Kitabu cha Nehemia

Kitabu cha Nehemia ni kimoja kati ya vitabu vya Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na hivyo pia vya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.

Gustave Doré, Nehemia Akikagua Magofu ya Ngome ya Yerusalemu, 1866.

Mazingira ya kitabu

hariri

Kinasimulia maendeleo na magumu ya Wayahudi katika kujenga upya mji wa Yerusalemu baada ya kurudi toka uhamisho wa Babeli. Kadiri ya wataalamu kadhaa habari hizo zinahusu miaka 12, tangu 445 KK hadi 433 KK, lakini wengine wana mtazamo tofauti.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Kwa habari zaidi juu ya mazingira ya kitabu cha Nehemia tazama maelezo ya mazingira ya kitabu cha Ezra.

Habari zenyewe

hariri

Nehemia kurudi Yerusalemu na kujenga upya kuta za Yerusalemu (1:1-7:73)

hariri

Nehemia kurudi (1:1-2:10)

hariri

Labda miaka 13 ilikuwa imepita tangu mfalme Artashasta (Artaxerxes I) alipomtuma Ezra Yerusalemu ili arekebishe hali ya Israeli (Ezra 7:7; Neh 2:1). Mwanzoni Ezra alikuwa na mafanikio, lakini Wayahudi walipojaribu kuimarisha Yerusalemu kwa kujenga kuta kandokando yake, maadui wao waliwashtaki kuwa wanaandaa maasi dhidi ya Uajemi. Walipopeleka habari hizo kwa Artashasta, yeye alitoa amri ya kusimamisha kazi hiyo mara moja (Ezra 4:7-23).

Labda wakati huo huko Uajemi Nehemia, aliyekuwa afisa wa Kiyahudi katika ikulu ya mfalme, alipandishwa cheo kuwa mnyweshaji mkuu wa mfalme (yaani mkuu wa vinywaji; Neh 1:11). Wayahudi waliposikia kwamba mmojawao anaweza kusema na mfalme, walifika Uajemi ili wamwone. Walimweleza habari za shida kubwa ambazo maadui wa Wayahudi walisababisha huko Yerusalemu kwa kutekeleza amri ya mfalme (1:1-3; Ezra 4:23). Amri ile ilimruhusu mfalme kubadilisha uamuzi wake baada ya muda akipenda kufanya hivyo (Ezra 4:21), na bila ya shaka wajumbe wa Kiyahudi kutoka Yerusalemu walitegemea kwamba Nehemia ataweza kumshawishi mfalme awasaidie tena.

Lakini Nehemia hakuwa mtu wa kutafuta nafasi nzuri tu. Alikuwa mtu wa Mungu na mtu wa maombi. Alijua kwamba matatizo ambayo yeye na watu wake waliyapata yalikuwa matokeo ya dhambi zao, na kwa moyo wa unyenyekevu na kukiri dhambi, aliweka mambo yote mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba msaada wake (4-11).

Kwa muda wa miezi minne Nehemia aliomba kuhusu mambo hayo. Kwa hiyo alikuwa tayari kumweleza mfalme shida zake, nafasi ilipotokea ghafla. Matokeo yake ni kwamba, aliruhusiwa kurudi Yerusalemu ili atekeleze miradi ya ujenzi aliyokusudia. Pia alipewa vifaa vilivyohitajika (2:1-8; labda ulikuwa wakati huo alipowekwa kuwa liwali wa Yerusalemu, taz.5:14).

Nehemia alipokwenda Yerusalemu, hali na mazingira yalikuwa tofauti na wakati wa safari ya Ezra, naye aliona vizuri kupokea msaada wa mfalme, yaani kusindikizwa na kundi la askari (9; taz. Ezra 8:21-23). Maafisa wengine waliokuwa wametawala eneo la Yerusalemu hapo awali, walikasirika na kugeuka kuwa maadui wakali walipogundua kwamba eneo hilo liliwekwa chini ya liwali Nehemia. Licha ya kuwa Myahudi, alikuwa na mamlaka kutoka kwa mfalme wa Uajemi, hivyo hawakuweza kumwingilia tena (10).

Mpango wa kazi uliofuatwa (2:11-3:32)

hariri

Kujenga upya kuta kubwa zilizobomolewa kulikuwa kazi ngumu sana, tena kubwa mno, hata wengine walisema haiwezekani. Kwa hiyo, kabla ya kutangaza madhumuni yake, Nehemia alichunguza mambo yote kwa siri, ili ajue vizuri kazi iliyotakiwa na vifaa vilivyohitajika (11-16). Ujuzi huo ambao Nehemia alijipatia, pamoja na maelezo yake ya jinsi Mungu alivyoongoza mambo yote mpaka alipotumwa Yerusalemu, yaliwaaminisha watu kwamba wakati umewadia wa kuanza kujenga ngome, wasiogope upinzani ambao utaendelea kuwepo (17-20).

Kazi ilipangwa vizuri. Vikundi mbalimbali vya watu vilipangwa kila mahali bega kwa bega kuzunguka mji wote, hata kuta zote ziiweza kujengwa wakati mmoja. Orodha ya wafanyakazi inaonyesha kwamba Wayahudi kutoka mbali na karibu walikuja kusaidia. Si waashi tu, bali pia makuhani, mafundi wa dhahabu, mafundi wa manukato, maafisa wa serikali, wafanyabiashara na hata wanawake walisaidia kazi hiyo (3:1-16). Walawi walijenga karibu na nyumba ya kuhani mkuu (17-21). Makuhani na watu wengine walioishi Yerusalemu, kwa kawaida walipangiwa sehemu za karibu na nyumba zao, na watu waliotoka mbali walijenga sehemu zilizobaki (22-32).

Upinzani wa mwanzo (4:1-23)

hariri

Wayahudi walikuwa na kibali cha mfalme wa Uajemi kwa mradi wa kujenga kuta, kwa hiyo wapinzani wao ambao pia walikuwa chini ya mfalme huyo, waliogopa kuwashambulia hadharani. Hata hivyo waliwadhihaki na kufanya mzaha juu ya kazi yao, wakitumaini kwamba wataweza kuwachosha na kuwaachisha kazi ya ujenzi (4:1-5).

Lakini Wayahudi hawakukatishwa tamaa haraka wakaendelea na kazi yao (6). Kwa hiyo maadui walikusudia kuleta machafuko na kuvuruga akili za Wayahudi kwa kuleta mashambulio ya siri sehemu mbalimbali mjini. Wayahudi waliposikia makusudi hayo walizidisha maombi na kuongeza ulinzi wao (7-9). Wale walioishi vijijini walimletea Nehemia habari kuhusu shughuli za maadui (10-12), lakini Nehemia hakuogopa hatari. Aliwapa wafanyakazi silaha na kuwagawa katika makundi mawili. Wengine walipofanya kazi wenzao walilinda. Maarifa ya kivita yalifikiriwa ili kujihami kama maadui watashambulia ghafla (13-21). Watu wa nchini waliofanya kazi Yerusalemu waliombwa kulala mjini bila ya kurudi nyumbani, kwa kusudi la kuongeza ulinzi wa usiku (22-23).

Uchoyo wa matajiri (5:1-19)

hariri

Tatizo lingine lililomkabili Nehemia lilikuwa hali ya manung'uniko yaliyoongezeka polepole na kwa muda mrefu baina ya matajiri na maskini. Watu waliokuwa na shida ya fedha walikopa kwa matajiri ili waweze kununua chakula na kulipa kodi zao kwa serikali ya Uajemi. Matajiri wakaona hali hiyo kuwa ni nafasi ya kupata faida kwa kuwadai watu riba kubwa. Kisha maskini waliposhindwa kulipa, matajiri walichukua mashamba yao kuwa malipo ya deni, au wakachukua hata watoto wao na kuwafanya watumwa. Shida hiyo ilizidi katika mwaka wa njaa na wakati wa kazi ya kujenga kuta, kwa sababu wafanyakazi hawakuweza kujipatia mishahara ya kawaida. Maskini hawakuona njia yoyote ya kuondokana na hali hiyo, wakamsihi Nehemia awasaidie (5:1-5).

Nehemia alijua uchoyo na hila za matajiri, kwa sababu siku moja aliwaona wakiuza Wayahudi wawe watumwa wa wageni, nao walijua kwamba ilikuwa siasa ya Nehemia kuwanunua watumwa wale tena na kuwapa uhuru (6-8). Kwa hiyo aliamuru kwamba vitu au watu waliochukuliwa kuwa malipo ya madeni warudishwe na kupewa uhuru, na riba juu ya mikopo iondolewe kabisa (9-13).

Muda wote wa miaka 12 ya uliwali wake, Nehemia aliwapa watu kielelezo kizuri ili wakifuate. Yeye hakudai kitu chochote alichostahili kufuatana na cheo chake, asije akawatwisha watu mzigo mkubwa zaidi. Aliwalisha wageni na wafanyakazi wake hata kutoka mfukoni mwake mwenyewe (14-19).

Kumalizika kwa kuta (6:1-7:73)

hariri

Maadui walipoona kuta zikikaribia kumalizika, waliona njia ya pekee ya kuzuia kazi hiyo ni kumwondoa Nehemia mwenyewe. Walijaribu kumwita katika vijiji vya mbali ili wakamwue huko, lakini Nehemia alitambua hila yao (6:1-4). Kisha wakaeneza fununu kwa njia ya barua wazi iliyosema kwamba Nehemia alipanga maasi dhidi ya Uajemi, lakini kazi yao ikawa bure (5-9).

Maadui wakafikiri maarifa mengine tena. Walijaribu kumsababisha Nehemia afanye mambo ambayo yataharibu sifa yake ya kuwa mtu asiyeogopa wapinzani naye avunje heshima ya hekalu. Mara nyingine tena wakashindwa (10-14). Hata wapelelezi na wasaliti ambao maadui walikuwa wamewaweka mjini Yerusalemu hawakuweza kumzuia Nehemia asimalize kazi yake ya kujenga ukuta (15-19).

Wakati huo Yerusalemu ulizungukwa na kuta imara ulioweza kulinda mji. Hata hivyo, Nehemia alitaka kuongeza usalama. Mji ulikuwa haujapata wenyeji wengi, kwa hiyo tahadhari ilitakiwa. Ili kuzuia mashambulio ya ghafla ya alfajiri, Nehemia aliagiza milango ya mji isifunguliwe mpaka watu wote wawe macho na katika shughuli zao za kawaida za mchana. Pia aliweka ulinzi wa ngome yote uliopangwa kwa maarifa, ili watu wa kila nyumba walinde karibu na eneo lao (7:1-4).

Kisha Nehemia akaandika orodha kubwa ya watu wote walioishi Yerusalemu. Orodha hiyo ililinganishwa na ile ya kundi la kwanza la watu waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na Zerubabeli karibu miaka 100 iliyopita (5-73; taz. Ezra 2:1-70, ambapo orodha hiyo imeandikwa).

Marekebisho ya Nehemia (8:1-10:39)

hariri

Masomo ya kwanza ya sheria (8:1-18)

hariri

Kuta zilimalizika siku ya 25 ya mwezi wa sita (yaani muda wa ujenzi ulikuwa siku 52, taz. 6:15). Sikukuu ya Israeli ya katikati ya mwaka iliadhimishwa katika mwezi wa saba (Law 23:24,27,34), na hiyo ilikuwa nafasi nzuri ya kuwakutanisha watu wote ili kusherehekea pia kumalizika kwa ujenzi wa kuta (taz. 7:73; 8:1). (Wakati uleule wa mwaka ulikuwa umechaguliwa kwa kuweka wakfu madhabahu iliyojengwa upya zaidi ya miaka 90 ya nyuma; taz. Ezra 3:1-6).

Kufuatana na maombi ya watu, Ezra akisaidiwa na baadhi ya Walawi, alisoma Torati na kuieleza kwa watu waliokutanika. Inaonekana kwamba sheria hiyo ilikuwa haijasomwa kwa muda mrefu sana, kwa hiyo watu walisikiliza kwa uangalifu sana (8:1-8). Walipogundua jinsi maisha yao yalivyokuwa mbali na sheria hiyo, walijaa huzuni hata Nehemia aliogopa kwamba mambo aliyoyakusudia kuwa sikukuu ya furaha na karamu kubwa yatageuka kuwa wakati wa huzuni na maombolezo (9-12).

Siku ya pili yake viongozi wa Israeli walirudi tena ili wasikilize zaidi ya sheria ya Mungu (13). Matokeo ya mambo hayo yalikuwa sherehe kubwa ya taifa zima iliyoitwa sikukuu ya Vibanda. Wakati wa sikukuu hiyo watu waliishi katika vibanda vya matawi ya miti na makuti, wakiwakumbuka mababu zao jinsi walivyoishi katika vibanda wakati wa safari yao ya jangwani walipotoka Misri (14-18; taz. Law 23:33-43).

Maungamo ya Waisraeli na kiapo chao cha kutii (9:1-10:39)

hariri

Siku mbili baada ya kumaliza sikukuu ya Vibanda (iliyokuwa tangu siku ya 15 hadi ya 22 ya mwezi ule, taz. 8:18; Law 23:34), watu walikutana tena kwa kusomewa sheria. Wakati huo baada ya kusomewa, ulifuata wakati wa kukiri dhambi na kumwabudu Mungu. Ibada hiyo iliongozwa na Walawi (9:1-5).

Ibada ilianza kwa kumtukuza Mungu mkuu aliye Mwumbaji, na kwa kumsifu kwa sababu ya kumchagua Ibrahimu na kufanya naye agano lake (6-8). Mungu siku zote alikuwa mwaminifu kwa watu wake wa Israeli, wakati wa shida zao huko Misri na hata katika safari kubwa ya jangwani (9-15). Hata walipomwasi, aliwasamehe na kuwaleta katika nchi ya ahadi yake (16-25). Wakaendelea kuasi, naye akaendelea kuwasamehe. Lakini waliendelea na ukaidi wao, hata mwisho, baada ya kushindwa na kunyanyaswa mara nyingi na maadui wao, walipelekwa kifungoni katika nchi za kigeni, kusudi Mungu aweze kuwanyenyekeza na kusababisha watubu (26-31). Ingawa wakati huo walikuwa wamerudi katika nchi yao, bado walikuwa chini ya utawala wa wageni. Walikubali kwamba mambo hayo yalikuwa adhabu ya haki kwa ajili ya dhambi zao, kwa sababu walikuwa wakiasi agano la Mungu (32-37).

Baada ya kukiri makosa yao, watu walitoa ahadi ya agano kuwa waaminifu kwa Mungu. Walithibitisha ahadi yao kwa kiapo kilichoandikwa na kutiliwa sahihi na viongozi wao kwa niaba yao (38). Nehemia alikuwa wa kwanza kutia sahihi (10:1), akifuatwa na makuhani (2-8), Walawi (9-13) na viongozi wa kiraia (14-27). Watu wote waliapishwa juu ya maandiko ya agano hilo kuwa waaminifu kwa sheria ya Mungu (28-29).

Mambo muhimu zaidi yaliyotajwa katika maandiko hayo yalihusu ndoa za mchanganyiko (30, taz. Kut 34:15-16); siku ya Sabato na mwaka wa Sabato (31, taz. Kut20:8-10; 23:10-ll; Kum 15:1-2); kodi ya hekalu (32, taz. Kut 30:11-16); mahitaji kwa ajili ya hekalu na huduma zake (33-34); sadaka za malimbuko ya nafaka na wazaliwa wa kwanza wa wanyama (35-36, taz. Hes 18:13-18) na zaka (yaani utoaji wa sehemu ya kumi ya mapato, 37-39; taz. Hes 18:21-28).

Watu waliorudi na kuta zilivyotabarukiwa (11:1-13:3)

hariri

Orodha za wenyeji wa Yerusalemu (11:1-12:26)

hariri

Watu wengi zaidi waliorudi kutoka kifungoni waliishi katika nchi iliyozunguka Yerusalemu kuliko katika mji wenyewe. Kwa hiyo wenyeji wa mjini walikuwa wachache, na mikakati ikafanyika ili kupata wenyeji zaidi mjini. Katika mpango huo kila mtu wa kumi wa wenyeji walioishi katika maeneo ya nchini alipaswa kuhamia Yerusalemu, na hivyo Yerusalemu uliimarishwa. Zaidi ya hayo, kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuja kwa hiari yao waishi mjini (11:1-2).

Hapa tunapata orodha ya wakuu wa jamii mbalimbali waliokuwa wamerudi pamoja na Zerubabeli. Licha ya watu wale wa makabila ya Yuda na Benyamini (3-9), wengi wao wanaonekana kuwa ni makuhani, Walawi au watumishi wa hekaluni (10-21; taz. 1 Nya 9:1-34, ambapo orodha hiyohiyo imeandikwa yenye mabadiliko na nyongeza chache tu).

Mipango mingine ilifanywa kwa kuangalia kazi za Walawi, kuhusu waimbaji wa hekaluni na kumpata mjumbe wa Kiyahudi katika mahakama ya mfalme wa Uajemi (22-24).

Kisha orodha nyingine inafuata yenye majina ya miji iliyohamiwa upya na watu. Miji hiyo ilikuwa katika maeneo ya Yuda na Benyamini ya hapo awali (25-36).

Orodha nyingine ina majina ya makuhani na Walawi waliorudi pamoja na Zerubabeli na Yoshua (12:1-9). (Ezra aliyetajwa katika orodha hiyo si yule anayejulikana sana.)

Baada ya kuwaorodhesha watu wa vizazi sita vya Yoshua (10-11), mwandishi anarudia kuorodhesha vichwa vya nyumba nyingine za makuhani wa asili (12-21).

Licha ya kushughulika na familia za makuhani, maelezo pia yalihusu watumishi wa kawaida wa hekaluni. Maelezo mengine yalihusu hata mambo ya baada ya wakati wa Nehemia (22-26).

Kuzindua kuta za mji (12:27-13:3)

hariri

Habari zinaendelea tena pale zilipoachwa kwanza katika 10:39. Baada ya kusoma sheria, kusherehekea sikukuu ya Vibanda na kiapo cha watu kuhusu uaminifu wao kwa agano, kuta zilizinduliwa rasmi. Makuhani, Walawi, waimbaji na wenyeji wengine wenye heshima walishiriki katika sherehe hiyo (27-30). Watu walikutana sehemu moja karibu na kuta upande mmoja wa mji. Kisha wakagawanyika kuwa makundi mawili wakaanza kwenda kila upande kuzunguka kuta zote. Kundi moja liliongozwa na Ezra (31-37) na lingine liliongozwa na Nehemia (38-39). Makundi hayo mawili yakakutana tena upande mwingine wa mji karibu na hekalu watu walipounganika kwa kutoa sadaka na kumtukuza Mungu kwa furaha kubwa (40-43).

Hatimaye maafisa wakawekwa ili waangalie michango na matumizi ya fedha na vitu vingine ambavyo watu walivileta hekaluni. Waisraeli wote walitoa sehemu ya kumi ya mapato yao wakaiweka katika fungu hilo la jumla. Kutoka huko vitu vile vikagawiwa kwa Walawi waliowasaidia makuhani na kushughulika na nyimbo na muziki hekaluni. Walawi tena walitoa sehemu ya kumi ya mapato yao kuwa posho ya makuhani (44-47).

Masomo mengine ya sheria yaliwaonya watu kwamba walipaswa kutunza utakatifu wa hekalu. Wapagani au watu wa mataifa hawakuruhusiwa kuingia hekaluni (13:1-3).

Marekebisho ya Nehemia ya baadaye (13:4-31)

hariri

Baada ya miaka 12 ya kuwa liwali wa Yerusalemu, Nehemia alimrudia mfalme wa Uajemi kwa muda (taz. 5:14; 13:6). Wakati ule ambao Nehemia hakuwepo Yerusalemu, dini ya Wayahudi ilirudi nyuma, na maadui wao wa zamani, yaani San-balati na Tobia Mwamoni waliweza kupata nafasi ya ushawishi wao tena Yerusalemu. Kuhani mkuu, Eliashibu, alistahili kulaumiwa zaidi katika mambo hayo. Alimruhusu mtu wa familia ya kuhani mkuu kumwoa binti wa San-balati (taz. mstari 28), pia alimruhusu Tobia aishi katika chumba cha hekaluni. Jambo lile lilikuwa kinyume kabisa cha sheria ambayo Nehemia alijaribu kuitekeleza vizuri, kwa sababu Tobia alikuwa Mpagani (taz. 4:3; 13:1). Nehemia aliporudi Yerusalemu alirekebisha mambo hayo mara moja (4-9).

Nehemia pia aligundua kwamba watu walikuwa wamevunja ahadi mojawapo ya maana sana ya agano waliyokuwa wametoa wakati wa kuweka wakfu kuta za mji. Hawakutoa zaka zao, na matokeo yake, Walawi walipaswa kuacha huduma yao hekaluni na kwenda mashambani kwao ili kutafuta riziki zao (10-14; taz. 10:35-39).

Pia watu walifanya kazi na biashara siku ya Sabato, na hivyo walivunja sheria nyingine ya ahadi ya agano (15-18; taz. 10:31). Kwa haraka Nehemia alikomesha mambo hayo. Kwa kufunga milango ya mji siku ya Sabato, aliwazuia watu waliotaka kuleta bidhaa zao mjini. Pia aliwazuia wasiuze nje ya malango au kungoja huko wakijiandaa kuuza mara baada ya kupita Sabato (19-22).

Siku za Ezra watu walikuwa wameapa kwamba watawaondoa wake zao wa kigeni, na kweli walifanya hivyo (Ezra 10:19,44). Wakati huo desturi hiyo mbaya ilienea tena, nayo ilitishia kuharibu dini ya Waisraeli. Kwa ushujaa ule uliokuwa tabia ya Nehemia, alirekebisha hali hiyo (23-29). Hakuna shaka lolote kwamba yeye, zaidi ya mtu yeyote, aliwasaidia watu wa wakati ule kutengeneza maisha yao katika msingi wa dini ya kweli kadiri ya sheria ya Mungu (30-31).

Muhtasari

hariri

Sura 1-7 zinasimulia ziara ya kwanza ya Nehemia mjini na ujenzi wa ngome mpya kati ya upinzani mkubwa wa Wasamaria na wengineo.

Sura 8-10 zinaeleza marekebisho ya kidini na ya kijamiii aliyoyajaribu Nehemia.

Sura 11 hadi 13:3 zinaorodhesha watu waliorudi Yerusalemu na kusimulia jinsi ngome ilivyotabarukiwa.

Nehemia 13:4-31 inahusu ziara ya pili aliyoifanya miaka 12 baadaye.

Viungo vya nje

hariri
Vitabu vya ufafanuzi
Vinginevyo
Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.