni, Mwita Marata, Gerald Nyaghesore Nyanduku, Rhobi Masosota Ighonga, Maro Daudi Mahende, Ghati Nesi, Msaghu Masosota n.k
Pia wapo wafanyabishara kama Sabhai Wakori, Saquid Nyamhanga Msaghu, na mfanyabiashara tajiri na chipukizi kijana Moniko Chacha Maighe anayetoa huduma ya biashara kwa kiasi kikubwa kijijini hapo.
Pia kijiji hiki kimebarikiwa wanajeshi wa ngazi za juu na maaskari kama Marehemu Luteni Kanali Meritus Masese Machota, na Ma – Kepteni Machoke Mahemba Chacha Soghora, Mstaafu Faustine Maro Ruge, Nicholaus Ighonga, John Machoghu, John Abas Mresi, Sabhai Nicholaus na wengine wengi.
Marejeo Edit
Kata za Wilaya ya Serengeti - Mkoa wa Mara - Tanzania | ||
---|---|---|
Busawe | Geitasamo | Ikoma | Issenye | Kebanchabancha | Kenyamonta | Kisaka | Kisangura | Kyambahi | Machochwe | Magange | Majimoto | Manchira | Mbalibali | Morotonga | Mosongo | Mugumu mjini | Natta | Nyamatare | Nyambureti | Nyamoko | Nyansurura | Rigicha | Ring'wani | Rung'abure | Sedeco | Stendi Kuu | Uwanja wa Ndege |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mara bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Ring'wani kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |