Uzima wa milele

(Elekezwa kutoka Immortality)

Uzima wa milele ni hali ya kuishi bila mwisho.[2]

Fountain of Eternal Life huko Cleveland, Ohio, Marekani. Inamaanisha "Binadamu kuinuka juu ya kifo, akimuelekea Mungu na Amani".[1]

Biolojia inaonyesha kuwa uhai wa mwili una mipaka, wala sayansi na teknolojia hazijaweza kuivuka.

Hata hivyo, toka zamani binadamu ameonyesha kwa njia nyingi hamu ya kuendelea kuishi kwa namna moja au nyingine.

Utenzi wa Gilgamesh, kimoja kati ya vitabu vya kwanza vya fasihi andishi (karne ya 22 KK hivi), kinasimulia habari za mtu aliyetaka kuishi milele.[3]

Katika dini mbalimbali

Katika dini mbalimbali, uzima wa milele unatarajiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (au miungu) kama tuzo kwa matu aliyefuata uadilifu wakati wa kuishi duniani.

Katika Ukristo

Neno “uzima wa milele” ni adimu katika Agano la Kale, ambamo yote yanaelekea ujio wa Mwokozi aliyeahidiwa. Kumbe katika mahubiri ya Yesu yote yanaelekea moja kwa moja uzima wa milele. Tukizingatia kwa makini maneno yake tutaona jinsi uzima huo ulivyo tofauti na maisha yajayo yaliyozungumziwa na wanafalsafa bora (k.mf. Plato) kama hali ya kimaumbile tu na isiyo ya hakika. Mwokozi anaongelea kwa hakika uzima wa milele, bora, usio na jana, leo wala kesho, unaopita maumbile na usiopimika, kama ule wa ndani ya Mungu, kwa kuwa unashiriki umilele wake usiobadilika. Uzima wa milele ndio ahadi kuu ya Yesu kwa wafuasi wake, hasa kadiri ya Injili ya Yohane. Sura ya 17 ya Injili hiyo inafafanua uzima wa milele kuwa uhusiano na Mungu na Yesu Kristo mwenyewe.

Kwa ahadi hiyo, sisi wanyonge tunaweza kushiriki uzima wa milele wa Mungu: hapa duniani katika mwanga hafifu wa imani, na kisha kufa katika uangavu wa utukufu usiofifia kamwe. Kwa kuwa lengo la Baba ni kwamba tuungane na Yesu Mwanae kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ili tuwe na utukufu wake. “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3). “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa” (2Pet 1:3-4). Sisi tuliobatizwa tunaitwa “wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo!” (1Yoh 3:1). Kwa sababu tumesadiki kwamba “Mungu ni upendo” (1Yoh 4:8) na kwamba “hakuna lisilowezekana kwa Bwana” (Lk 1:37). “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu” (Gal 4:6-7).

Yesu alifundisha kuwa “njia imesonga iendayo uzimani” (Math 7:14) na kuwa tukitaka kuupata ni lazima tuache dhambi na kushika amri za Mungu (taz. Math 19:17). Mara kadhaa alisema kuwa anayemwamini “yuna uzima wa milele” (Yoh 5:24; 6:40,47), maana yake anayemsadiki kuwa Mwana wa Mungu kwa imani hai, inayoambatana na upendo na utekelezaji wa amri, ameshaanza kuwa na uzima wa milele. Ndivyo alivyosema tangu aanze kuhubiri, “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao... Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa... Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu” (Math 5:3,6,8). Uzima wa milele ni kushiba huko na kumuona Mungu katika ufalme wake. Kwa namna ya pekee, wanaoteswa kwa kufanya atakavyo Mungu wanaambiwa, “Furahini na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (Math 5:12). Yesu akajieleza zaidi kabla ya mateso yake aliposema, “Baba... ulimpa Mwanao mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:1-3).

“Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yoh 3:2), yaani si kwa kuzingatia mng'ao wa sifa zake katika viumbe (vile vinavyoonekana, pamoja na roho za watakatifu zinazojitokeza katika maneno na matendo yao), bali moja kwa moja jinsi alivyo. “Wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1Kor 13:12). Mtume Paulo hakusema nitamjua ninavyojijua mpaka ndani; kwa sababu najifahamu kuliko wengine, lakini mimi pia sielewi yote niliyonayo ndani, k.mf. siwezi kupima uzito wote wa dhambi zangu. Mungu tu ananijua fika: yeye tu anaelewa kikamilifu siri za moyo wangu. Mbinguni nitamjua anavyonijua, moja kwa moja, pasipo kupitia kiumbe chochote wala wazo lolote la kimaumbile, kwa sababu hakuna wazo la namna hiyo linaloweza kumchora Mungu na ukweli wake usio na mipaka. Kila wazo la namna hiyo linazingatia sifa mojawapo ya Mungu (k.mf. wema). Mawazo hayo mbalimbali hayatoshi kutujulisha dhati yake, umoja usiogawanyika kamwe. Mawazo hayo yanahusiana na uzima wake wa ndani kama vile rangi saba za upinde wa mvua zinavyohusiana na mwanga mweupe ambao zinatokana nao. Hapa duniani sisi ni kama tumeona hizo rangi saba na sasa tunatamani kuona huo mwanga mweupe unaozisababisha. Kabla hatujaona umungu wenyewe hatuwezi kuona ulinganifu wa dhati wa sifa zake, hasa huruma isiyo na mipaka na haki isiyo na mipaka. Mawazo yetu kuhusu sifa za Mungu ni vipande tu vya sura nzima, ambavyo vinaleta picha ya Mungu isiyopendeza vya kutosha. Tukifikiria haki yake, inaonekana ni kali mno, na tukifikiria upendeleo wa huruma yake unaonekana kwenda kinyume cha haki. Tukitafakari zaidi tunakiri kuwa ndani ya Mungu haki na huruma ni kitu kimoja, hazitofautiani kweli. Tunaungama hivyo kwa hakika, lakini hatujaona ulinganifu wa dhati wa sifa hizo, kwa kuwa unadai tutazame umungu ulivyo, moja kwa moja, pasipo mawazo ya kimaumbile.

Mtazamo huo ndio uzima wa milele. Nani anaweza kueleza ukuu usiopimika wa furaha na upendo utakaokuwemo ndani mwetu kutokana na mtazamo huo? Upendo wa Mungu wenye nguvu na wa moja kwa moja, hivi kwamba hakuna lolote litakaloweza kuupunguza; kwa upendo huo tutamfurahia hasa Mungu kuwa Mungu, mtakatifu, mwenye haki na huruma pasipo mipaka, na tutaabudu mipango yote ya maongozi yake iliyolenga kufunua wema wake. Tutazama katika heri yake, alivyosema Mwokozi, “Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako” (Math 25:21,23). Tutamuona Mungu vile anavyojiona, ingawa hatutaweza kumaliza vilindi vya hali yake, vya upendo wake na vya uweza wake. Pia tutampenda anavyojipenda. Vilevile tutamuona Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo heri ya milele yenyewe, mbali ya furaha ya ziada tutakayokuwanayo kwa kuwaona na kuwapenda Bikira Maria na watakatifu wote, hasa tuliowafahamu duniani.

Tanbihi

  1. Marshall Fredericks (2003). "GCVM History and Mission". Greater Cleveland Veteran's Memorial, Inc. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-02-16. Iliwekwa mnamo 2009-01-14.
  2. "Oxford English Dictionary "Immortality"". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-05-31. Iliwekwa mnamo 2014-09-18.
  3. Joel Garreau (Oktoba 31, 2007). "The Invincible Man". The Washington Post: C01.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Marejeo

Viungo vya nje

Mtazamo wa kidini na wa kiroho

Katika fasihi

  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.