Muungano na Mungu kwa njia ya Yesu ni lengo kuu la binadamu wote kadiri ya Ukristo na unatarajiwa kukamilika katika uzima wa milele, lakini unatakiwa kuanza katika maisha yao duniani kwa imani, sakramenti na utekelezaji wa maadili mema[1].

Walimu wa kiroho wameonyesha kwamba muungano huo unazidi kufikiwa katika sala ya kumiminiwa. Waliyoyasema si ya juu mno kwa mtu anayefuata njia ya unyenyekevu na kujikana, akizidi kuelewa kwamba Mungu “amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:52). Si ya juu mno kwa mtu anayeamini kwamba katika ubatizo amepokea mbegu ya uzima wa milele, na anayetambua haja ya kuzidi kusadiki thamani isiyo na mipaka ya ekaristi. Muhimu ni kupokea toka kwa Mungu yale yote anayotaka kutupatia kwa huruma yake isiyo na mipaka ili kutuvuta kwake na kutushirikisha milele uzima wake wa ndani na heri yake isiyo na mwisho.

Mtu akiwa mwaminifu – si tu katika kutimiza kwa makini wajibu wowote wa kila siku, bali pia katika kusikiliza minong’ono ya Roho Mtakatifu anayezidi kudai kadiri anavyofadhili – basi kwa kawaida anainuliwa hadi “muungano sahili”. Hapo kazi ya Mungu inakuwa na nguvu za kutosha ivute vipawa vya roho ambayo kazi yake yote inakuja kumuelekea yeye badala ya kupotea nje. Si utashi tu unatawaliwa naye (kama katika sala ya utulivu), bali pia akili na kumbukumbu, hata mtu ni kama ana hakika ya uwemo wa Mungu. Ubunifu hautikisiki tena, bali unatulia; pengine ni kama umesinzia ili kuacha akili na utashi viungane na Mungu. Hapo neema ya pekee ya Roho Mtakatifu ni kama maji yanayotiririka bustanini toka mtoni, kwa kutumia mfano wa Teresa wa Yesu.

Inatokea pia kwamba utendaji wote wa roho uende upande wake wa juu, hata kuna kusimamishwa kwa muda kwa hisi za nje, yaani mwanzo wa kutoka nje ya nafsi kama si kutoka kwenyewe. Ikiwa pengine mtaalamu aliyezamia somo lake hasikii anachoambiwa, zaidi tena itamtokea mtu aliyevutiwa na Mungu. Hapo anapokea maji hai ambayo yanaburudisha na kutakasa kama mvua toka mbinguni, kwa kutumia mfano mwingine wa Teresa wa Yesu, aliyesema, “Mungu hamuachii kutoa mchango mwingine isipokuwa ule wa utashi uliotawaliwa kabisa… Jinsi ilivyo nzuri hali inayompata kisha kuzama katika ukuu wa Mungu na kuungana kabisa naye, ingawa kwa muda mfupi, kwa sababu nionavyo mimi muungano huo haufikii kamwe nusu saa!”

Teresa anasema pia hiyo sala ya muungano mara nyingi si kamili, yaani ubunifu na kumbukumbu havisimamishwi, bali vinavipiga vita akili na utashi: “Kwa muungano tunaouzungumzia hapa, je, ni lazima vipawa hivyo visimamishwe? Hapana. Bwana anaweza kuwatajirisha watu kwa njia mbalimbali na kuwafikishia makao hayo bila kuwapitisha njia ya mkato niliyoielekeza”, yaani utamu wa kutokuwa na mitawanyiko ya mawazo, wa kutochoka na wa kusikia nderemo kwa wingi.

Matokeo ya sala ya muungano ni mtu kubadilika kama mdudu anapokuwa kipepeo. Anasikia majuto makubwa kwa makosa yake; anapata ari motomoto ya kumtumikia Mungu na kumtangaza ili apendwe; anaumia kuona wakosefu wakipotea;anahisi mateso ya Bwana yalivyokuwa. Hapo anaanza kutimiza maadili kishujaa, hasa kutii kikamilifu matakwa ya Mungu na kumpenda jirani. Pengine wafiadini walijaliwa sala hiyo katikati ya mateso yao.

Sala ya utulivu mtamu na ya muungano sahili zinapatikana kati ya matakaso ya Kimungu ya hisi na roho. Maana kwa kawaida kuna kipindi cha amani katika ya hayo mawili, yaani usiku wa hisi (mwanzo wa makao ya nne) na usiku wa roho (makao ya sita) unaoingiza katika muungano mkavu na muungano wa kutoka nje ya nafsi hadi kufikia muungano unaotugeuza.

Tanbihi

hariri
  1. Yoh 14:20; Yoh 15:4-5, 20; Rom 6:5; 1Kor 6:17; 2Kor 5:17; 2Kor 13:5; Gal 2:20; Ef 1:23; Ef 3:17; Ef 4:16; Ef 5:29-30; Kol 2:6; 1Yoh 3:9-10; 1Yoh 4:13-15
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Muungano na Mungu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.