Agano la Kale
Agano la Kale ni mkusanyo wa vitabu vya sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo inayotumiwa na waumini wa Ukristo duniani kote. Pengine mkusanyo huu unagawanywa katika makundi kadiri ya mada au mtindo: sheria, historia, ushairi na unabii, ambayo ni tofauti kiasi na kawaida ya Tanakh ya Uyahudi wa leo.
Vitabu vyote vya Agano la Kale viliandikwa kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kwa mujibu wa wanahistoria wa Biblia, vitabu vya Agano la Kale viliandikwa kati ya karne ya 11 KK na karne ya 1 KK.
Orodha tofauti za vitabu vya Agano la Kale
Katika mapokeo ya Kikristo kuna orodha tofauti za vitabu vya Agano la Kale. Hasa kuna matoleo yenye vitabu 39 na kuna matoleo yenye vitabu 46.
- Waprotestanti wengi hukubali vitabu 39 ambavyo ni sawa na Tanakh ya Wayahudi.
- Wakatoliki hukubali vitabu 46 yaani hivyo 39 na 7 vingine (Deuterokanoni) ambavyo ni: Kitabu cha Yuditi, Kitabu cha Tobiti, Kitabu cha Yoshua bin Sira, Kitabu cha Hekima, Kitabu cha Wamakabayo I na Kitabu cha Wamakabayo II, halafu sehemu za nyongeza za vitabu vya Kitabu cha Danieli na Kitabu cha Esta.
- Baadhi ya Waorthodoksi wana vitabu vingine pia kama vile Esra 1 (Esra ya Kiebrania huhesabiwa kama Esra 2), 3 Wamakabayo na zaburi 151; kama nyongeza 4 Wamakabayo; Ufunuo wa Esra na hata vingine.
Biblia ya Kiebrania au Biblia ya Kigiriki?
Asili ya mahesabu haya mawili ni hasa desturi tofauti ndani ya Uyahudi wakati wa Yesu na karne mbili za kwanza BK. Kanuni ya Biblia ilikuwa haijafungwa wakati ule. Hivyo palikuwa na mikusanyo tofauti kati ya Wayahudi wenye lugha ya Kiebrania au ya Kiaramu kwa upande mmoja na Wayahudi waliotumia lugha ya Kigiriki kwa upande mwingine.
Wayahudi wenye lugha ya Kigiriki (waliokaa nje ya Palestina, hasa katika nchi mbalimbali za Dola la Roma na kuzidi idadi ya Wayahudi katika Palestina Israeli yenyewe) walitumia toleo la Kigiriki la Septuaginta. Wakristo wa kwanza walizoea toleo hilo hasa kwa sababu lugha ya mawasiliano kati ya Wakristo ilikuwa Kigiriki kama lugha ya kimataifa. Ndiyo sababu Agano Jipya lote liliandikwa kwa Kigiriki.
Upande wa Uyahudi uamuzi kuhusu vitabu vinavyofaa kuhesabiwa kuwa sehemu za Biblia ya Kiebrania lilifanywa kati ya miaka 80 - 135 BK]] ambapo wataalamu Wayahudi waliamua kukubali vitabu vile tu vilivyotunzwa kwa Kiebrania. Hivyo maandiko kadhaa zisizoandikwa kwa Kiebrania vilifungwa nje. Sababu mojawapo ya uamuzi wao ilikuwa kubishana na Wakristo waliovitumia.
Jumuia za Kiyahudi zilipokea uamuzi huo lakini Wakristo waliendelea kutumia Septuaginta, iliyotafsiriwa baadaye kwa Kilatini na lugha nyingine za mataifa na za makabila yaliyopokea imani ya Kikristo.
Hivyo Biblia ya Wakristo ulikuwa na vitabu vya Septuaginta hadi matengenezo ya Kanisa katika karne ya 16.
Martin Luther alianza kutafsiri Biblia upya kutoka lugha asilia akaona achague vitabu vyake, akinyofoa 7 vya Agano la Kale pamoja na vichache vya Agano Jipya kadiri alivyoviona kuwa na mafundisho sahihi kiimani. Hivyo upande wa Agano la Kale alilingana na Wayahudi na kutofautiana na jinsi ilivyokuwa kawaida katika Kanisa Katoliki ambalo katika Mtaguso wa Trento (karne ya 16) lilithibitisha matumizi ya vitabu 46 katika Agano la Kale.
Tangu Luther matoleo mengi ya Kiprotestanti huonyesha vitabu vya Agano la Kale kuwa 39. Mara nyingine vitabu 7 vya Deuterokanoni vinaongezwa baada ya Agano la Kale kama sehemu ya pekee vikiitwa "Apokrifa".
Vitabu vya Agano la Kale
Orodha hii inafuata kawaida ya Wakristo walio wengi. Umbo la majina ni ule wa tafsiri ya "Biblia - Habari Njema kwa Watu Wote". Vitabu saba vinafuatwa na alama ya DK ni vile ambavyo huhesabiwa kando na Waprotestanti wengi kama "Apokrifa" lakini hutazamiwa kama vitabu kamili vya Biblia (Deuterokanoni) katika mapokeo ya Kanisa Katoliki na ya Waorthodoksi wengi.
Vitabu vya Kihistoria
- 1. Vitabu vitano vya Torati vinavyoitwa pia "vitabu vya Musa":
- Mwanzo (Kitabu cha Kwanza cha Musa)
- Kutoka (Kitabu cha Pili cha Musa)
- Walawi (Kitabu cha Tatu cha Musa)
- Hesabu (Kitabu cha Nne cha Musa)
- Kumbukumbu la Sheria (Kumbukumbu la Torati; Kitabu cha Tano cha Musa)
- Mwanzo (Kitabu cha Kwanza cha Musa)
- 2. Vitabu vingine vya kihistoria
- Yoshua
- Waamuzi
- Ruthu (Kitabu cha Ruthi)
- Samueli I
- Samueli II
- Wafalme I
- Wafalme II
- Mambo ya Nyakati I
- Mambo ya Nyakati II
- Ezra
- Nehemia (Kitabu cha Pili cha Ezra)
- Tobiti DK
- Yudith DK
- Esta
- Wamakabayo I DK
- Wamakabayo II DK
- Yoshua
Vitabu vya Kishairi au vya hekima
- Yobu (Kitabu cha Ayubu)
- Zaburi
- Methali
- Mhubiri
- Hekima DK
- Yoshua bin Sira DK
- Maombolezo (Maombolezo ya Yeremia)
- Yobu (Kitabu cha Ayubu)
Vitabu vya manabii
Viungo vya nje
Makala hii kuhusu mambo ya Agano la Kale bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Agano la Kale kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.