Deuterokanoni

Vitabu vya deuterokanoni (kutoka Kigiriki "deuteros" = ya pili na "kanon" = orodha) ni maandiko ya Agano la Kale yanayotazamwa na Wakatoliki, na baadhi ya Waorthodoksi na ya Makanisa ya Kale ya Mashariki kama sehemu kamili ya Biblia.

Wayahudi na Waprotestanti wengi huviita apokrifa na kuvitazama kama vitabu vinavyostahili kuheshimiwa lakini si sawa na Biblia yenyewe.

Vitabu vya deuterokanoni vya Agano la KaleEdit

Katika Biblia zinazotolewa na Kanisa Katoliki ni vitabu saba vifuatavyo (pamoja na sehemu za vitabu vya Kitabu cha Esta na Kitabu cha Danieli):

Baadhi ya Waorthodoksi wana vitabu vingine pia kama vile Ezra 1 (Ezra ya Kiebrania huhesabiwa kama Ezra 2), Kitabu cha tatu cha Wamakabayo na Zaburi ya 151; kama nyongeza Kitabu cha 4 cha Wamakabayo; Ufunuo wa Ezra na hata vingine.

Vitabu hivyo vyote ama havikuandikwa (Bar, 2 Mak, Hek) ama havikupatikana mapema kwa lugha ya Kiebrania (asili kwa Sir, Judt, 1Mak) wala ya Kiaramu (asili kwa Tob), bali kwa Kigiriki tu.

Historia ya orodha ya vitabu vya deuterokanoniEdit

Hadi karne ya kwanza KK orodha ya vitabu vya Biblia ya Kiebrania ilikuwa haijaamuliwa, ingawa ilikuwa wazi ya kwamba vitabu vya Torati ni maandiko matakatifu kamili; katika suala la vitabu vingine Wayahudi bado walitofautiana, k.mf. Masadukayo walikataa hata vile vya Manabii.

Sehemu kubwa ya Wayahudi nje ya Israeli na Mesopotamia walitumia toleo la Kigiriki lililoitwa Septuaginta ambalo lilitafsiriwa na wataalamu Wayahudi huko Misri katika karne ya pili na tatu KK.

Wakati ule Septuaginta ilikuwa ndiyo Biblia ya Wakristo wa kwanza (ambao wengi wao hawakujua Kiebrania) kabla ya kukamilika kwa orodha ya vitabu vya Agano Jipya.

Baada ya maangamizi ya Hekalu la Yerusalemu (70) na hasa katika karne ya 2 wataalamu Wayahudi waliamua kutovikubali kama sehemu za Tanakh vitabu visivyopatikana kwa lugha ya Kiebrania wakati walipopatana juu ya mapokeo yao ili kujiimarisha dhidi ya Ukristo na ustaarabu wa kigeni.

Wakristo hawakufuata maazimio hayo ya Wayahudi, hivyo mwishoni mwa karne ya pili Wakristo katika magharibi ya Mediteranea walianza kutafsiri Septuaginta katika Kilatini kilichokuwa lugha kuu kwao.

Matamko ya Kanisa KatolikiEdit

Vitabu vya Deuterokanoni vilihesabiwa rasmi kuwa sehemu ya Biblia hasa kuanzia Hati ya Damasi au De explanatione fidei, iliyotolewa na Papa Damasus I mwaka 382 (kwa Kilatini).

Tafsiri ya Kilatini ya Hieronimo kilichoitwa Vulgata ilipata kuwa toleo muhimu katika Kanisa Katoliki. Hieronimo mwenyewe alipotafsiri Biblia upya katika Kilatini alisema vitabu vya Septuaginta kama Hekima, Yoshua bin Sira, Yudith na Tobiti havistahili kuwemo katika Biblia lakini alivitafsiri ndani ya Vulgata kufuatana na maelekezo wa Papa Damaso I aliyemuagiza kazi.

[1]

Orodha hiyo ya Papa Damaso I ilipata nguvu Afrika Kaskazini kutokana na Agostino wa Hippo kuifanya ipitishwe na Mtaguso wa Hippo (393), Mtaguso wa Tatu wa Kartago (397) na Mtaguso wa Nne wa Kartago (419).

Wakati huohuo Papa Inosenti I aliituma kwa askofu Exuperius wa Toulouse (405).

Baadaye Mtaguso wa Firenze (1442) na Mtaguso wa Trento (1546) ilivitambua rasmi kuwa sehemu za Biblia kamili kwa Kanisa Katoliki.

Misimamo ya WaprotestantiEdit

Wakati wa Matengenezo ya kiprotestanti katika karne ya 16 Martin Luther na wengineo walishika msimamo mkali kuhusu kanuni ya Biblia akafuata azimio la Wayahudi na shauri la Hieronimo kuhusu vitabu hivyo.

Pamoja na hivyo waliweka pembeni hata baadhi ya vitabu vya Agano Jipya ambavyo zamani ulitokea wasiwasi juu yake na kwa sababu hiyo pengine vinaitwa pia deuterokanoni:

Baada ya kifo cha Martin Luther, Waprotestanti walikubali tena vitabu vyote vya Agano Jipya na kurudisha umoja katika jambo hilo la msingi kwa Ukristo.

MarejeoEdit

  1. "Hic prologus Scripturarum quasi galeatum principium omnibus libris, quos de hebraeo vertimus in latinum, convenire potest, ut scire valeamus, quicquid extra hos est, inter apocrifa seponendum. Igitur Sapientia, quae vulgo Salomonis inscribitur, et Iesu filii Sirach liber et Iudith et Tobias et Pastor non sunt canone. Macchabeorum primum librum hebraicum repperi, secundus graecus est, quod et ex ipsa φράσιν probari potest." (Hieronimo katika "Prologus Galeatus" au utangulizi kwa vitabu vya Samueli na Wafalme katika Vulgata)
Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.