Kitabu cha Zaburi ni kimojawapo kati ya vitabu vya Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na kwa hiyo pia vya Agano la Kale ambalo ni sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.

Kitabu cha Zaburi kwa Kiebrania.
"Mfalme Daudi aandikisha zaburi"; Funiko la Kitabu cha Zaburi kutoka karne ya 11; kazi ya uchongaji wa meno ya ndovu.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Yaliyomo

hariri

Kina sura 150; kila sura ni zaburi moja. Zaburi ni aina ya sala iliyotungwa kama shairi au wimbo. Zaburi zinafundisha jinsi binadamu awezavyo kuzungumza na Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo kitabu cha Zaburi kinatumiwa na Wayahudi na Wakristo kama kitabu cha sala.

Mada za zaburi hasa ni sifa za Mungu, shukrani, maombolezo, huzuni na toba, furaha na imani, elimu ya kidini, na ombi la ushindi dhidi ya maadui wasiomcha Mungu.

Zaburi nyingi zimetungwa kama shairi la Kiebrania; mara nyingi fungu moja linarudia wazo la fungu lililopita, k.m. katika Zaburi 22, mistari 1-2:

Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Mbona uko mbali sana kunisaidia, mbali na maneno ya kilio changu?
Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu;
napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati.

Katika kitabu hicho zaburi kadhaa zimewekwa pamoja: kwa mfano, Zaburi za Wakorahi (baadhi zikiwa 42—49), za Asafu (73—83), za kumsifu Mungu aliye Mfalme au Mtawala wa wote (93—99) au Zaburi za kuhiji (120—134).

Baadaye Zaburi ziligawanywa katika vitabu vitano: 1—41; 42—72; 73—89; 90—106; 107—150. Kila kimojawapo kinamsifu Mungu katika mstari wake wa mwisho: 41:13; 72:19; 89:52; 106:48; na Zaburi yote ya 150. Inawezekana kuwa mgawanyo huo ulifanyika ili kuiga mgawanyo wa vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, yaani Torati.

Baadhi ya Zaburi zinazojulikana sana ni:

Zaburi tatu fupifupi

hariri

Wewe, Mungu, Bwana wetu,
jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni.
Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao
umeiweka misingi ya nguvu;
kwa sababu yao wanaoshindana nawe;
uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota ulizoziratibisha;
mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
na binadamu hata umwangalie?
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
umemvika taji ya utukufu na heshima;
umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
Kondoo, na ng’ombe wote pia;
naam, na wanyama wa kondeni;
ndege wa angani, na samaki wa baharini;
na kila kipitiacho njia za baharini.
Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

Zab 123

hariri

Nimekuinulia macho yangu, wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi kwa mkono wa bwana zao;
kama macho ya mjakazi kwa mkono wa bibi yake;
hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu,
hata atakapoturehemu.
Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
kwa maana tumeshiba dharau.
Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
na dharau ya wenye kiburi.

Zab 130

hariri

Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia;
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize sauti ya dua zangu.
Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha, ili Wewe uogopwe.
Nimemngoja Bwana, roho yangu imemngoja,
na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
naam, walinzi waingojavyo asubuhi.
Ee Israeli, umtarajie Bwana;
maana kwa Bwana kuna fadhili,
na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atawakomboa Israeli na maovu yake yote.

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Zaburi kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.