Waraka kwa Wagalatia

ya tisa kitabu Agano Jipya, mchanganyiko sita sura ya
(Elekezwa kutoka Gal)

Barua kwa Wagalatia ni kati ya vitabu 27 vya Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo.

Uongofu wa Mtume Paulo kadiri ya Caravaggio.
Agano Jipya

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Mazingira hariri

Barua hiyo iliandikwa na Mtume Paulo akiwa Efeso.

Tofauti na zile kwa Wathesalonike, hii ni kali sana kwa kuwa Paulo aliiandika (mwaka 54 hivi) mara baada ya kusikia kwa mshangao na huzuni kwamba wanafunzi wake wa mkoa wa Galatia wanataka kupotoshwa na Wakristo wengine wanaosisitiza haja ya kushika Torati ili kupata wokovu.

Ili kumpinga Paulo na mafundisho yake kuhusu neema, wazushi hao walikanusha pia mamlaka yake kama mtume, eti, hajawahi kumuona Yesu, na anarahisisha masharti ya dini ili ajipatie wafuasi na heshima.

Basi, ilimbidi ajitetee na kusimulia baadhi ya matukio ya maisha yake yanayotusaidia kumfahamu zaidi na kutambua kwamba msimamo wake wa awali kama Farisayo haukumuelekeza hata kidogo kupuuzia Torati.

Ni tukio la ghafla la kutokewa na Mfufuka tu lililoweza kupindua mtazamo wake. Baada ya hapo, msimamo wake mpya ulikubaliwa na viongozi wa Kanisa mama la Yerusalemu waliotambua karama yake ya pekee kwa uongofu wa mataifa.

Akitetea uhuru wao kuhusu masharti ya Torati, Paulo hakukosa kueleza kwamba hauruhusu kufuata udhaifu wa kibinadamu (unaowakilishwa na mwili), bali ni kwa ajili ya kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu ambao ni wa juu kuliko Torati na hatimaye unazaa tunda lake bora.

Akiandika kwa hasira takatifu ili kuzuia Injili isibadilishwe wala msalaba usibatilishwe - kwa sababu wokovu ukipatikana kwa kushika Torati, Kristo amekufa bure - mara baada ya salamu akashambulia kwa nguvu wazushi na kuonyesha kwa madondoo ya Biblia kuwa haiwezekani kujipatia uadilifu kwa kujaribu kufuata sheria za Musa walivyotaka wao.

Kinyume chake alidai uadilifu wetu unatokana na imani kwa Yesu Kristo na msalaba wake.

Inavyojulikana, Wayunani walikuwa na hamu kubwa kuliko wengine ya kupata maarifa, halafu kubishana nao kwa ufasaha na kushinda.

Katika mazingira hayo, falsafa na dini zilikuwa mada kuu na kuingiliana na hadithi za ajabuajabu kuhusu miungu, malaika na wengineo.

Karibu barua zote za mitume zilikabili hatari hiyo, ambayo ikazidi kuwa kubwa na kuleta mafarakano katika Kanisa hasa katika karne II, ilipoitwa “Gnosis” (= ujuzi). Ndiyo sababu Paulo alijitahidi kuishinda mapema iwezekanavyo.

Ilimbidi kwanza ajitetee kuwa mtume halisi anayefundisha kulingana na mitume wengine, halafu aonyeshe tunavyookolewa kwa imani, si kwa kufuata Torati, hatimaye atoe mawaidha kuhusu uhuru wa Kikristo, kwamba unategemea kumfuata Roho Mtakatifu si tamaa za dunia (Gal 1:1-12; 2:15-3:14; 4:4-20; 5; 6:7-18).

Viungo vya nje hariri

Tafsiri ya Kiswahili hariri

  • [1] Agano Jipya kwa lugha ya Kiswahili.

Vingine hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya Agano Jipya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Waraka kwa Wagalatia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.