Matakaso ya Kimungu
Matakaso ya Kimungu, kadiri ya teolojia ya maisha ya kiroho hasa katika Kanisa Katoliki, ni yale ambayo Mungu mwenyewe anawafanyia waamini
ili kuwatakasa kuliko wanavyojitahidi kujifanyia.
Utangulizi
haririUkamilifu wa Kikristo umo hasa katika upendo, ambao unatuunganisha na Mungu na jirani, lakini unadai pia matendo ya maadili mengine na ya vipaji vya Roho Mtakatifu. Ni kama binadamu ambaye mwili ni sehemu ya utu wake, ingawa utu umo hasa katika roho inayomtofautisha na wanyama. Hata katika suala hilo watu walipotoka pande mbili. Watulivu walipuuzia maadili hayo wakaacha utekelezaji wa kujinyima na wa kuwatendea mema majirani. Kinyume chao, wengine walisisitiza matendo ya toba, ibada na huruma wasitambue vya kutosha ukuu wa upendo wa Mungu, na hivyo wakazingatia juhudi zao na utume wa njenje kuliko mafumbo.
Ukamilifu wa Kikristo unadai matendo ya maadili mengine ambayo ni ya amri na yanatakiwa kuhuishwa na upendo. Amri kuu inatudai tuzidi kukua katika maadili yote kama vile katika upendo. Ukamilifu unadai maadili yote ya kumiminiwa na ya kujipatia, halafu vipaji saba ambavyo vinahusiana na upendo hivi kwamba vinakua pamoja nao.
Upendo ndio kiungo cha ukamilifu huo wa maadili na vipaji, ambavyo ni kama fungu la maua la kumtolea Mungu; lakini upendo wa wanaoanza hautoshi kuunda ukamilifu, mpaka ukue. Kwa kawaida upendo wa waliokamilika unapaswa kuwa mkubwa na motomoto kuliko ule wa wanaoanza na wanaoendelea; unadai pia utekelezaji wa maadili yote na wa vipaji saba kwa kiwango kinacholingana na upendo. Mtu hawezi kuwa mkamilifu bila kupenya mafumbo ya imani kwa kipaji cha akili, wala kuyaonja kwa kile cha hekima (ingawa hicho kinaelekea zaidi sala hasa katika watakatifu kadhaa na utendaji katika wengine).
Ili tuifikie hatua ya waliokamilika tunahitaji kujikana, kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu na kupokea kwa mikono miwili misalaba au matakaso yanayokusudiwa kufisha umimi na kuhakikisha ndani mwetu nafasi ya kwanza ishikwe moja kwa moja na upendo wa Mungu wenye kuangaza na kuwaka zaidi na zaidi.
Matakaso yanayodaiwa na ukamilifu wa Kikristo
hariri“Kwa ajili yake (Kristo) nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye… ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote kuufikia ufufuo wa wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo, kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu: nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu, katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo… Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo” (Fil 3:8-9,10-15,16). Ndio ukamilifu wa Kikristo kweli, si wa kifalsafa tu; nao umependekezwa kwa wale wote wanaolishwa na Maandiko hayo hadi mwisho wa dunia.
Watu kadhaa walisema Thoma wa Akwino alizungumzia kidogo tu matakaso ya Kiroho. Kumbe alifafanua maneno hayo kwa Wafilipi kuhusu kushiriki mateso ya Kristo kusudi tusipoteze misalaba yetu, tufanane naye na kuokoa watu pamoja naye (maana ulimwengu umejaa misalaba tasa, kama ule wa mhalifu wa pili aliyesulubiwa pamoja na Yesu: njia ya kuifanya ilete faida ni kuibeba kwa uvumilivu na upendo pamoja naye). Pia alifafanua mfano wa mzabibu wa kweli ambao Baba anausafishia kila tawi lizaalo: “Ili waadilifu wanaozaa matunda wazae kwa wingi zaidi, Mungu anapogolea ndani mwao yaliyo ya ziada; anawatakasa kwa kuwatumia tabu na kuruhusu washambuliwe na vishawishi ambavyo katikati yake wazidishe nguvu na juhudi. Hapana duniani mtu safi kiasi kwamba asihitaji kutakaswa zaidi”.
Ndiyo matakaso ya Kimungu yaliyokuja kuelezwa zaidi na Yohane wa Msalaba, mwalimu wa Kanisa aliyeyachimba kuliko wote. Katika mafundisho yake tunapata pia mwanga mkubwa ili kutofautisha hatua tatu za maisha ya Kiroho.
Basi, tuone yale yanayohitajika ili tufikie kilele cha ustawi wa kawaida wa upendo. Tunaposema kilele tusisahau neno kawaida; vilevile tunaposema kawaida tusisahau neno kilele. Mara nyingi tunaita “ya kawaida” yale ambayo wengi wanayafikia kweli, bila kujiuliza vya kutosha juu ya yale ambayo wangeyafikia kama wangekuwa waaminifu. Haifai kutamka kwamba “Muungano wa karibu mfululizo na Mungu uko juu kuliko kilele cha ustawi wa kawaida wa upendo”, kwa sababu tu wengi hawaufikii. Tusichanganye yanayotakiwa kuwepo na yale yaliyopo maishani, la sivyo tutasema uaminifu hauwezekani, kwa kuwa walio wengi wanajali faida yao (k.mf. pesa na anasa) kuliko uadilifu.
Wengi wanafuata yale yasiyo mabaya mno badala ya kutimiza wajibu unaowadai juhudi kubwa katika mazingira ambamo yote yanawaelekeza kudidimia; wanafuata mkondo kadiri ya sera ya kujitahidi kidogo iwezekanavyo. Si tu kwamba wanayavumilia yasiyo mabaya mno, bali wanayatenda na mara nyingi wanayaunga mkono ili wadumishe hali yao. Wanasiasa wengi wanajitetea kwamba wanafanya hivyo ili kuepa mabaya makubwa zaidi ambayo wengine wangeyafanya mahali pao kama wenyewe wangepotewa na wadhifa wao kwa kutowapendeza watu. Hivyo, badala ya kuwasaidia kurudi juu wanawasaidia kudidimia, wakijitahidi tu kupunguza kasi ya anguko. Kuna kitu cha namna hiyo katika maisha ya Kiroho pia.
Sheria ya ustawi wa upendo ni tofauti na ile ya ubinadamu wetu ulioanguka. Hata baada ya ubatizo tunaendelea kuwa na madonda yanayotuelekeza kudidimia, kumbe neema inayotuumba upya hatua kwa hatua inatufanya tupande daima. Tunapongojea uzima wa milele, maisha yetu yanatushangaza kwa jinsi yalivyo na mwanga na giza pamoja: “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana” (Gal 5:16-17). Upendo wa Kristo uliomo ndani mwetu haujashinda umimi wetu moja kwa moja, bali unahitaji bado kushindana nao kwa nguvu. Unahitajika utakaso mkubwa: si tu ule tunaotakiwa kujipatia, bali ule tunaopatiwa na Mungu anapokuja kupogolea matawi ya mzabibu ili yazidi kuzaa.
“Ili tufikie nuru ya Kimungu na muungano kamili wa upendo na Mungu - nayasemea yanayowezekana duniani - roho inapaswa kupitia usiku wenye giza… Kwa kawaida, wateule wanapojitahidi kufikia hiyo hali ya ukamilifu wanakuta giza nene, na kupaswa kuteseka katika mwili na roho namna ambayo ujuzi wa kibinadamu hauwezi kueleza hata kidogo… Picha zake hazijulikani na mtu isipokuwa na wale wenye mang’amuzi hayo” (Yohane wa Msalaba). Tawi ambalo Mungu analisafisha si hai tu, bali anajitambua pia, na ili mtu aweze kujua kupogolewa ni nini inabidi kumpate mwenyewe. Kila mmoja anapaswa kubeba msalaba wake, lakini hajui msalaba ni nini kabla hajaubeba kwa upendo.
Bila tabu hatufikii kushinda kikamilifu umimi, tamaa, uzembe, hasira, wivu, kijicho, utovu wa haki, kujipendea, kujidai kipumbavu, kujifanya lengo hata la ibada, hamu kubwa mno ya kufarijika, kiburi upande wa akili na wa roho, yale yote yanayopingana na imani na tumaini kwa Mungu, ili tumpende kikamilifu “kwa moyo wote, kwa akili yote, kwa nguvu zote, kwa roho yote” na kumpenda jirani, hata adui, tunavyojipenda. Tunahitaji kwa wingi imani, subira na ustahimilivu ili kudumu katika upendo kwa vyovyote, yanapotimia maneno ya Mtume Paulo: “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2Tim 3:12).
Kwa hiyo Yohane wa Msalaba, akielekeza njia inayofikisha kwa hakika na haraka zaidi kwenye ukamilifu, alisema hatuwezi kuufikia Mungu asipotutakasa hisi - ndiyo ishara ya kuingia hatua ya mwanga - na asipotutakasa roho - kwenye kizingiti cha hatua ya muungano. Kujitakasa hakutoshi: “Mtu, hata akiwa na juhudi namna gani, hawezi kujitakasa kikamilifu: hawezi kabisa kujiandaa aungane na Mungu kwa upendo kamili. Ni lazima Mungu mwenyewe ashughulike na kumtakasa kwa moto ambao ni giza kwa roho… Watu wanaanza kuingia huo usiku wa giza Mungu mwenyewe anapowakomboa polepole kutoka hali ya wanaoanza, ambapo wanatafakari katika njia ya Kiroho, ili awaingize katika hali ya wanaoendelea, ambayo ni ile ya wanasala. Wanapaswa kupitia njia hiyo ili wawe wakamilifu, maana yake wafikie muungano na Mungu”.
Kwanza tunaachishwa faraja za kihisi, ambazo zinafaa kwa muda, lakini zikitafutwa zinakuwa kizuio. Ndiyo sababu tunahitaji kutakaswa hisi kwa ukavu na kuongozwa kwenye maisha ya Kiroho yasiyotegemea mno hisi, ubunifu na mifuatano ya mawazo. Hapo, ingawa pana giza la kusumbua, tunaangaziwa na vipaji vya Roho Mtakatifu ujuzi unaotuingiza kwa undani katika mambo ya Mungu, tuyapenye pengine kwa nukta moja kuliko kwa miezi au miaka ya kutafakari. Ili kushinda vishawishi dhidi ya usafi wa moyo au ya subira, vinavyotokea mara nyingi wakati wa usiku wa hisi, unahitajika pengine ushujaa mkubwa unaoleta faida baadaye. Katika usiku huo hisi zinatupwa kwenye giza na ukavu kwa sababu ya kutoweka kwa neema za kihisi ambazo mtu alikuwa anaziishia akizifurahia kwa umimi. Lakini katika giza hilo, akili na utashi vinaanza kupata mwanga wa uzima ambao unapita mifuatano ya mawazo na unaelekeza kumkazia Mungu macho ya upendo katika sala. “Basi, mtu ametoka na kuanza kupenya njia ya roho wanayoifuata wale wanaoendelea, njia inayoitwa ya kuangazwa au ya kumiminiwa sala” (Yohane wa Msalaba).
Baadaye utahitajika utakaso mwingine wa kujaliwa ili kuondolewa kasoro ambazo “haziponyeki kadiri hao wanaoendelea wanavyodhani ni mema ya Kiroho… Basi, anayetaka kusonga mbele kweli, ni lazima apitie utakaso wa usiku wa roho. Hapo tu ataweza kuona njia ya kufaa aungane na Mungu” (Yohane wa Msalaba). Utakaso huo wa roho unawapata walioendelea zaidi ambao wanatamani mema lakini wanadai wayafanye wao na kwa namna yao. Hao wanapaswa kutakaswa kila namna ya kushikilia kibinadamu mawazo na matendo yao, namna yao binafsi ya kuona, kutaka na kutenda. Utakaso huo ukivumiliwa vizuri, katikati ya vishawishi dhidi ya maadili ya Kimungu, unawazidishia mara mia imani, tumaini na upendo.
Jaribu hilo linajitokeza kwa namna tofauti katika maisha ya sala tu na katika yale ya kitume. Pia ni tofauti kadiri linavyolenga kumfikisha mtu mapema kwenye ukamilifu mkuu au linavyotokea mwishoni tu ili kumsaidia kutakaswa walau kiasi kabla hajafa, akistahili kwa ustawi wa upendo, si toharani asipoweza kustahili. Hivyo dogma ya purgatorio inathibitisha haja ya matakaso hayo.
Hapo mchanganyiko wa mwanga na giza ni mkubwa kuliko ule wa usiku wa hisi. Mtu anaonekana amekosa urahisi wa kusali na wa kutenda aliokuwa anaufurahia mno kutokana na mabaki ya kujipendea na kiburi. Lakini katika huo usiku wa roho unaonekana mwanga mkuu zaidi; polepole, katikati ya vishawishi dhidi ya imani, tumaini na upendo, zinajitokeza kama nyota kuu tatu sababu zenyewe za maadili hayo ambazo ni: ukweli asili wenye kufunua, huruma yenye kusaidia na wema mkuu wa Mungu. Mtu anafikia kumpenda kwa usafi mkubwa na kwa uwezo wake wote.
Maelezo hayo yanahitajika tusije tukapunguza ukuu wa ustawi kamili wa kawaida wa maisha ya Kikristo. Kilele hicho kinachoweza kufikiwa duniani ni kile cha heri nane za Injili: hizo (hasa zile za mwisho) zinapita juhudi na kupatikana upande wa mafumbo, kama hayo matakaso ya Kimungu.
Ukamilifu wa Kikristo na sala ya kumiminiwa
haririFundisho la kwamba ukamilifu unadai matakaso ya Kimungu ya hisi na roho lina mengi yanayotokana nalo. Kwanza, sala ya kumiminiwa, yaani kuzama katika mafumbo ya imani, imo katika njia ya kawaida ya utakatifu, kwa kuwa inaanza katika ukavu wa utakaso wa hisi. Ingekuwa kosa kubwa kuchanganya sala hiyo na faraja ambazo hazifuatani nayo daima. Usemi wa kuwa mizizi ya ujuzi ni michungu lakini matunda yake ni matamu unafaa kuhusu mizizi na matunda ya sala ya kumiminiwa. Pili, siku hizi hakuna tena mtu anayesema kuzama katika mafumbo ni karama tu, kama ile ya unabii au ile ya kusema kwa lugha ngeni. Wote wanakubaliana sala hiyo inahusiana na neema inayotia utakatifu, yaani neema ya maadili na vipaji. Hatimaye, tusipoweza kustahili neema ya kuzama katika sala, maana yake si kwamba ipo nje ya njia ya kawaida ya utakatifu. Mwadilifu hawezi kustahili vilevile neema ya kufa kitakatifu, ingawa ni ya lazima kwa uzima wa milele. Wala hawezi kustahili neema ya hakika inayomkinga dhidi ya dhambi ya mauti ili adumu katika neema inayotia utakatifu. Lakini zawadi hizo asizoweza kuzistahili, anaweza kuzipata kwa sala nyenyekevu, zenye tumaini na udumifu.
Tusichanganye maswali mawili yafuatayo: “Je, sala ya kumiminiwa ipo katika njia ya kawaida ya utakatifu? Je, waadilifu wote wanaweza kuifikia, bila kujali tofauti za mazingira, malezi na uongozi?” Kama vile isivyofaa kuchanganya haya yafuatayo: “Je, neema inayotia utakatifu ni mbegu ya uzima wa milele? Je, kati ya wale walioipokea kwa ubatizo au kati ya waliodumu nayo miaka kadhaa, wataokoka wote au walau wengi wao?” Wanasala hasa ni wachache kwa sababu wachache tu wanajua kujitenga na viumbe. Wengine wanaweza wakawa na nia njema, lakini hawana juhudi zile zote zinazohitajika ili kufikia ukamilifu. Tena ili kuufikia ni muhimu kupata malezi mazuri na uongozi mzuri, ingawa Mungu anavifidia kwa watu kadhaa wenye juhudi nyingi. Tusisahau pia kwamba wito wa kuwa mwandani wake unaweza kuwa wa jumla na wa mbali tu, au maalumu na wa jirani. Tena huo wa pili unaweza kuwa wa kutosha au wa hakika. Hatimaye huo wa hakika unaweza kuhusu viwango vya chini au vile vya juu vya muungano na Mungu.
Tusipunguze ukuu wa lengo; kuhusu njia za kulifikia, busara izipendekeze kulingana na hali mbalimbali za watu, na kadiri walivyo kati ya wanaoanza au wanaoendelea. Hivyo tutahakikisha ukuu wa lengo, na uongozi wa kufaa kulifikia.