Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani ilipigwa kuanzia mwaka 1861 hadi 1865 kati ya majimbo ya kusini na majimbo ya kaskazini nchini Marekani. Mwaka 1861 kundi la majimbo ya kusini lilijitenga na Muungano wa Madola ya Amerika likajiita "Shirikisho la madola ya Amerika" (Confederate States of America). Serikali ya Muungano haikukubali hatua hiyo ukaiona kama uasi. Mashambulio ya jeshi la kusini dhidi ya vituo vya kijeshi ndani ya kusini vilivyokuwa chini ya amri ya Muungano yalianzisha vita iliyodumu hadi 1865 na kuleta ushindi wa kaskazini, yaani jeshi la Muungano. Shirikisho likavunjwa na majimbo yake kurudishwa katika Muungano. Vita hii ilileta vifo vingi, pamoja na mwisho wa utumwa katika Marekani.
Mandharinyuma ya vita
haririTofauti za kusini na kaskazini ya Marekani
haririSababu za vita zilianza katika tofauti kubwa baina ya kaskazini na kusini ya Marekani tangu mwanzo wake. Marekani ilianzishwa kutokana na uasi wa makoloni ya Uingereza kwenye pwani ya Amerika Kaskazini zilizotaka haki za kujitawala. Lakini makoloni hayo yalikuwa na tofauti za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi kati yao tangu mwanzo. Katika kusini, mashamba makubwa ya pamba, mpunga, tumbaku na miwa yalikuwa muhimu. Ilhali hapakuwa na wafanyakazi wa kutosha wenye mashamba walianza kuchukua kwanza Waingereza maskini na baadaye watumwa kutoka Afrika. Katika kaskazini, mashamba makubwa hayakuwa muhimu vile; makoloni kadhaa yaliundwa na makundi ya kidini ambayo yalikataa utumwa, hasa Makweka. Wahamiaji wengi kutoka Ulaya walielekea kaskazini ambako hali ya hewa ilifanana zaidi na Ulaya na hivyo idadi ya wakazi iliongezeka kushinda kwenye majimbo ya kusini. Sehemu kubwa ya ardhi ya kaskazini ililimwa na wakulima wadogo waliofanya shughuli zao wenyewe bila watumwa.
Utumwa na uzito wa kisiasa
haririMwaka 1787 baada ya uhuru na wakati wa kuundwa kwa katiba ya Muungano wa Marekani swali muhimu lilikuwa jinsi ya kukadiria kiasi cha kodi ambacho kila jimbo lilitakiwa kuchangia katika muungano pamoja na swali kuhusu idadi ya wawakilishi wa kila jimbo kwenye bunge. Majimbo ya kusini yalikataa kutumia idadi ya wakazi pekee kama kizio; hatimaye walifikia mapatano kuwa msingi kuwa idadi ya wakazi katika kaskazini lakini kwa majimbo ya kusini penye watumwa wengi ilikuwa idadi ya watu weupe pamoja na 3/5 ya idadi ya watumwa. Kanuni hii ilitumiwa pia katika makadirio ya idadi ya wawakilishi kila jimbo lilistahili kutuma bungeni. Kwa hiyo swali la watumwa na tofauti kuhusu watumwa katika kusini na kaskazini lilikuwa swali la kisiasa tangu mwanzo wa Marekani. Majimbo kadhaa ya kaskazini yaliwahi kukataa au kudhibiti utumwa tayari wakati wa kutunga katiba. Bunge la taifa lilianzishwa kuwa na vitengo viwili; upande wa Senati kila jimbo lilipata wawakilishi 2 kama ni jimbo kubwa au ndogo; lakini upande wa Nyumba ya Wawakilishi idadi ya wabunge ilitakiwa kulingana na idadi ya raia wenye kura na hapo watumwa -ambao hawakuwa na haki ya kura- walihesabiwa kwa kiwango cha 3/5. Katika miaka iliyofuata polepole majimbo mengi ya kaskazini yalipiga utumwa marufuku kwa kufuata mantiki ya Tangazo la Uhuru la Marekani kutoka Uingereza lililowahi kusema "binadamu wote wameumbwa sawa, wamepewa na Muumbaji haki maalumu kama vile uhai, uhuru na kufuatia raha". Sababu nyingine zilikuwa tofauti za kiuchumi; majimbo ya kaskazini yalianza kuwa na viwanda na miji mingi mikubwa lakini uchumi wa kusini ulikuwa hasa kilimo kilichotegema kazi ya watumwa. Hata hivyo, katika majimbo ya kusini utumwa ulikuwa tayari nguzo ya uchumi kwa hiyo mawazo ya kaskazini yalikuwa na wafuasi wachache; pamoja na hayo, kuwepo kwa tabaka la watumwa weusi kuliunganisha wazungu maskini na tajiri katika majimbo ya kusini; maana hata kama raia alikuwa maskini hakuwa kwenye msiosho wa ngazi, muda wote aliona watu waliokuwa chini yake.
Kutafuta uwiano kati ya majimbo ya watumwa na majimbo yaliyokataa watumwa
haririUwiano kati na majimbo yenye msimamo tofauti katika swali la utumwa uliendelea kuwa changamoto katika siasa ya Marekani. Maungano ya Marekani yaliendelea kukua; walowezi kutoka Ulaya walifika na kuingia katika maeneo mapya walipoanzisha mashamba na miji mipya na wakati uleule kuwasukuma Maindio wenyeji, waliowahi kupungukiwa kutokana na magonjwa ya kigeni kutoka Ulaya, kuelekea magharibi. Katika maeneo haya majimbo mapya yalianzishwa yaliyopokelewa katika Muungano. Hapa swali la utumwa ulikuwa muhimu hasa katika kutunza uwiano kati ya majimbo yenye watumwa na majimbo yaliyokataa utumwa. Harakati za kupinga utumwa kisiasa yalikua katika kaskazini. Wafuasi wake walisikitika uwezo na athira ya matajiri wa kusini waliotumia kazi ya watumwa; waliogopa upanuzi wa utumwa katika Marekani; wengine kwa sababu za kiutu na kidini, wengine wakiogopa kushindana na kazi rahisi ya watumwa ingeleta hasara kwa wakulima wadogo.
Katika maeneo ya Kansas na Nebraska swali la utumwa lilisababisha mapigano na mauaji. Serikali kuu ilitaka kuingiza maeneo hayo rasmi katika Muungano; majimbo ya kusini yalikataa kwa hofu ya kuongeza idadi ya majimbo bila utumwa. Hatimaye wanasiasa walipatana kuacha jambo hili wazi hadi raia wa majimbo wangeamua baadaye wenyewe kukubali au kukataa utumwa katika maeneo yale, badala ya kuamua katika bunge. Mapatano hayo yalitazamiwa kama uhaini na watu wengi katika kaskazini. Kansas iliona mapigano kati ya watetezi na wapinzani wa utumwa ambako miongo ya watu waliuawa; kiongozi mkali wa wanamgambo wa upinzani wa utumwa alikuwa John Brown aliyejaribu baadaye, mnamo mwaka 1859, kuanzisha uasi wa watumwa huko Virginia katika mashambulio ya Harper's Ferry.
Kukua kwa harakati dhidi ya utumwa, uchaguzi wa Lincoln na farakano
haririKatika kaskazini chama kipya cha Republican Party kilikua kilichopinga upanuzi wowote wa utumwa. Marepublican hawakulenga kufuta utumwa lakini walitaka kuzuia upanuzi wake katika maeneo mapya, hata hivyo viongozi wa kusini waliogopa wangeweza kuleta mwisho wa utumwa[1]. Uchaguzi wa mwanasiasa Abraham Lincoln katika Novemba 1860 aliyekuwa mgombea wa Republican kuwa rais wa Marekani ulisababisha matangazo ya majimbo yafuatayo kuondoka katika Muungano: South Carolina ilitangulia tarehe 20 Desemba 1860, iliyofuatwa katika Januari 1861 na Mississippi , Florida, Alabama, Georgia na Louisiana. Wabunge wao walikutana kwenye Februari 1861 wakaunda bunge la Shirikisho na kumchagua Jefferson Davis kutoka Missisippi kuwa rais wakaendelea kukubali katiba ya Shirikisho. Hayo yote yalitokea kabla Abraham Lincoln kuingia madarakani tarehe 4 Machi 1861. Majimbo mengine yalifendelea kujitenga na Muungano na kujiunga na Shirikisho: Texas kwenye mwezi Machi na Virginia kwenye Aprili, Tennessee, Arkansas na North Carolina kwenye Mei 1861.
Kwa hiyo majimbo 11 kati ya 34 yalitangaza kujitenga na Muungano, sehemu za majimbo mawili yalifuata. Majimbo yote ya kusini yalikuwa na wakazi milioni 9 hivi, lakini kati ya hao zaidi ya milioni 3 walikuwa watumwa wenye asili ya Kiafrika; majimbo ya kaskazini yalikuwa na wakazi milioni 21; karibu viwanda vyote vilikuwa kwenye kaskazini.
Majaribio ya upatanisho
haririKulikuwa na majaribio ya kutafuta mapatanisho; pendekezo moja lilikuwa kutumia mstari wa latitudo 36°30′ ambo ulikuwa mpaka wa kaskazini wa Missiouri; maeneo yote mapye katika magharibi upande wa kusini wa mstari huo yangekuwa majimbo ya watumwa, yote upande wa kaskazini yangekuwa maeneo bila watumwa. Marepublican walikataa walikuwa tayari kuahidi usalama wa utumwa katika maeneo ulipokuwepo tayari, ambayo haikutosha kwa viongozi wa kusini.
Katika ghotuba yake baada kuapishwa rais Lincoln alisema kwamba hatambui hatua za kujitenga na Muungano; alitangaza hakuwa na nia ya kuvamia majimbo yaliyojitenga wala kumaliza utumwa pale, lakini alisisitiza angekuwa kutumia nguvu kutetea mali ya Muungano katika majimbo yote, kama vile ngome za kijeshi, vituo vya bandari na vya posta. Alisihi majimbo ya kusini kurudi katika muungano.
Wawakilishi wa kusini walifika Washington walikuwa tayari kufanya mkataba na muungano na kulipa kwa ajili ya mali ya Muungano. Lincoln alikataa aliwaona kama wawakilishi wa serikali isiyo halali ambayo hawezi kutambua. Ilhali maafisa wa sehemu ya ngome za jeshi la Muungano katika kusini wameshakabidhi vituo vyao kwa serikali ya shirikisho, Lincoln alitaka kushika hasa ngome zile ambazo bado zilikuwa na maafisa na wanajeshi walioendelea kutii mari zake ; hizo zilipatikana katika Virginia, Florida na ngome ya Fort Sumter pale Charleston, South Carolina.
Mwanzo wa vita
haririVita ilianza wakati jeshi la Shirikisho lilishambulia ngome ya Fort Sumter pale South Carolina mnamo tarehe 12 Aprili 1861. Afisa mkuu wa ngome aliendelea kusimama upande wa serikali ya Muungano; alikuwa na amri kukaa katika ngome bila kushambulia mji au meli za bandari. Serikali ya kusini ilizuia vyakula visifike tena na kudai wanajeshi wa Muungano waondoke. Kwenye 12 Aprili walianza kufyatulia ngome kwa mizinga, siku iliyofuata watetezi walisalimisha amri.
Vita ilikuwa ndefu na watu 650.000 walikufa lakini mwishoni kaskazini ilishinda.
Marejeo
hariri- ↑ Linganisha "The Doom of Slavery, in the Union, Its Safety, out of it", imeandikwa na John Townsend, Charelston 1860, online [https://archive.org/details/doomslaveryinun02goog hapa]
Viungo vya nje
hariri- [http://web.archive.org/20080102180529/http://www.civil-war.net/ Ilihifadhiwa 2 Januari 2008 kwenye Wayback Machine. The Civil War Home Page]
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |