Pierre Nkurunziza

Pierre Nkurunziza (18 Desemba 1963 - 8 Juni 2020) alikuwa mwanasiasa kutoka nchini Burundi, na rais wa taifa hilo tangu mwaka 2005 hadi kifo chake.

Pierre Nkurunziza


Rais wa Burundi
Muda wa Utawala
26 Agosti 2005 – 8 Juni 2020
Makamu wa Rais Martin Nduwimana
Yves Sahinguvu
Terence Sinunguruza & Gervais Rufyikiri
mtangulizi Domitien Ndayizeye

tarehe ya kuzaliwa 18 Desemba 1963 (1963-12-18) (umri 61)
Bujumbura, Burundi
tarehe ya kufa 8 Juni 2020
chama Baraza la Kitaifa kwa kutetea demokrasia, Burundi (CNDD-FDD)
ndoa Denise Bucumi
watoto 5
mhitimu wa Chuo Kikuu cha Burundi
dini Ukristo, Uprotestanti
signature

Alikuwa mwenyekiti wa chama cha Baraza la Kitaifa la Kutetea Demokrasia, Burundi (CNDD-FDD) hadi kuchaguliwa kuwa rais.

Tarehe 13 Mei 2015 kundi la wanajeshi wa nchi walitangaza kupinduliwa kwake,[1] lakini saa chache baadaye wakakamatwa.

Historia yake

hariri
 
Pierre Nkurunziza, akiwa rais wa Burundi, akitembelea nchi ya Norwei tarehe 10 Juni 2006.

Nkurunziza alizaliwa mwaka 1963 mjini Bujumbura katika familia ya kabila la Wahutu.[2]

Alisoma shule ya msingi kwenye mkoa wa Ngozi.

Baba yake Eustache Ngabisha alikuwa mbunge wa Burundi mwaka 1965 akaendelea kuwa mkuu wa mkoa katika mikoa miwili. Mzee aliuawa katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1972 pamoja na Warundi wengine 400,000 hivi.

Nkurunziza alikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Burundi wakati vita ya wenyewe kwa wenyewe ilianza baada ya kuuawa kwa rais wa kwanza aliyechaguliwa kutoka jamii ya Wahutu Melchior Ndadaye mwaka 1993.

Baada ya shambulio la jeshi dhidi ya Wahutu kwenye chuo kikuu alijiunga na kundi la CNDD-FDD mwaka 1995 akawa askari na kupanda ngazi hadi kuwa makamu wa mwenyekiti wa CNDD-FDD mnamo 1998, halafu mwenyekiti mwaka 2001.[3]

Baada ya mapatano ya amani ya mwaka 2003 aliendelea kuwa waziri wa utawala katika serikali ya mpito ya rais Domitien Ndayizeye.

Baada ya ushindi wa CNDD-FDD katika uchaguzi wa 2005 alichaguliwa na bunge kuwa rais. Alichaguliwa tena kwa kura ya wananchi wote mwaka 2010.

Mwaka 2015 alitangaza nia ya kugombea urais tena. Hii imesababisha ghasia kwa sababu wapinzani walidai kufuatana na katiba ya nchi anastahili kuongoza vipindi viwili tu. Mwenyewe pamoja na chama chake anadai ya kwamba mara ya kwanza alichaguliwa na bunge tu na kikatiba anastahili kuchaguliwa mara mbili na wananchi wote.

Tarehe 24 Julai 2015 Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Nkurunziza mshindi wa uchaguzi kwa 69.41% za kura. Agathon Rwasa alishika nafasi ya pili kwa 18.99% ingawa alikuwa amehimiza wananchi wasipige kura.

Mwaka 2020 aliamua kutogombea tena. Mshindi wa uchaguzi kwenye Mei 2020 alikuwa Evariste Ndayishimiye aliyepangwa kula kiapo kama rais mpya kwenye Agosti 2020.

Maisha ya binafsi

hariri

Nkurunziza alilelewa pamoja na ndugu 7. Watano kati yao waliuawa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya 1993 au katika mapigano kama wanamgambo wa CNDD-FDD. Leo hii ana dada 1 aliye hai.

Alipenda kucheza mpira wa miguu.

Tarehe 6 Juni 2020 alikuwa akishiriki kucheza mpira wa kikapu kwenye mji wa Ngozi kaskazini mwa Burundi. Akapata shtuko la moyo akapelekwa hospitalini; siku iliyofuata alionekana kupata nafuu lakini siku ya Jumatatu hali yake ilikuwa mbaya akaaga dunia hospitalini.

Marejeo

hariri
  1. Taarifa ya BBC
  2. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-12-12. Iliwekwa mnamo 2015-05-08.
  3. http://www.culturaldiplomacy.org/academy/index.php?pierre-nkurunziza

Viungo vya Nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: