Mathayo wa Bascio
Mathayo wa Bascio, O.F.M. (jina la awali: Matteo Serafini; Pennabilli, 1495 hivi - Venezia, 6 Agosti 1552) alikuwa padri wa Utawa wa Ndugu Wadogo kutoka Dola la Papa, leo nchini Italia, ambaye ni maarufu kama asili ya tawi la Wakapuchini.
Mara alipopata upadrisho mwaka 1525 alijisikia hamu ya kuishi kikamilifu zaidi kadiri ya kanuni iliyoandikwa na mwanzilishi, Fransisko wa Asizi. Hivyo aliacha konventi yake akapewa na Papa Klementi VII (1523-1534) fadhili za kuvaa kanzu ya pekee, kushika ufukara kadiri ya kanuni, kuwa mkaapweke na kuhubiri anakotaka.
Ingawa viongozi wa shirika hawakupenda uhuru huo, Mathayo alipata mapema watu walioamua kumfuata katika urekebisho huo, kuanzia Ludoviko wa Fossombrone na Rafaeli wa Fossombrone.
Mtumishi wa kanda aliwatafuta sana, lakini walilindwa vizuri na Katerina Cibo, ndugu wa Papa. Ili kukwepa dhuluma, wakajiunga na Wakonventuali, halafu tarehe 3 Julai 1528 wakapewa na Klementi VII haki ya kuwa na Mtumishi wao chini ya Mkuu wa Wakonventuali na ya kupokea wanovisi.
Mapema walianza kuitwa Wakapuchini kutokana na kofia yao kubwa.
Walipokutana kwa mkutano mkuu wa kwanza mwaka 1529 huko Albacina, karibu na Fabriano, alichaguliwa mkuu wa kwanza, lakini baada ya muda mfupi alijiuzulu akarudi kati ya Waoservanti.
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |