Meksiko

nchi katika Amerika ya Kaskazini
(Elekezwa kutoka Mexico)


Meksiko ni nchi kubwa (km2 1,972,550) inayohesabiwa kijiografia kuwa sehemu ya Amerika ya Kaskazini au pengine ya Amerika ya Kati. Kwa vyovyote kiutamaduni ni sehemu ya Amerika ya Kilatini.

Estados Unidos Mexicanos
Muungano wa Madola ya Mexiko
Bendera ya Mekiko Nembo ya Mekiko
Bendera Nembo
Kaulimbiu ya taifa: (hakuna)
Wimbo wa taifa: Himno Nacional Mexicano
Lokeshen ya Mekiko
Mji mkuu Mji wa Mexiko (Kihisp.: Ciudad de Mexico)
19°03′ N 99°22′ W
Mji mkubwa nchini Mji wa Mexiko (Kihisp.: Ciudad de Mexico)
Lugha rasmi (hakuna kitaifa)
Kihispania (hali halisi)
Serikali Shirikisho la Jamhuri
Claudia Sheinbaum
Uhuru
Imetangazwa
imetambuliwa

16 Septemba 1810
27 Septemba 1821
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
1,972,550 km² (ya 15)
2.5%
Idadi ya watu
 - 2023 kadirio
 - 2000 sensa
 - Msongamano wa watu
 
129,875,529 (ya 10)
101,879,171
61/km² (ya 142)
Fedha Peso (MXN)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
(UTC-8 to -6)
varies (UTC)
Intaneti TLD .mx
Kodi ya simu +52

-


Imepakana na Marekani upande wa kaskazini. Upande wa kusini majirani ni Guatemala na Belize.

Ina pwani ndefu na bahari za Pasifiki na Ghuba ya Meksiko.

Ina muundo wa shirikisho ya majimbo 32 yanayojitawala.

Meksiko ilikuwa nchi ya staarabu za juu ya Waazteki na Wamaya hadi kuvamiwa na Hispania mnamo mwaka 1521, halafu koloni la Hispania hadi uhuru wa mwaka 1821.

Kwa sasa ni nchi ya 15 kiuchumi duniani, hivyo ni pia mwanachama wa kundi la G20.

Mji mkuu ni Mexico City, ambao katika eneo lake lote una watu zaidi ya milioni 20.

Historia

hariri

Nchi jinsi ilivyo leo imeundwa na wakoloni Wahispania walioivamia kuanzia mwaka 1519 na kuvunja utawala wa milki za wenyeji kama Azteki na Maya.

Kabla ya uvamizi wa Hispania

hariri

Watu wa kwanza waliofika huko kutoka kaskazini walikuwa Waindio, wajukuu wa wahamiaji walioingia Amerika kutoka Asia ya Kaskazini. Hakuna uhakika kufika huko kulitokea lini: labda miaka 10,000 iliyopita[1].

Hao Waindio walikuwa wakulima hodari sana na mazao mbalimbali ambayo leo ni msingi wa chakula kote duniani yalianzishwa na kupandishwa nao, yakiwa pamoja na mahindi, mboga na nyanya. Kilimo cha mahindi hukadiriwa kilianzishwa takriban mnamo mwaka 9000 KK[2][3].

 
Sanamu ya kichwa ya Kiolmeki

Kilimo kiliweka msingi kwa vijiji na jamii zilizoshirikiana katika maeneo makubwa. Miji ya kwanza inajulikana kuanzia takriban mwaka 1500 KK.

Staarabu mbalimbali zilistawi na kukua katika maeneo ya pwani (Waolmeki, Wamaya) na katika nyanda za juu za Mexico ya kati (Wazapoteki, Wamixeki, Watolteki, Waazteki).

Waolmeki

hariri

Ustaarabu wa kwanza unaojulikana ulikuwa wa Waolmeki baina ya 1500 KK na 400 KK. Habari zao zinajulikana kutokana na akiolojia na mabaki ya miji na sanaa yao. Waolmeki walijenga miji wakaacha mifano ya sanaa yenye kiwango cha juu.

Waliishi katika kanda la pwani la Mexiko katika majimbo ya leo ya Veracruz na Tabasco. Ni watu wa kwanza katika Mexiko wanaojulikana kubuni mwandiko na kalenda, mchezo wa mpira na ujenzi wa piramidi za hekalu. Walikuwa hodari sana kuchonga sanamu ya mawe, hasa vichwa vikubwa vyenye urefu WA zaidi ya mita 3. Walifaulu kuunda sanaa hii bila kujua vifaa vya metali.

 
Hekalu - piramidi ya Kimaya
 
Ukurasa kutoka kitabu cha Kimaya - maandishi ya hiroglifi

Sanamu nyingine inayorudirudi ni mtu-jagwaa inayounganisha sehemu ya maumbile ya binadamu na jagwa. Takriban mwaka 400–300 KK miji yao iliachwa na wakazi; hakuna uhakika ni nini iliyosababisha mwisho wa ustaarabu huu.

Wamaya

hariri

Upande wa mashariki wa Waolmeki ustaarabu wa Wamaya ulianza tangu takriban mwaka 2000 KK. Wamaya walikalia rasi ya Yucatan pamoja na Guatemala na Belize ya leo. Waliishi katika vijiji na miji iliyojitegemea na kugombana kati yao mara kwa mara.

Wamaya walibuni mwandiko wa hiroglifi wenye alama nyingi kupita maandishi mengine katika Amerika ya Kale na kutunga vitabu. Waliendeleza pia hisabati, wakijua namba "sifuri" na kuboresha mfumo wa kalenda.

Walikuwa hodari sana katika astronomia yaani elimu ya nyota. Walipamba miji yao kwa majengo makubwa na mazuri na kuwa wafanyabiashara hodari. Sanaa yao ilijua uchongaji wa mawe na pia uchoraji.

Jamii ya Wamaya ilifikia kiwango cha juu kuanzia mwaka 500 KK wakati miji mikubwa ya kwanza ilipotokea. Mnamo mwaka 800 BK jamii za Wamaya katika Yucatan ziliporomoka; wataalamu wengi huamini ya kwamba mabadiliko ya ekolojia na halihewa pamoja na kuchoka kwa rutuba ya ardhi yalisababisha kutoka kwa watu katika makazi ya awali.

Lakini ustaarabu huu uliona tena kipindi cha kustawi katika maeneo mengine hadi kuja kwa Wahispania. Miji mbalimbali ya Wamaya iliendelea kujitetea dhidi ya wavamizi na Nojpeten, mji wa mwisho wa kujitegemea ulitekwa mwaka 1696 tu.

Teotihuacan

hariri
 
Barabara ya mahekalu na piramidi ya jua mjini Teotihuacan

Teotihuacan ilikuwa mji mkubwa katika nyanda za juu, karibu na Mexico City ya leo. Kuanzia mwaka 100 KK hadi takriban 550 BK ilikuwa mji mkubwa wa Amerika, pia moja kati ya miji mikubwa duniani na kitovu cha utamaduni kilichoathiri staarabu zote za Mexiko.

"Teotihuacan" ilikuwa jina la Waazteki kwa mji huu, jina la kienyeji halikuhifadhiwa. Maana ya jina ni "mahali pa kuzaliwa kwa miungu". Wakati wa maendeleo yake mji ulikuwa na eneo la kilomita za mraba 30 ukiwa na wakazi angalau 150,000, labda hata 250,000 walioishi humo[4].

Hakuna uhakika ni akina nani waliojenga Teotohuacan. Mji wote ulipangwa kwa kufuata barabara mbili zilizoelekea kaskazini-kusini na mashariki-magharibi. Hekalu kubwa na piramidi zinaonyesha umuhimu wa dini, na mabaki ya nyumba za wakubwa na watu wa kawaida yanaruhusu kupata picha ya jamii iliyoishi hapa.

Teotohuacan ilikuwa kitovu cha biashara ya misafara ya mbali na pia ya elimu. Ukubwa wa mji unaonyesha kiwango cha juu cha utawala na ushirikiano kati ya watu wake.

Katika karne ya 6 BK sehemu kubwa ya majengo iliharibika na kuchomwa. Hakuna uhakika kama hii ilikuwa tokeo la uvamizi kutoka nje au vurugu au mapinduzi ndani ya mji. Baada ya maharibio yale mji ulianza kurudi nyuma na idadi ya watu kupungua. Mnamo mwaka 750 BK watu wote waliondoka: ni maghofu ya majengo makubwa tu yaliyobaki[5].

Milki ya Azteki

hariri
 
Askari wa Azteki

Kuanzia mwaka 1325 kabila la Azteki likaunda mji wa Tenochtitlan kwenye kisiwa cha ziwa la Tezcoco. Waazteki wakaendelea kuunda milki kubwa lililoeena na kutawala sehmu kubwa ya nyanda za juu za Mexiko. Msingi wa milki yao ilikuwa ushirikiano na mji miwili jirani iliyounda mwungano wa pande tatu lakini Waazteki waliendelea kuwa mshiriki mkuu na mtawala wa Tenochtitlan hatimaye alikuwa mtawala mkuu. Walishambulia maeneo ya miji na makabila jirani na kuwalazimisha kulipa kadi kwao. Kama walikubali kutoa kodi kila mwaka na pia kushiriki katika vita za milki watawala wa kienyeji waliruhusiwa kuendelea na utawala wa ndani. Dini yao iliweka uzito kwa sadaka za binadamu waliochinjwa kwenye mahekalu ya miungu yao. Waliunda mfumo wa mikataba ya vita na milki nyingine ambako walikutana kwa mapigano yaliyo kubaliwa awali kwa shabaha ya kukamata wafungwa wengi iwezekanavyo na kuwatoa kama sadaka kwa miungu hekaluni baadaye.

Uvamizi wa Wahispania

hariri

Mwaka 1519 Mhispania Hernan Cortez alifika kwenye pwani la Mexiko. Katika miaka iliyofuata alifaulu kuendelea hadi mji wa Tenochtitlan akiongozana na kundi la Wahispania mamia kadhaa. Cortez aliweza kuungana na miji na makabila ya Waindio waliochoka utawala wa Azteki na kumpa askari za usaidizi. Mwaka 1520 waliingia Tenochtitlan kama wageni wa mfalme Montezuma II wakaendelea kumkamata lakini baada ya kifo cha mfalme walifukuzwa wakakimbia kwa matatizo katika "usiku wa huzuni" (Kihisp. noche triste). Waazteki walidhoofishwa sana kutokana na epidemia ya ugonjwa wa ndui[6]. Cortez aliweza kukusanya jeshi kubwa la Waindio waliopinga Waazteki akavamia na kuharibu Tenochtitlan mwaka 1521 na kwenye magofu ya mji huu alianzisha mji mpya wa Mexico City (Kihisp. Ciudad de Mexico).

Ukoloni

hariri
 
Jinsi Bikira Maria alivyomtokea Juan Diego kwenye kilima Tepeyac, Mexico City.

Baada ya Hispania kuteka sehemu kubwa ya nchi mwaka 1521, liliundwa koloni la Hispania Mpya chini ya makamu wa mfalme.

Bila kujali ukatili wa Wahispania, Waindio walijiunga haraka na Kanisa Katoliki kuhusiana na njozi ya mwenzao Juan Diego aliyetokewa na Bikira Maria huko Guadalupe (12 Desemba 1531), wakachanganyikana na wavamizi na kufanya taifa jipya lenye sura ya kichotara, kiasi kwamba wengi wanajiona "mestizos" (machotara) hata wasipokuwa na damu mchanganyiko.

Tangu uhuru hadi leo

hariri

Baada ya karne tatu na baada ya vita vya ukombozi, mwaka 1821 wakazi walijipatia uhuru kwa jina la Mexico.

Vita ya uhuru

hariri

Mfano wa uhuru wa Marekani mwaka 1776 ulikuwa na athira pia kati ya wasomi wenyeji wa Mexiko. Jamii ya kikoloni iliundwa juu ya ubaguzi kati ya Kreoli (walowezi wenye asili ya Hispania bila mchanganyiko na Waindio), Mestizos (asilimia kubwa ya wenyeji waliotokana na ndoa za wanaume Wahispania na wanawake Waindio) na Waindio wenyewe. Lakini vyeo vyote vya juu, kama maafisa wa juu wa serikali, vilipatikana pekee kwa watu waliozaliwa Hispania na kutumwa Mexiko. Mawazo ya uhuru yalianza kupatikana kati ya Kreoli na Mestizos wa matabaka ya juu.

Chanzo cha vita ya uhuru kilikuwa mabadiliko katika Ulaya. Napoleon mtawala wa Ufaransa alimkamata mfalme Ferdinand VII wa Hispania akamlazimisha kujiuzulu na kumpa kaka yake Yosefu Napoleon ufalme wa Hispania. Hatua hii ilifuatwa na wimbi la uasi nchini Hispania dhidi ya mfalme Mfaransa.

Katika Hispania Mpya (Mexico) kamati za miji kadhaa zilizoongozwa na Kreoli ziliapa kumfuata mfalme mfungwa halali pekee. Kamati Kuu ya Mexiko City ilitaka kuanzisha bunge la pekee kwa sababu Hispania haikuwa tena na serikali halali. Mfalme mdogo (gavana mkuu) alikubali. Viongozi wengine walitangaza ilhali mfalme halali hayuko tena sasa, nguvu yote iko mkononi mwa wananchi. Hapo Wahispania katika koloni walioshika vyeo vikuu waliamua kumpindua mfalme mdogo na kuwakamata viongozi wa Kreoli.

Uasi ulifaulu lakini vikundi vidogo vya wapinzani wa uhuru kutoka Hispania waliendelea kukutana nchini na kukusanya viongozi. Hatimaye padre Kreoli Miguel Hidalgo y Costilla alikusanya jeshi la wanamgambo wakulima Waindio na Kreoli akapigana na jeshi lililokuwa chini ya mamlaka ya maofisa Wahispania. Miguel Hidalgo alishindwa na kuuawa, lakini hii ilikuwa chanzo cha uasi mkubwa ambao Wakreoli na wakulima Waindio walipigana na jeshi lililofuata amri ya Wahispania katika koloni.

Mwaka kiongozi wa upande wa migambo ya uhuru Guerrero na jenerali wa jeshi la serikali Agustin de Iturbide walikutana wakapatana kuungana. Vikosi vingi vya jeshi la kikoloni vilihamia upande wao. Gavana mpya aliyefika kutoka Hispania aliamua kukubali uhuru uliotangazwa tarehe 28 Septemba 1821. Iturbide alikuwa rais wa kwanza na baadaye kwa kipindi kifupi Kaisari wa Mexiko hadi kujiuzulu mwaka 1823: hapo Mexiko ikaendelea kuwa jamhuri.

Karne ya 19

hariri
 
Maeneo yaliyoongezwa, yaliyotengwa au kujitenga na Mexiko tangu uhuru wa mwaka 1821: A) Maeneo yaliyotwaliwa na Marekani (nyekundu, kichungwa, nyeupe), Chiapas kuchukuliwa kutoka Guatemala (buluu), eneo la Yucatan lililotwaliwa (nyekundu) na maeneo ya Shirikisho la Amerika ya Kati (zambarau).

Katika miaka iliyofuata nchi haikupata msimamo imara kisiasa wala kiuchumi. Serikali mara nyingi zilikuwa hafifu na kubadilishana.

Vikundi vya ushikiliaji ukale na uliberali vilipigana hadi kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka wa uhuru maeneo ya kusini yalijitenga na kuwa Shirikisho la Amerika ya Kati lililofarakana baadaye kuwa nchi za Guatemala, Honduras, El Salvador, Nikaragua na Costa Rica.

Mwaka 1835 Marekani ilijaribu kununua maeneo ya Texas na Kalifornia lakini Meksiko ilikataa. Hata hivyo utawala wa Mexiko kuhusu maeneo haya ya kaskazini yake ulikuwa hafifu na wa juujuu tu, Waindio walijitegemea hali halisi nje ya miji michache. Hivyo serikali ya Mexiko ilikaribisha walowezi kutoka Marekani kuhamia Texas. Hao walowezi wenye utamaduni wa Kiingereza-Kimarekani walitangaza uhuru wao mwaka 1836 wakaunda Jamhuri ya Texas iliyochukuliwa na Marekani mwaka 1845 kuwa jimbo lake.

Hatua hii ilisababisha Vita ya Marekani na Mexiko ya miaka 18461848. Mexiko ikashindwa na kaskazini yote ikawa sehemu ya Marekani (Kalifornia, New Mexico, Arizona, Nevada, Utah na Colorado, jumla theluthi moja ya eneo lake lote.

Mexiko ilishambuliwa mara mbili na Ufaransa kutokana na madai juu ya madeni ya taifa kwa raia au benki za nje. Kwenye vita ya keki (1838-1839) Ufaransa ilidai fidia kwa uharibifu uliotokea katika duka la keki la Mfaransa mjini Mexiko na manowari za Ufaransa zilishambulia bandari za Mexiko hadi rais wake kukubali deni hili.

Mashambulio makubwa zaidi yalifuata mwaka 1861. Mexiko ilishindwa kulipa madeni kwa mataifa ya nje. Ufaransa chini ya Napoleon III iliamua kufanya Mexiko nusu-koloni yake; jeshi la Ufaransa ilivamia nchi, kufukuza serikali na kumweka Mwaustria Maximilian I kama "Kaisari wa Mexiko". Serikali ya rais Benito Juarez ilipinga uvamizi huu kwa njia ya vita ya wanamgambo na mwaka 1866 Wafaransa walipaswa kuondoka tena, Maximilian aliuawa mwaka 1867.

Karne ya 20

hariri

Utawala wa rais Porfirio Díaz uliendelea kwa miaka zaidi ya 30 na kuwasha moto ya mapinduzi ya Mexiko alipojaribu kushinda tena kwa udanganyifu mwaka 1910.

Miaka hadi 1921 vita ya wenyewe kwa wenyewe iliharibu sehemu kubwa za nchi. Kuna makadirio ya kwamba wananchi milioni 1,5 (kati ya milioni 15) waliuawa na zaidi ya 200,000 walikuwa wakimbizi, hasa kwenda Marekani[7].

Mwaka 1917 katiba mpya ya nchi ilitolewa na mkutano wa bunge maalumu. Katiba hii ilikuwa katiba ya kwanza duniani kutangaza haki za kijamii. Hizo haki zililenga kutunza na kuboresha hali ya wananchi wenye maisha magumu kama wafanyakazi na wakulima dhidi ya mabepari na wenye mashamba makubwa[8]. Katiba hii iliweka mamlaka nyingi mikononi mwa rais wa taifa anayechaguliwa na wananchi wote kwa kipindi kimoja cha miaka 6, halafu hawezi kuchaguliwa tena. Shabaha nyingine ya vifungu katika katiba ilikuwa kupunguza uwezo wa Kanisa Katoliki kuathiri siasa na jamii na hatimaye kukomesha imani hiyo.

Siasa hii dhidi ya Ukristo iliendelea chini ya rais Calles na kusababisha kipindi kingine cha vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 1926-1929. Katika mapigano hayo yaliyoitwa La Cristiada wakulima wengi walichukua silaha kwa jina la Kristo Mfalme dhidi ya jeshi la serikali ili kutetea uhuru wa dini, wakipinga kufungwa kwa makanisa, kuzuiwa ibada mbalimbali za hadhara na kuuawa kwa mapadre kama Mtakatifu Kristofa Magallanes na wenzake. Vita hivyo vilisababisha vifo 250,000 na idadi hiyohiyo ya wakimbizi waliojisalimisha Marekani.

Baada ya mapinduzi mamlaka ilichukuliwa na Chama cha kitaifa cha mapinduzi (Partido Nacional Revolucionario PNR) kilichoendelea kutawala kwa miaka 71 kuanzia 1929 hadi 2000.

Wakazi ni 129,875,529: wengi wao ni machotara wenye damu ya Wahindi wekundu (31/55% hivi) na Wazungu (42/65% hivi). Wenye asili ya Ulaya tu ni 9/18%. Wenye asili ya Afrika ni 2%.

Ni nchi ya kwanza duniani kwa wingi wa watu wanaotumia lugha ya Kihispania ambayo ni lugha ya taifa, lakini wengine (9.8/14.9%) wanaendelea kutumia lugha asilia tangu kabla ya ukoloni kama vile Nahuatl, Yukatek Maya, Mixtek na Zapotek.

Nchini wanaishi Wamarekani milioni 1, halafu wahamiaji wengine kutoka Amerika ya Kati, Lebanon, nchi nyingine za Asia n.k. Kinyume chake, Wameksiko 13 milioni wako Marekani, na raia wengine 23 milioni wa nchi hiyo wana asili ya Meksiko.

Upande wa dini walio wengi ni wafuasi wa Yesu Kristo katika Kanisa Katoliki (77.7%) au madhehebu mengine (11.2%). Ni nchi ya pili duniani kwa wingi wa Wakatoliki, baada ya Brazil, na karibu nusu kati yao wanashiriki ibada kila wiki. Wasio na dini ni 8.1%.

Majimbo ya Mexiko

hariri
  1. Aguascalientes
  2. Baja California
  3. Baja California Sur
  4. Campeche
  5. Chiapas
  6. Chihuahua
  7. Coahuila
  8. Colima
  9. Durango
  10. Guanajuato
  11. Guerrero
  12. Hidalgo
  13. Jalisco
  14. Mexico
  15. Michoacán
  16. Morelos
  17. Nayarit
  18. Nuevo León
  19. Oaxaca
  20. Puebla
  21. Querétaro
  22. Quintana Roo
  23. San Luis Potosí
  24. Sinaloa
  25. Sonora
  26. Tabasco
  27. Tamaulipas
  28. Tlaxcala
  29. Veracruz
  30. Yucatán
  31. Zacatecas
 
Ramani ya Mexiko
 
 
 
 

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Michael S. Werner (January 2001). Concise Encyclopedia of Mexico. Taylor & Francis. pp. 386–. ISBN 978-1-57958-337-8
  2. A single domestication for maize shown by multilocus microsatellite genotyping, Proc Natl Acad Sci U S A. 2002 Apr 30; 99(9): 6080–6084. doi: 10.1073/pnas.052125199
  3. ""The Evolution of Corn". University of Utah HEALTH SCIENCES. Retrieved 2 January 2016". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-04-01. Iliwekwa mnamo 2016-03-20.
  4. "Architecture, Astronomy, and Calendrics in Pre- Columbian Mesoamerica, Vincent H. Malmstrom" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2006-11-03. Iliwekwa mnamo 2016-03-21.
  5. Teotihuacan, Department of Arts of Africa, Oceania, and the Americas, The Metropolitan Museum of Art October 2001
  6. Ndui ilikuwa ugonjwa iliyokuwa kawaida katika Ulaya wakati ule lakini ilikuwa ugonjwa mgeni kwa wenyeji wa Amerika ambao walikosa kinga dhidi yake; hivyo ilikuwa kati ya magonjwa wa kuambukizwa kutoka Ulaya yaiyoua Waindio wengi katika karne zilizofuata.
  7. Robert McCaa, "Missing millions: the human cost of the Mexican Revolution." Mexican Studies 19#2 (2001)
  8. Akhtar Majeed, Ronald Lampman Watts, and Douglas Mitchell Brown (2006). Distribution of powers and responsibilities in federal countries. McGill-Queen's Press. p. 188. ISBN 0-7735-3004-5.

Marejeo

hariri
  • Camp, Roderic A. Politics in Mexico: Democratic Consolidation Or Decline? (Oxford University Press, 2014)
  • Davis, Diane. Urban leviathan: Mexico City in the twentieth century (Temple University Press, 2010)
  • Domínguez, Jorge I (2004). "The Scholarly Study of Mexican Politics". Mexican Studies / Estudios Mexicanos. 20 (2): 377–410.
  • Edmonds-Poli, Emily, and David Shirk. Contemporary Mexican Politics (Rowman and Littlefield 2009)
  • Kirkwood, Burton. The History of Mexico (Greenwood, 2000) online edition Ilihifadhiwa 24 Desemba 2009 kwenye Wayback Machine.
  • Krauze, Enrique (1998). Mexico: Biography of Power: A history of Modern Mexico 1810–1996. New York: Harper Perennial. uk. 896. ISBN 0-06-092917-0.
  • Meyer, Michael C.; Beezley, William H., whr. (2000). The Oxford History of Mexico. Oxford University Press. uk. 736. ISBN 0-19-511228-8.
  • Levy, Santiago. Good intentions, bad outcomes: Social policy, informality, and economic growth in Mexico (Brookings Institution Press, 2010)
  • Meyer, Michael C., William L. Sherman, and Susan M. Deeds. The Course of Mexican History (7th ed. Oxford U.P., 2002) online edition Ilihifadhiwa 2 Februari 2011 kwenye Wayback Machine.
  • Russell, Philip (2010). The history of Mexico: from pre-conquest to present. Routledge. ISBN 978-0-415-87237-9. Iliwekwa mnamo Julai 9, 2010.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Tannenbaum, Frank. Mexico: the struggle for peace and bread (2013)
  • Werner, Michael S. ed. Encyclopedia of Mexico: History, Society & Culture (2 vol 1997) 1440pp online edition Ilihifadhiwa 24 Januari 2010 kwenye Wayback Machine.
    • Werner, Michael S. ed. Concise Encyclopedia of Mexico (2001) 850pp; a selection of unrevised articles

Viungo vya nje

hariri
 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu maeneo ya Mexiko bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Meksiko kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.