Mapigano ya Tours na Poitiers

Mapigano ya Tours na Poitiers ilikuwa vita ya mwaka 732 kati ya jeshi la Waarabu Waislamu kutoka Hispania na jeshi la Wafaranki katika Ufaransa ya Kati.

Mapigano ya Tours na Poitiers - uchoraji wa karne ya 19

Waarabu katika Ulaya

hariri
 
Ramani ya maeneo chini ya utawala wa Kiislamu mnamo mwaka 720 kuanzia mipaka ya Uhindi hadi Hispania.

Waarabu walikuwa wamevuka mlango wa Gibraltar na kuvamia Hispania kuanzia mwaka 711. Mwaka 719 walivuka milima ya Pirenei na kuingia katika Gallia (leo: Ufaransa) ya kusini walipounda jimbo chini ya utawala wao. Wakati ule watawala wa sehemu za kusini wa Gallia-Ufaransa bado walikuwa Wagermanik Wavisigothi waliogawiwa kwa madola madogo ilhali kutoka kaskazini utawala wa Wafranki ulienea. Kutoka huko waliendelea na vita za kuteka nyara katika maeneo ya Wakristo.

Mwaka 732 jeshi kubwa linalokadiriwa kuwa na wanajeshi kati ya 30,000 na 80,000 likiongozwa na jemadari Abdul Rahman Al Ghafiqi likaelekea kaskazini kwa nia ya kupora mji tajiri wa Tours, kitovu cha kidini na cha kiutamaduni cha Gallia-Ufaransa.

Wafranki

hariri

Mtemi Mvisigothi wa sehemu zile aliitwa Odo akamwendea waziri mkuu wa Wafaranki Karolo Nyundo akaomba msaada wake na kumkubali kama mkuu wake. Karolo aliwahi kuimarisha utawala wa Wafaranki juu ya sehemu kubwa za Ujerumani na Ufaransa na kuwa na jeshi hodari la askari waliozoea kumfuata na kumtii. Karolo alijua ya kwamba askari wapandafarasi Waarabu walikuwa hatari sana akaona jeshi lake lililokuwa hasa wa askari waendao kwa miguu lilihitaji kupigana nao katika eneo lililofaa na hasa lenye vizuizi kwa farasi. Aliposikia kuwa Waarabu walikaribia, Karolo alikusanya jeshi lake juu ya mlima wenye miti mingi na kuwaamuru kusubiri palepale hadi Waarabu washambulie.

Waarabu walishtuka kukutana na jeshi kubwa kiasi lililosimama bila kuwashambulia. Kwa siku 6 majeshi mawili yalitazamana na kuwa na mapigano madogo tu. Ilikuwa mwezi wa Oktoba na hali ya hewa ilianza kuwa baridi. Askari Waarabu hawakuzoea sana kukaa katika baridi, tofauti na Wafaranki. Hivyo jemadari Mwarabu aliamua kushambulia ili wanajeshi waweze kupora katika mji wa Tours halafu kurudi kwao Hispania.

Mapigano

hariri

Jeshi la Wafaranki (kabila kubwa la Wagermanik lililotawala Ufaransa) chini ya makamu wa mfalme Karolo Nyundo lilikutana nao karibu na miji ya Tours na Poitiers. Karolo aliwasubiri wanajeshi wa nyongeza kutoka kwa Wasaksonia na Walangobardia, Waarabu waliwasubiri Wafaranki watoke nje ya misitu walipokuwa na kambi yao. Mwishowe Waarabu walishambulia siku ya saba lakini walishindwa kuvunja msimamo wa Wakristo. Jemadari Abdul Rahman Al Ghafiqi aliuawa mapiganoni, jeshi lake likakimbia na kurudi Hispania.

Umuhimu kwa historia ya Ulaya na ya Uislamu

hariri

Ushindi huu wa Wafaranki hutazamwa mara nyingi kama hatua muhimu ya kuzuia uenezaji wa Uislamu katika Ulaya ya Magharibi. Hata kama Waarabu walirudi miaka mitatu baadaye walishindwa tena wakikutana na Wafaranki waliojiamini wakishikamana kuzuia majaribio yote ya Waarabu kueneza utawala wao nje ya Hispania.

Waarabu waliendelea kukaa Hispania kwa karne zilizofuata lakini uenezaji wao ulisimamishwa.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mapigano ya Tours na Poitiers kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.