Qabus bin Said al Said

(Elekezwa kutoka Qaboos bin Said al Said)

Qabus bin Said al Said (pia Qaboos; ar. قابوس بن سعيد آل سعيد‎; 18 Novemba 1940 - 10 Januari 2020) alikuwa Sultani wa Oman tangu mwaka 1970 hadi 2020. Alikuwa kizazi cha kumi na nne cha mwanzilishi wa Jumba la Al Said. Alikuwa kiongozi aliyehudumu miaka mingi katika Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiarabu, akihudumu kwa karibu miaka hamsini.

Qabus bin Said al Said.

Qabus alikufa kwa saratani tarehe 10 Januari 2020 huko Muskat, Oman akiwa na umri wa miaka 79. [1].

Baada ya kifo chake Haitham bin Tariq al Said amekuwa Sultani wa Oman. [2]

Miaka ya kwanza

hariri

Qabus ibn Said alikuwa mwana pekee wa Sultani Said ibn Taimur na mkewe Mazun. Yeye yuko kizazi cha saba cha nasaba ya Al-Bu-Sa'id iliyoanzishwa na Imam Ahmad ibn Sa'id mnamo 1741.

Alizaliwa mjini Salalah iliyokuwa mji mkuu wa Omani chini ya baba yake na huko alisoma shule.

Mwaka 1958 alitumwa Uingereza alipoingia katika shule ya sekondari ya bweni. Baada ya kutimiza miaka 20, aliingia 1960 kwenye Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst, Uingereza.

Mwaka 1962, akiwa luteni, alitumwa kuhudumia katika jeshi la Uingereza huko Ujerumani.

Baada ya kurudi Omani mnamo mwaka 1964, alizuiliwa na babake asiwasiliane na watu wengi. Qaboous alianza kuelewa jinsi gani nchi yake ilikuwa nyuma mno kimaendeleo.

Kumpindua baba na kushika usultani

hariri

Qabus aliporudi kutoka Uingereza, Omani ilikuwa na matatizo. Kwa upande mmoja mafuta ya petroli yalianza kupatikana na kuleta mapato kwenye mfuko wa sultani. Kwa upande mwingine babake alikataa mabadiliko nchini; nchi yote ilikuwa na kilomita 10 za barabara ya lami na hospitali 1 pekee. Kwa amri ya sultani geti za miji zilifungwa wakati wa machweo; mtu yeyote aliyetembea nje ya nyumba yake wakati wa usiku alitakiwa kutembea kwa kushika koroboi maana miji haikuwa na taa[3]. Sultani mzee hakupenda kujenga shule kwa wananchi walioendelee kuishi maisha ya wavuvi, wafugaji na wakulima. Sultani Taimur mwenyewe alisisitiza kuangalia maombi yote ya wageni kupata viza akakubali wachache. Sultani mzee alikuwa na wasiwasi juu ya mwanawe aliyerudi kutoka Uingereza na mawazo mapya akamweka chini ya ulinzi katika sehemu ya kasri yake[4].

Wakati huohuo, kulikuwa na uasi katika eneo la Dhofar, magharibi mwa Omani. Jeshi la Sultani, ambalo wakati ule liliongozwa na maafisa Waingereza, lilipambana na waasi wa kikabila walioongozwa na wanamapinduzi Wakomunisti kutoka nchi jirani ya Yemen Kusini. Waingereza walihofia kwamba siasa ya sultani Taimur ingeongeza nguvu ya uasi pamoja na athira ya Wakomunisti katika Omani. Hivyo walipanga mapinduzi ya kijeshi na kukabidhi mamlaka kwa kijana Qabus.[5].

Qabus alikubali akashika madaraka tarehe 23 Julai 1970. Sultani Taimur aliyejeruhiwa wakati alipokamatwa katika makazi yake, alipelekwa Uingereza alipotibiwa na kupewa mahali pa kukaa chini ya ulinzi. Sultani mzee aliaga dunia mwaka 1972.

Utawala

hariri

Mwanzoni, Qabus alikazia ukandamizaji wa uasi katika Dhofar. Aliomba msaada na wanajeshi kutoka Jordani, Iran na Uingereza; pia aliahidi kumsamehe mara moja mwasi yeyote aliyerzd upande wa serikali. Hadi mwaka 1975 amani ilirudishwa Dhofar.

Mkazo mwingine ilikuwa kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi na kufanya Omani kuwa nchi ya kisasa. Mwanzoni wa utawala wake alipiga marufuku utumwa. Oman ilijiunga na Umoja wa Mataifa na Ligi ya Kiarabu mnamo 1971. Qabus alitumia mapato ya mafuta kwa kuwekeza pesa katika ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, na shule na kuanzisha huduma za afya. Tangu miaka ya 1980, uwekezaji ummelega zaidi upande wa kuanzisha viwanda na kujenga kilimo cha kisasa ilhali nchi iliendelea kutegemea mapato ya uuzaji wa mafuta. Katika miaka 50 ya utawala wake nchi ilisogea mbele na mapato ya wananchi yaliongezeka mara 50.

Mabadiliko haya hayakwenda sambamba na mabadiliko ya siasa ambako sultani aliendelea kushika madaraka yote, pamoja na kutangaza sheria na kuteua majaji. Qabus mwenyewe alikuwa waziri mkuu akisimmia pia wizara ya ulinzi, ya fedha na mambo ya nje na kuwa rais wa Benki Kuu ya Oman. [6] 1991 sultani alianzisha Baraza la Ushauri lenye wanachama wanaochaguliwa na kupewa kazi ya kujadili sheria zinazoendelea kutungwa na serikali. Baada ya maandamano katika nchi za Kiarabu za kudai demokrasia zilizofika pia Omani kwenye mwaka 2011, Qabus alitangaza nia ya kupeleka mfumo wa nchi kuwa ufalme wa kikatiba lakini hii haikutekelezwa hadi kifo chake.

Siasa ya Nje

hariri

Katika siasa ya nje Qabus alifaulu kutoshiriki katika mapambano kati ya nchi jirani (kama vile Saudia, Yemen, Iran) na Marekani. Alilenga kutunza mawasiliano na uhusiano na pande zote hadi akapokea viongozi wa Israeli. Aliweza mara kadhaa kupatanisha maadui au kuleta maelewano kati ya maadui.

Qabus alikuwa na uhusiano wa karibu na Iran kuliko majirani Waarabu akifaulu kutosimamama upande wowote katika fitina baina ya Iran, Saudia na Marekani.[7] Mara kwa mara Omani iliweza kusaidia mawasiliano kati ya pande mbili.[8][9] Qabus aliwezesha majadiliano ya siri baina ya Marekani na Iran kuhusu mapatano ya kinyuklia yaliyokubaliwa wakati wa Rais Obama na kuachwa baadaye na Rais Trump.[10]

Mwaka 2011 Qabus alisaidia kuachishwa kwa watalii wa Marekani waliowahi kukamatwa na Iran na kuhukumiwa kuwa wapelelezi.[11]

Qabus alikataa kushiriki katika mashambulio ya Saudia na UAE dhidi ya Wahuthi wa Yemen mwaka 2015, na hakuchukua upande katika fitina baina ya Saudia na Qatar mnamo 2016.

Mnamo Oktoba 2018, Qabus alimkaribisha waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kutembelea Oman ingawa hakuna uhusiano wa kibalozi baina ya nchi hizo. Netanyahu alikuwa kiongozi wa pili wa Israeli aliyetembelea Oman, baada ya ziara ya Shimon Peres mnamo 1996.[12]

Maisha ya binafsi

hariri

Qabus alifunga ndoa kwa miaka kuanzia 1976 hadi 1979 iliyokwisha baada ya talaka. Hakuoa tena wala hakuzaa watoto. Alipoaga dunia mwaka 2020 baada ya kipindi cha kugonjeka kansa, familia pamoja na wawakilishi wa serikali, bunge la ushauri na jeshi walimteua binamu yake Tariq bin Taimur Al Said aliyetajwa katika barua iliyoandikwa na Qabus kabla ya kifo chake na kutunzwa kama siri lakini ilifunguliwa baada ya kifo chake.

Marejeo

hariri
  1. Sultan Qaboos of Oman dies aged 79
  2. "Oman names culture minister as successor to Sultan Qaboos". AP NEWS. 2020-01-11. Iliwekwa mnamo 2020-01-11.
  3. Coup in Oman: : Out of Arabian Nights Into 20th Century, taarifa ya Dana Adams Schmidt Special kwenye The New York Times, tar. 5 Septemba 1970
  4. Sultan of Muscat and Oman Is Overthrown by Son, gazeti la New York Times, July 27, 1970, iliangaliwa Januari 2020
  5. Britain’s coup in Oman, 1970, tovuti ya Mark Curtis, Declassified UK, February 6, 2016
  6. Stephen Kinzer: The joy of benevolent dictatorship, The Boston Globe, 14. März 2017
  7. Slackman, Michael. "Oman Navigates Between Iran and Arab Nations", The New York Times, 16 May 2009. 
  8. Gladstone, Rick. "Iran’s President to Speak at the U.N.", 4 September 2013. 
  9. "A visit from the sultan".
  10. "Oman's Sultan Qaboos dies, cousin Haitham named successor". The Jerusalem Post | JPost.com.
  11. "Oman Played Pivotal Role In Americans' Release". NPR.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 11 Januari 2020.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  12. "Netanyahu makes historic visit to Oman". The Jerusalem Post | JPost.com.
  Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Qabus bin Said al Said kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.