Tulia Ackson

Mwanasiasa wa Tanzania

Tulia Ackson (amezaliwa 23 Novemba 1976) ni mwanasheria na mwanasiasa Mtanzania mwanachama wa Chama cha kisiasa cha Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hon. Dr. Tulia Ackson
Nchi Tanzania
Kazi yake mwanasheria na mwanasiasa
Cheo Spika wa bunge la Tanzania
Chama cha kisiasa CCM

Tarehe 1 Februari 2022 alichaguliwa na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa spika wa Bunge hilo. [1]

Maisha hariri

Ackson alizaliwa kwenye kata ya Bulyaga, Tukuyu, kwenye wilaya ya Rungwe. Alisoma shule huko Tukuyu na Mbeya.

Miaka 1998-2003 alisoma sheria kwenye chuo kikuu cha Dar es Salaam akaendelea kusomea shahada ya uzamivu huko Cape Town, Afrika Kusini miaka 2005-2007.

Alirudi Dar es Salaam alipofundisha sheria kwenye chuo kikuu hadi mwaka 2014 alipoteuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Mwaka 2015 alikuwa kati ya wabunge 10 walioteuliwa na rais John Magufuli kuingia bungeni kwa miaka 20152020 [2] akachaguliwa pia kuwa naibu spika.

Tulia Ackson kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amechaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabaraza ya Kitaifa Duniani (IPU) na Baraza la Uongozi la IPU, chombo chake kikuu cha kufanya maamuzi kinachojumuisha wabunge kutoka duniani kote.

Anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Duarte Pacheco, mbunge kutoka Ureno, ambaye alimaiza muda wake wa miaka mitatu mwishoni mwa Mkutano wa 147 wa IPU huko Luanda, Angola.

Baada ya kuchaguliwa, Ackson alisema: “Asanteni kwa imani mliyonipa kwa kunichagua. Ninasikiliza nafasi hii kwa unyenyekevu huku nikifahamu majukumu yote inayokuja nayo. Nawathibitishia azma yangu ya kufanya kazi pamoja nanyi kufanya IPU iwe taasisi yenye ufanisi zaidi, inayowajibika na inayoeleweka.”

Wabunge walipiga kura kwa siri. Kukiwa na wagombea wanne kwenye kura, Rais mpya wa IPU alichaguliwa kwa 57% ya kura baada ya duru moja ya upigaji kura.

Wabunge kutoka Mabaraza 130 ya IPU wanachama walishiriki katika uchaguzi huo. Kwa lengo la kukuza usawa wa jinsia, kila Baraza la IPU lilistahili kupiga kura tatu ikiwa na uwiano sawa wa jinsia. Vikundi vyenye wajumbe wa jinsia moja walistahili kura moja tu.

Kwa mara ya kwanza katika historia, wagombea wote wengine watatu kwenye kura – Adji Diarra Mergane Kanouté wa Senegal, Catherine Gotani Hara wa Malawi na Marwa Abdibashir Hagi wa Somalia – walikuwa wabunge wanawake kutoka Afrika.

Tulia Ackson ni mwanamke wa tatu tu kuwa Rais wa IPU baada ya Najma Heptulla wa India (1999–2002) na Gabriela Cuevas wa Mexico (2017–2020). Pia, yeye ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushikilia nafasi hiyo.

Marejeo hariri

  1. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2022-02-01. Iliwekwa mnamo 2022-02-01. 
  2. Tovuti ya Bunge la Tanzania, iliangaliwa Mei 2017