Karama (kutoka Kiarabu الكرامة) ni zawadi yoyote inayotokana na ukarimu wa Mungu kwa viumbe wake.

Mapokeo ya KiislamuEdit

Karama inatazmiwa kipaji cha pekee kutoka Mungu. Katika surat 19 (Al Maryam) Mariamu analishwa kwa neema ya Allah hii inatazamiwa pia kama karama. Karama inaweza kupatikana kama tabia au uwezo wa pekee, kama mtu mwenye kufanya miujiza kwa idhini ya Mungu. Mwenye kutoa karama ni Allah. Kwa sababu hiyo yeye anasifika kama Karimu. Katika Uislamu hilo ni mojawapo kati ya majina 99 ya kumsifia.

Katika UkristoEdit

Katika Biblia karama kwa kawaida ni tafsiri ya neno la Kigiriki χάρισμα ("kharisma" kutokana na χάρις, "kháris" neema). Neno hilo limekuwa likitumika sana katika Kanisa kuanzia Pentekoste na katika barua za Mtume Paulo, kwa msisitizo kuwa karama zote zinamtegemea Roho Mtakatifu.

Karama si zile za kushangaza tu, tena zile muhimu zaidi si hizo, bali zile zinazojenga zaidi Kanisa, kama zile za uongozi: “Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha” (1Kor 12:28). “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidii; mwenye kurehemu, kwa furaha” (Rom 12:6-8).

Karama nyingine muhimu zinawezesha kuishi kwa useja kama Yesu na Paulo, au kwa ndoa: “Nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane; ni heri wakae kama mimi nilivyo” (1Kor 7:7-8). “Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa” (Math 19:11). Tunavyoona katika historia ya watawa, mara nyingi karama ya useja inaendana na nyingine katika maisha ya sala, ya kijumuia na ya kitume. Hivyo Filipo “alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri” (Mdo 21:9).

Karama zinagawiwa na Roho Mtakatifu jinsi anavyotaka, si kwa sifa au faida ya binafsi, bali kwa ustawi wa taifa la Mungu. “Kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye... Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?... Kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa... Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani” (1Kor 12:11,29-30; 14:12,33). Kwa ajili hiyo mitume walipambanua na kuratibu karama katika ibada na katika maisha ya jumuia zisije zikavuruga Kanisa.

Karama za kushangaza zina hatari mbalimbali, hasa zikitiwa maanani mno. Hapo ni rahisi zilete majivuno, kijicho na mafarakano. “Ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je, si watu wa tabia ya mwili ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?... Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki... Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Kor 3:3; 4:8; 10:12). Katika mambo yasiyothibitika ni rahisi kudanganyika kuwa yametoka kwa Mungu, kumbe sivyo. Kisha kudanganyika ni vigumu kuachana nayo hata yakiwa na madhara kwa mhusika au kwa Kanisa. “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1Yoh 4:1).