Hesabu (Biblia)
Kitabu cha Hesabu ni cha nne katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na vilevile katika Agano la Kale ambalo ni sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Majina
haririKwa asili kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania (neno lake la kwanza linatumika kama jina la kitabu katika lugha hiyo: במדבר bemidbàr, yaani "jangwani").
Jina la Kiswahili linatokana na lile la Kigiriki Αριθμοί, aritmòi, na la Kilatini Numeri, maana yake “hesabu” kwa vile kinaleta hesabu mbalimbali.
Wengine wanakiita Kitabu cha Nne cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa Mose ndiye mwandishi wa kitabu hicho.
Yaliyomo
haririKitabu cha Hesabu kina sura thelathini na sita, na kinasimulia hasa safari za Waisraeli kutoka Mlima Sinai hadi nchi ya Israeli. Pia, kinataja maagizo mbalimbali ya Mungu na hesabu mbili za Wanaisraeli.
Kadiri ya kitabu hicho, idadi yao wakati wa kutoka Misri ilikuwa ifuatavyo: wanaume wa kuweza kwenda vitani walikuwa 603,500 (mbali na Walawi waliohesabiwa peke yao: wanaume 22,000 wakiwa pamoja na watoto wa kiume); ukiongeza wanawake na watoto mpaka umri wa miaka ishirini, basi jumla yao iliweza kufikia watu milioni tatu, ingawa si lazima kuamini idadi hiyo ni sahihi (katika makala za kale pengine namba hizo hazilingani kwa kuwa ilikuwa rahisi kukosea wakati wa kunakili).
Uzito wa kazi ya kuwaongoza watu wengi hivyo wanaonung’unika kila mara ulimchosha Musa hata akamuomba Mungu tena ampunguzie mzigo au amuue kabisa (Hes 11:1-30). Musa alieleza shida yake kama rafiki kwa mwenzake, kwa unyofu uleule wa watu wengine wa Mungu katika Biblia. Mungu akamkubalia akawashirikisha watu sabini roho yake kwa ajili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. [1]
Katika nafasi hiyo Musa alimueleza Yoshua kwamba hawaonei kijicho kwa kupewa karama, tena angependa kama Waisraeli wote wangekuwa manabii. [2]
Kinyume chake Hes 12 inasimulia kijicho kilivyowafanya dada na kaka wa Musa wamseme wakijidai nao pia ni manabii. Lakini Mungu akawaeleza kuna namna mbalimbali za unabii, na Musa ni wa pekee. Kisha akatoa adhabu ambayo ikaondolewa kwa maombezi ya Musa tu: ndiyo sababu anasifiwa kwa upole wake. [3]
Waisraeli walipofikia mipakani mwa nchi takatifu walituma wapelelezi ili waivamie kwa mafanikio, nao waliporudi walisimulia uzuri wake, lakini pia walitisha kwa kuzidisha habari za wananchi na miji yao (Hes 13). Hapo Waisraeli wakaanza kunung’unika usiku kucha (Hes 14) wakapanga kuwaua kwa mawe Kalebu na Yoshua waliotaka kuivamia nchi bila ya hofu kwa jina la Bwana. Lakini Mungu akaonyesha utukufu wake na kutisha ataleta tauni ili kuwaangamiza wote kwa ukaidi wao. Kwa maombezi ya Musa, akakubali kuwahurumia lakini akaamua warudi jangwani na kuzungukazunguka huko mpaka wafe wote; ila watoto wao pamoja na Kalebu na Yoshua ndio watakaoingia nchi takatifu kuimiliki. Maana ya kiroho ni kwamba hatutakiwi kuzitia shaka ahadi za Mungu; hata zikionekana ngumu kupatikana, ni lazima tuwe na moyo mkuu na imani hata tukabili vipingamizi vyovyote.
Kinyume chake, Waisraeli walipoamua kuivamia nchi kwa kusikitikia adhabu waliyopewa wakashindwa kabisa, maana ni lazima tumtii Mungu kwa wakati wake. Pia kughairi kutokana na matatizo kunaweza kukatusukuma tutende namna ambayo haimpendezi tena; ni lazima tuchukue majukumu ya matendo yetu na kukubali adhabu au matatizo tuliyojitakia:majuto hayo yanafaa kwa kuonyesha utiifu kwa Mungu (Zab 119:71).
Manung’uniko ya Waisraeli katika safari yao jangwani yakawaletea adhabu nyingine, mojawapo ile ya kugongwa na nyoka wengi wenye sumu kali. Lakini walipoomba msamaha, Mungu akamuagiza Musa atengeneze nyoka wa shaba na kumuinua juu ya mti ili mtu aliyeumwa akimtazama tu apate kupona (Hes 21:4-9). [4]
Mazingira ya kitabu
haririKitabu cha Hesabu kinapoanza, watu wa Israeli walikuwa wameishi karibu na Mlima Sinai kwa muda wa karibu mwaka mmoja. Katika muda huo Mungu aliwaandaa kwa maisha yaliyowakabili, akiwafundisha aina ya dini, kanuni za uadilifu na utamaduni alivyotaka wawe navyo kama watu wake wa agano. (Kwa habari zaidi taz. maelezo katika utangulizi wa kitabu cha Walawi.) Wakati huo muda umewadia kwa Waisraeli waondoke katika Mlima Sinai na wasafiri kuelekea nchi ya ahadi, yaani Kanaani. Kitabu cha Hesabu kinasimulia habari za maandalio kwa safari hiyo, kinaeleza kwa kifupi maagizo mengine yaliyobidi kutimizwa, pia kinasimulia matukio mengine ya maana sana yaliyotokea njiani.
Taifa jangwani
haririKatika matukio mawili kati ya muda wa Waisraeli kutoka Misri na kuingia kwao Kanaani, Musa alihesabu watu kwa sensa maalumu ya kitaifa. Sensa hizo mbili zimeandikwa katika kitabu cha Hesabu, na kutokana na sensa hizo kitabu kilipata jina lake.
Sensa ya kwanza ya mwanzo wa kitabu iliwasaidia watu kuandaa jeshi kwa kuteka nchi ya Kanaani. Ingawa safari ya kwenda Kanaani ingeweza kuchukua majuma machache tu, kwa kweli ilichukua karibu miaka 40. Sababu yake ilikuwa kwamba, watu walimwasi Mungu wakikataa kumtegemea kuwa angewapa ushindi. Matokeo yake, Mungu aliwaacha jangwani mpaka kizazi kile kilipokufa na kizazi kipya kilipokua wawe watu wazima. Sensa ya pili iliandikwa karibu na mwisho wa kitabu, hivyo ilikuwa karibu miaka 40 baada ya ile ya kwanza, na makusudi yake yalikuwa kuwapanga watu wa kizazi kipya ili wateke nchi ya Kanaani.
Sensa hizo mbili zilichukua sehemu ndogo tu ya kitabu kizima, kwa hiyo jina la Kiswahili la kitabu hiki 'Hesabu' halionyeshi hasa yaliyomo katika kitabu. Jina la Kiebrania, 'Jangwani', linafaa zaidi, kwa sababu kitabu kinasimulia habari za safari yao kutoka Mlima Sinai hadi mpakani mwa nchi ya Kanaani, na sehemu nyingi zaidi ya safari hiyo ilikuwa jangwani. Habari nyingi zilizosimuliwa katika kitabu cha Hesabu zinahusu safari hiyo. Kitabu kinatoa habari chache sana kuhusu miaka yote 40, Waisraeli waliposafiri na kutangatanga jangwani (Hes 32:13).
Muhtasari
hariri1:1-10:10 Maandalizi ya safari
10:11-14:45 Kutoka Sinai hadi Kadeshi
15:1-19:22 Mafundisho ya Kadeshi
20:1-22:1 Kutoka Kadeshi hadi jangwa la Moabu
22:2-32:42 Matukio katika nchi tambarare ya Moabu
33:1-36:13 Maandalizi ya kuingia Kanaani
Marejeo
haririVitabu vya ufafanuzi
hariri- Ashley, Timothy R (1993). The Book of Numbers. Eerdmans.
- Fretheim, Terence E (1998). "Numbers". Katika John Barton (mhr.). Oxford Bible Commentary. Oxford University Press.
- Knierim, Rolf P; Coats, George W (2005). Numbers. Eerdmans.
- Olson, Dennis T (1996). Numbers. Westminster John Knox Press.
- Stubbs, David L (2009). Numbers. Brazos Press.
Vingine
hariri- Bandstra, Barry L (2004). Reading the Old Testament: an introduction to the Hebrew Bible. Wadsworth.
- Blenkinsopp, Joseph (2004). Treasures old and new: essays in the theology of the Pentateuch. Eerdmans.
- Brueggemann, Walter (2002). Reverberations of faith: a theological handbook of Old Testament themes. Westminster John Knox.
- Campbell, Antony F; O'Brien, Mark A (1993). Sources of the Pentateuch: texts, introductions, annotations. Fortress Press.
- Clines, David A (1997). The theme of the Pentateuch. Sheffield Academic Press.
- Dawes, Gregory W (2005). Introduction to the Bible. Liturgical Press.
- Gilbert, Christopher (2009). A Complete Introduction to the Bible. Paulist Press.
- Knierim, Rolf P (1995). The task of Old Testament theology: substance, method, and cases. Eerdmans.
- Kugler, Robert; Hartin, Patrick (2009). An Introduction to the Bible. Eerdmans.
- McDermott, John J (2002). Reading the Pentateuch: a historical introduction. Pauline Press.
- Van Seters, John (2004). The Pentateuch: a social-science commentary. Continuum International Publishing Group.
- Van Seters, John (1998). "The Pentateuch". Katika Steven L. McKenzie, Matt Patrick Graham (mhr.). The Hebrew Bible today: an introduction to critical issues. Westminster John Knox Press.
- Ska, Jean-Louis (2006). Introduction to reading the Pentateuch. Eisenbrauns.
Viungo vya nje
hariri- Toleo katika lugha asili:
- במדבר Bamidbar - Numbers Ilihifadhiwa 14 Mei 2012 kwenye Wayback Machine. (Hebrew – English at Mechon-Mamre.org)
- Tafsiri za Kiyahudi:
- Numbers at Mechon-Mamre Ilihifadhiwa 6 Juni 2012 kwenye Wayback Machine. (Jewish Publication Society translation)
- Numbers (The Living Torah) Ilihifadhiwa 1 Agosti 2011 kwenye Wayback Machine. Rabbi Aryeh Kaplan's translation and commentary at Ort.org
- Bamidbar - Numbers (Judaica Press) translation [with Rashi's commentary] at Chabad.org
- Tafsiri za Kikristo:
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
- ↑ Huo pia ni mfano wa Agano Jipya, ambapo askofu hawezi kuchunga waamini peke yake, bali anahitaji msaada wa viongozi wa daraja za chini, yaani makasisi na mashemasi (Mdo 6:1-6).
- ↑ Hamu hiyo ikatimia siku ya Pentekoste: katika Kanisa wote wanapewa Roho Mtakatifu na kuwa manabii, hata wanawake na watoto (Mdo 2:16-18).
- ↑ Kijicho kitasumbua daima taifa la Mungu, hata katika Agano Jipya (1Kor 12:1-31; 14:37-38).
- ↑ Ufafanuzi wa tukio hilo ulitolewa na Yesu mwenyewe: ndiye aliyeinuliwa juu ya mti wa msalaba ili watakaomtazama kwa imani wapate kuishi (Yoh 3:14-15).