Historia ya Iceland

Historia ya Iceland inahusu eneo ambalo siku hizi linaunda Jamhuri ya Iceland.

Historia ya awali hariri

Iceland iko mbali na bara la Ulaya na la Amerika tena katika mazingira ya baridi. Hivyo inaaminika haikuwa na watu kabisa hadi mwaka 800 BK. Wataalamu hawakubaliani kama ni mabaharia kutoka Norwei au Eire waliobahatika kufika kisiwani na kujenga makao ya kwanza.

Hakika waliofika wengi kidogo walikuwa Waviking au Wanorwei wa kale katika karne ya 9. Kama Waeire walikuwepo walifukuzwa au kuwa sehemu za Waviking. Mtu wa kwanza aliyekumbukwa kwa jina alikuwa Flóki Vilgerðarson.

Waviking waliofika walikuja pamoja na familia na watumishi au watumwa wao. Mnamo mwaka 930 machifu na wasimamizi wa familia zilizokuwepo walipatana kuhusu aina ya katiba kwa Iceland. Walianzisha bunge la Althing. Ulikuwa mkutano wa watu 36 walioitwa "Godi" wakiwa na cheo cha kuunganisha madaraka ya chifu, hakimu na kuhani. Utaratibu huu wa kuwa na bunge umeendelea hadi leo bila kusimama. Hivyo Iceland ni nchi ya pekee ambako utaratibu wa kidemokrasia wa kale umeendelea wakati katika nchi za Ulaya nafasi ya wafalme au watawala wengine iliongezeka na kumeza haki zote za watu wa kawaida.

Mwaka 985 Mwiceland aligundua njia ya kufika Greenland na baadaye Amerika ya Kaskazini. Mviking "Erik Mwekundu" alifukuzwa kisiwani kwa sababu alikuwa mwuaji. Alielekea magharibi kwa jahazi yake na kufika kwanza Greenland halafu pwani ya Kanada ya leo. Aliita bara jipya "nchi ya mzabibu" kwa sababu alikuta aina ya mizabibu isipokuwa bila matunda.

Chini ya Norwei na Denmark hariri

Tangu 1262 uhuru wa Iceland ulikwisha kwa sababu viongozi walijiunga na Ufalme wa Norwei. Iceland iliendelea kuwa na bunge lake na madaraka mbalimbali - hasa kwa sababu usafiri uliendelea kuwa mgumu - lakini mabwana wakuu walikuwa sasa wafalme wa Skandinavia, kwanza Wanorwei, baadaye Wadenmark.

Mwaka 1918 Denmark ilirudisha madaraka yote ya serikali kwa Waiceland wenyewe isipokuwa mfalme wa Denmark aliendelea kama Mkuu wa nchi.

Kuanzia uhuru hariri

Wakati wa Vita Kuu ya Dunia ya Pili Denmark ilivamiwa na Ujerumani na Althing iliamua ya kwamba kuanzia sasa kisiwa kitajitawala kabisa. Mwaka 1944 Iceland ilipata uhuru kamili.

Baada ya vita kwisha Iceland ilipata kuwa nchi mwanachama ya NATO lakini haina wanajeshi hadi leo. Ilifanya mkataba na Marekani ya kuwa Wamarekani wanapewa haki ya kutumia kituo cha ndege kisiwani na kwa upande mwingine wanaahidi kutetea Iceland.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Iceland kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.