Ukahaba

(Elekezwa kutoka Kahaba)

Ukahaba (kutoka Kiarabu: قحبه qahabatun = malaya) ni tabia au tendo la kufanya ngono nje ya ndoa au uhusiano mwingine unaokubalika katika jamii, tena na watu mbalimbali na kwa malipo. Mtendaji anayepokea malipo huitwa kahaba, changudoa au malaya; washiriki wanaotoa malipo huitwa wateja.

Makahaba wa Toulouse-Lautrec DMA
Sheria kuhusu ukahaba duniani      Ukahaba unaruhusiwa, kuna utaratibu wa kisheria      Ukahaba unaruhusiwa, danguro ni marufuku, hakuna utaratibu wa kisheria      Ukahaba ni marufuku      hakuna habari juu ya nchi hizi

Kama ukahaba unaendeshwa katika nyumba maalumu mahali hapo panaitwa danguro.

Jinsi na namna ya ukahaba

hariri

Kimsingi kuna aina mbili za ukahaba.

  1. Malaya anajifanyia kazi na kuamua mwenyewe namna gani. Huyu atapatikana mara nyingi akitembea barabarani, kusubiri kwenye vilabu vya pombe au kwa kutangaza namba ya simu. Wanajitangaza pia kupitia intaneti (Whatsapp, Instagram, Twitter, Facebook na Telegram) na kukutana na wateja mahali mbalimbali.
  2. Malaya wanafanya kazi chini ya usimamizi wa mtu mwingine au watu wengine. Hali yao inaweza kufanana na aina ya ajira wakilipwa kwa kila tendo la ngono kutoka msimamizi anayepokea fedha; au wanatakiwa kutoa malipo kwake kutokana na mapato yao. Kundi hili linapatikana mara nyingi katika danguro, lakini wako pia barabarani katika maeneo maalumu wanapotazamiwa na kuwadi. Katika kundi hili kuna hasa aina ya utumwa wa kingono ambapo mabinti na wanawake wanalazimishwa kujiuza kwa wateja. Mwaka 2009 Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba 79% za watu wanaouzwa ni kwa ajili ya biashara ya ukahaba ambayo imekuwa hivyo biashara ya watumwa kubwa kuliko zote za historia ya binadamu. Kila mwaka watu 800,000 hivi wanavushwa mipaka ya nchi zao kwa ajili hiyo, wakiwemo hasa wanawake, wale wenye umri chini ya miaka 18 wakiwa hadi 50%.

Hali ya kisheria

hariri

Misimamo ya jamii na sheria inatofautiana kati ya nchi na nchi. Hata kama ukahaba unapatikana kote duniani, umepigwa marufuku katika nchi nyingi. Lakini mahali pengi penye sheria dhidi ya ukahaba polisi inafumba macho au kutofuatilia biashara hii.

Kati ya misimamo kuhusu ukahaba iko ifuatayo:

  • Ukahaba hutazamwa kama jinai. Watendaji wanatishiwa kwa adhabu za kisheria kuanzia faini, jela hadi adhabu ya mauti (kama Saudia). Mara nyingi ni hasa makahaba wanaolengwa kwa adhabu hizi, lakini mahali pengine pia wateja. Hata hivyo katika nchi nyingi zenye sheria dhidi ya ukahaba polisi inafumba macho au kutofuatilia biashara hii.
  • Ukahaba hutazamwa kama ubaya unaovunja heshima hasa ya wanawake, yaani malaya. Malaya huangaliwa kama waathirika wanaostahili kusaidiwa, kwa hiyo hawana adhabu. Lakini wote wengine wanaofaidika na ukahaba wanalengwa kwa adhabu: wenye danguro, makuwadi, washiriki katika biashara ya makahaba hadi wateja wenyewe katika nchi kadhaa (mfano: Uswidi)
  • Ukahaba hutazamwa kama ubaya usioshindikana, kwa hiyo serikali imetunga sheria na taratibu kwa lengo la kupanga upatikanaji wa ukahaba. Danguro zinapaswa kuandikishwa serikalini, zinatembelewa na idara ya afya ya umma; malaya wanaruhusiwa katika mitaa maalumu ya miji pekee, wanapaswa kupimwa na kupatiwa matibabu mara kwa mara. Vijiji na miji midogo vinaweza kuzuia ukahaba katika maeneo yao.
  • Ukahaba hautazamwi tena kama jinai wala kosa bali kama chaguo la watu wazima. Kwa hiyo ukahaba huangaliwa kama namna ya biashara kama biashara nyingine; malaya huitwa "wafanyakazi wa ngono", wanatakiwa kulipa kodi na wanalindwa na sheria za kazi (mifano Uholanzi na Ujerumani).
  • Utaratibu maalumu uko katika Uajemi ambako kuna "mutaa" au ndoa ya muda kulingana na mafundisho ya Kishia. Chini ya utaratibu wa mutaa kuna uhusiano unaolingana na ndoa au pia urafiki katika nchi nyingine; lakini mutaa inaruhusu pia mikataba ya muda mfupi na inadai mapatano juu ya malipo upande wa mwanamume. Kwa hiyo inapatikana pia kama njia ya ukahaba ambao vinginevyo ni marufuku nchini Uajemi.

Afya ya jamii

hariri

Si siri kwamba ukahaba unachangia sana uenezi wa maradhi ya zinaa, ukiwemo UKIMWI.

Tanbihi

hariri
 
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:
  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ukahaba kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.