Tabianchi

Takwimu za joto, unyevu, shinikizo la anga, upepo, mvua, hesabu ya chembe za anga na vipimo vingine vya hali ya hewa katika mkoa fulani kwa muda mrefu
(Elekezwa kutoka Climate)

Tabianchi (Kiing. climate) inamaanisha jumla ya halijoto, unyevuanga, kanieneo ya angahewa, upepo, usimbishaji na tabia nyingine zinazoathiri hali ya hewa katika sehemu fulani ya uso wa dunia kwa muda mrefu. Tabianchi ni tofauti na halihewa ikitazama vipindi virefu lakini halihewa inatazama hali ya sasa au katika muda mfupi. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema: Tabianchi ni jumla ya halihewa zote zinazoweza kutokea mahali pamoja duniani katika kipindi kisichopungua miaka 30.

Ramani ya dunia inayoonyesha kanda za tabianchi kuanzia ikweta: tropiki, yabisi, wastani, kibara na baridi.

Tabianchi inaathiriwa sana na latitudo yaani umbali na ikweta penye mnururisho mwingi wa jua, uso wa nchi, kimo, kuwa karibu au mbali na magimba ya maji na mikondo ya bahari.

Ufafanuzi wa tabianchi

 
Wastani ya halijoto duniani kwa kila mwezi kwa kipindi cha miaka 30 kuanzia 1961 hadi 1990

Tabianchi huangaliwa hasa katika sayansi za metorolojia na jiografia lakini kuna pia tawi la fizikia linaloichungulia. Kutokana na mitazamo tofauti ya sayansi hizi kuna pia ufafanuzi tofauti kuhusu tabianchi.

Kamati ya "Intergovernmental Panel on Climate Change" (IPCC) ilitoa ufafanuzi ufuatao:

"Tabianchi kwa maana ya kawaida ni "halihewa ya wastani" au kwa umakini zaidi: takwimu za vipimo husika mbalimbali kwa kutazama wastani na ubadilikajibadilikaji katika vipindi vya muda kuanzia miezi hadi miaka mamilioni. Kipindi cha kawaida kiliamuliwa na Shirika la Metorolojia Duniani (World Meteorological Organization - WMO) ni miaka 30. Vipimo hivi ni pamoja na halijoto, usimbishaji na upepo.
Kwa maana pana zaidi tabianchi ni hali ya tabia hizi kwa dunia yote"[1]

Tabia nyingi zinazoathiri tabianchi zinadumu muda mrefu kama vile kimo, uhusiano wa eneo la nchi kavu na eneo la maji, umbali na milima na bahari. Tabia hizi zinabadilika polepole sana katika vipindi vya miaka mamilioni kufuatana na michakato ya gandunia

Athari nyingine kwa tabianchi zinaweza kubadilika katika vipindi vifupi zaidi:

  • mikondo ya bahari inasafirisha joto au baridi kutoka sehemu moja ya bahari kwenda nyingine na hivyo kuathiri nchi.
  • uwingi au uhaba wa mimea inayofunika uso wa nchi unaathiri viwango vya joto la jua vinavyofyonzwa na kiasi cha maji kinachoweza kufyonzwa au kuvukiza.
  • mabadiliko katika kiasi cha gesi joto katika angahewa yanaathiri kiwango cha nichati ya jua kinachofyonzwa na dunia na hivyo kiwango cha kupanda kwa halijoto duniani au kinyume.
  • kuongezeka kwa vumbi hewani kwa mfano kutoka milipuko mikubwa ya volkeno au pigo za meteoriti kubwa sana kunaweza kusababisha kupungukiwa kwa nishati ya jua inayofikia uso wa dunia hivyo kuleta kupoa kwa halijoto.
 
Kiwango cha mnururisho unaofikia uso wa ardhi kinategemea latitudo

Athira kuu zinazoamulia tabianchi

Athira kuu zinazoamulia tabianchi ni latitudo ya eneo, kina chake juu ya usawa wa bahari na hali ya uso wa ardhi yake, pamoja na kuwepo au kutokuwepo karibu na magimba makubwa ya maji, kama bahari au maziwa.

  • latitudo ni msingi kwa kiasi cha nishati (joto, nuru) inayopokelewa kutoka Jua. Maeneo yaliyo karibu na ikweta hupokea zaidi kuliko maeneo yaliyo mbali na ikweta. Hivyo maeneo karibu na ikweta huwa na joto kushnda maeneo karibu na ncha za dunia.
  • uso wa ardhi una athiri; safu ya milima mirefu inaweza kuzuia mawingu hivyo kusababisha mvua kubaki upande mmoja na kuuzuia upande mwingine; misitu mikubwa kama beseni ya Kongo au Amazonas inazalisha uvukizaji mwingi.
  • Halijoto kinapungua kadri eneo liko juu ya usawa wa bahari

Aina za tabianchi

Tabianchi ya eneo huitwa kwa majina kama vile wastani, yabisi, baridi, tundra, tropiki, kiikweta, kimediterania, na kadhalika. Mpangilio unaotumiwa sana ni ile iliyoanzishwa na Vladimir Koeppen mwenye kanda tano:

  • A: tabianchi ya tropiki
  • B: tabianchi yabisi
  • C: tabianchi fufutende ya latitudo za kati
  • D: tabianchi baridi ya latitudo za kati
  • E: tabianchi ya nchani

Hizi kanda tano hugawiwa kwa vikundi vya ngazi ya pili kama vile msitu wa mvua, monsuni, savana, nusutropiki, kibara nyevu, kibahari, kimediteranea, nusuaktiki, tundra, barafu ya nchani, jangwa na kadhalika.

A: Tabianchi ya tropiki

Tabianchi ya tropiki huwa na halijoto ya juu wakati wote kwenye uwiano wa bahari na nyanda za chini. Miezi yote hupatikana na kiwango cha wastani ya halijoto ya 18°C au zaidi. Aina hii hugawiwa kwa vikundi:

Tabianchi ya msitu wa mvua wa tropiki: Miezi yote 12 hupatikana na usimbishaji usiopungua milimita 60. Tabianchi hizi hupatikana hasa katika eneo kati ya latitudo za 5 hadi 10 kusini na kaskazini ya ikweta, mahali pachache hata hadi latitudo ya 25° kutoka ikweta. Muda wote kuna kanieneo ya hewa duni kwa hiyo hakuna tofauti ya majira.
Tabianchi ya monsuni ya tropiki: aina hii ya tabianchi hutokea hasa Amerika Kusini na katika beseni ya Bahari Hindi ikisababishwa na upepo wa monsuni unaobadilika mwelekeo wake kwa utaratibu kimajira. Tabianchi huwa na mwezi kavu zaidi unaotokea mnamo wakati wa solistisi wa wakati baridi katika nusutufe ya dunia (yaani Desemba kwa nusutufe ya kaskazini na Juni kwa nusutufe ya kusini). Usimbishaji uko chini ya 60 mm/mwezi lakini zaidi ya 100 mm /mwaka.
Tabianchi ya savana: inaitwa pia tabianchi ya tropiki nyevu na kavu. Maeneo haya huwa na kipindi cha ukame. Kufuatana na kiasi cha mvua kuna savana tofauti, ama kavu ama nyevu zaidi. Kiwango cha usimbishaji ni kati ya milimita 500 na 1500 kwa mwaka.

B: Tabianchi yabisi au nusuyabisi

Hapa hewa ni kavu. Kuna kiasi cha mvua lakini kutokana na joto na jua maji mengi zaidi hupotea kuliko mvua unaonyesha. Kwa lugha nyingine uvukizaji ni mkubwa kuliko usimbishaji, kwa hiyo hewa ni kavu.

Kama uvukizaji ni kubwa kuliko usimbishaji kwa muda wa miezi 10-12 kila mwaka tabianchi huitwa yabisi. Hapa kiwango cha mvua hakipitii milimita 80 kwa mwaka.

Kama uvukizaji ni kubwa kuliko usimbishaji kwa muda wa miezi 6 - 9 kila mwaka tabianchi huitwa nusuyabisi.

Tabia ya kawaida kwa eneo yabisi ni kupotea kwa mito ambayo haishii baharini au katika maziwa makubwa bali hupotea tu njiani au kuishia katika maziwa ya chumvi au jangwa la chumvi. Maziwa ya chumvi hupatikana pale ambako maji hayapotei kabisa lakini hupungukiwa mno na mishale ya jua hivyo kiasi kinachobaki kama ziwa au matope huwa na chumvi nyingi. Au hata ziwa la chumvi linakauka kwa miezi kadhaa ya mwaka na kuacha uwanja mkubwa wa chumvi tu.

Maeneo penye tabianchi yabisi yapo hasa katika sehemu za nusutropiki zisizofikiwa na upepo wa pasati lakini kuna tabianchi yabisi pia penginepo kwa mfano kwenye milima ya juu au karibu na ncha za dunia.

 
Tabianchi za latitudo za kati a) fufutende b) baridi

C: Tabianchi fufutende ya latitudo za kati

Kanda za tabianchi hii hupatikana kati ya kanda la nusutropiki (lenye halijoto wastani katika mwaka juu ya 20°C) na kanda la baridi (lenye halijoti wastani chini ya 10°C wakati wa mwezi wa joto zaidi).

Kwa hiyo kuna halijoto za wastani juu ya 10 °C katika miezi ya joto zaidi (katika nusutufe ya kaskazini Aprili hadi Septemba) na halijoto ya wastani baina ya −3 °C na 18 °C wakati wa mwezi wa baridi zaidi.

Uoto asilia katika kanda hizi ni hasa misitu; ndani ya bara kuna pia maeneo ya manyasi na pia nusujangwa. Usimbishaji hutokea miezi yote ila tu ni zaidi karibu na bahari inaweza kupungua mbali na bahari.

Hapo kuna maeneo tofauti kama yafuatayo:

  • Tabianchi ya kimediteranea au ya nusutropiki na majirajoto kavu: aina hii hutokea kwa kawaida upande wa magharibi ya bara fulani baina latitudo za 30° hadi 45°. Majirabaridi huwa poa na mvua nyingi; majirajoto kuna halihewa yabisi na joto kutokana na kipaumbele wa kanieneo angahewa ya juu isipokuwa katika maeneo ya pwani ambako mkondo baridi wa bahari inaweza kupoza joto na kuleta ukungu bila mvua.

Mifano ni Cape Town katika Afrika Kusini, Yerusalemu katika Mashariki ya Kati, Los Angeles na San Francisco katika Marekani.

  • Tabianchi nyevu ya nusutropiki hutokea zaidi ndani ya bara au kwenye pwani za mashariki, hasahasa katika digrii za latitudo 30°. Tofauti na tabia za kimediteranea majirajoto kuna unyevuanga juu. Pale ambako tabianchi hizi zinatokea katika Asia ya Mashariki majirabaridi ni yabisi na baridi zaidi kutokana na kanieneo angahewa ya juu kutoka Siberia lakini majirajoto nyevu sana kutokana na athira ya monsuni za Asia ya Kusini Magharibi.
  • Tabianchi ya kibahari: tabianchi hizi hutokea pale ambako athari ya bahari, halijoto yake na upepo zake zinaathiri tabianchi ya bara. Kwa mfano sehemu kubwa za Ulaya ya Magharibi, ya Kati na Kaskazini zinaathiriwa na mkondo wa ghuba unaosukuma maji ya vuguvugu kutoka Ghuba ya Meksiko hadi pwani za Norwei na Urusi ya Kaskazini. Hivyo tabianchi ya sehemu hizi ni tofauti na sehemu za Kanada katika latitudo zilezile: miezi ya majirajoto ni ya kupoa zaidi lakini miezi ya majirabaridi ina halijoto ya juu zaidi kuliko Amerika ya kaskazini ng'ambo ya bahari ya Atlantiki.

D: Tabianchi baridi ya latitudo za kati

Tabianchi hizi zinatokea zaidi ndani ya mabara. Kuna halijoto ya wastani chini ya -1°C wakati wa mwezi baridi na juu ya 10°C wakati wa mwezi wa joto zaidi. Kwenye nusutufe ya kusini ya dunia tabianachi hutokea mahali pachache tu kwa sababu maeneo ya nchi kavu ni madogo zaidi katika nusutufe ya kusini ya dunia.

  • Tabianchi za kibara zenye halijoto ya juu wakati wa majirajoto: mnamo latitudo chini na juu ya 40° halijoto ya wastani ya mwezi wa joto zaidi inafikia kiwangio juu ya 22 °C. Katika Ulaya ya Mashariki kipindi hiki ni yabisi kuliko huko Amerika ya Kaskazini. Katika Asia ya Maskariki kanieneo angahewa ya juu ya Siberia inasukuma tabianchi hii kuelekea kusini zaidi; majirabaridi huwa yabisa sana lakini majirajoto kunatokea kwa unyevuanga juu kutokana na athira monsuni.

E: Tabianchi ya nchani

Hizi tabianchi karibu na ncha za dunia huwa na halijoto wastani chini ya 10 °C mwaka wote.

  • Tabianchi za tundra zinatokea katika kaskazini kabisa za mabara ya Amerika, Asia na Ulaya na kwenye visiwa karibu na Antaktiki. Mwezi wa joto zaidi huwa na halijoto ya wastani baina 0 °C na 10 °C. Sehemu kubwa ya mwaka ina halijoto wastani chini ya 0 °C.
  • Tabianchi ya barafu inapatika Antaktiki, Greenland ya Kati na kwenye eneo la barafu ya kudumu juu ya bahari ya Aktiki. Miezi yote huwa na halijoto wastani chini ya 0 °C.

Mabadiliko ya tabianchi

Mabadiliko ya tabianchi hutokea kieneo au hata duniani kote kila baada ya muda fulani. Mabadiliko hayo yanatazamwa moja kwa moja kutokana na vipimo vya angahewa kwa miongo ya miaka au kwa kufanyia utafiti viini vya mashimo yaliyotobolewa kwenye ardhi au barafu ya Aktiki.

Mabadiliko hayo yanaweza kusababishwa na mabadiliko ya kiasi cha nuru ya Jua kinachofika duniani pamoja na mabadiliko katika angahewa ya dunia. Mabadiliko ya tabianchi yaliyojadiliwa sana tangu mwisho wa karne ya 20 yanahusu kuongezeka kwa gesi joto kutokana na shughuli za binadamu, hasa kuchomwa kwa fueli kisukuku.

Marejeo