Wawanda ni kabila la watu kutoka kusini-magharibi mwa nchi ya Tanzania. Wanapatikana katika mkoa wa Songwe, wilaya ya Mbozi, hususani tarafa ya Kamsamba, yenye kata za Kamsamba, Chilulumo, Mkulwe, Mpapa na Ivuna. Wawanda ni neno litokanalo na eneo husika, kwa maana ya watu wa tambarare ya bondeni.

Mwaka 1987 idadi ya Wawanda ilikadiriwa kuwa 24,000 [1].

Lugha yao ni Kiwanda, ambacho hakina tofauti na Kinyamwanga, isipokuwa katika matamshi tu; pia kinaingiliana sana na Kifipa. Kifupi Wawanda, Wanyamwanga na Wafipa ni watu wenye asili moja isipokuwa uongeaji wao unatofautiana kimatamshi lakini maana inabaki kuwa ileile moja.

Shughuli za kujipatia kipato kwa Wawanda ni kilimo, biashara na uvuvi. Wawanda, hasa wanaume vijana, hupendelea kujishughulisha sana na uvuvi wa samaki katika Ziwa Rukwa na Mto Momba ambao hutiririsha maji yake ndani ya Ziwa Rukwa.

Upande wa akina mama wa Kiwanda walio wengi hujihusisha na kilimo na biashara ndogondogo za hapa na pale, pia wapo wafanyabiashara wakubwa wa kabila la Wawanda ambao hubeba samaki na kuwauza Tunduma na maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya Tanzania.

Pia, kutokana na mwingiliano wa watu na makabila mbalimbali, kwa sasa Wawanda wameelimika sana, kiasi kwamba wamewekeza sana kwenye elimu, hasa kwa watoto wao.

Kabila la Wawanda hupendelea sana ugali wa mtama, ulezi, uwele na wachache hula ugali wa dona. Pia Wawanda hupenda kula samaki na nyama. Walio wengi hupendelea kula maboga na viazi vitamu. Halafu kuna matunda ya msimu, kama vile tikitimaji na maembe ambayo hupatikana sana mwezi Desemba.

Wawanda ni wakarimu sana, hasa wao kwa wao, maana hata unywaji wao wa pombe hunywa pamoja, na hualikana kufanya kazi kwa pamoja, hasa kipindi cha kilimo, mavuno na kazi mbalimbali, hivyo kufanya kazi pamoja huwaweka karibu sana muda mwingi.

Wawanda, mtoto akizaliwa, ndugu na majirani huenda kumsalimia mama mtoto wakiwa wamebeba pombe.

Tanbihi

hariri
  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wawanda kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.