Yvonne Cherrie

mwigizaji wa Tanzania

Yvonne Cherrie (alizaliwa 19 Agosti 1981) ni mshindi wa tuzo ya ZIFF kama mwigizaji bora wa filamu na mifululizo ya vipindi vya televisheni kutoka nchini Tanzania. Pia ni mtunzi wa muswada, mwandishi, mtayarishaji na mwongozaji wa filamu. Anafahamika zaidi kwa jina lake la uhusika uliompatia umaarufu kama "Monalisa". Vilevile Lulu katika tamthilia ya Siri ya Mtungi. Cherrie, alianza kuonesha upenzi wa kuigiza tangu akiwa mtoto mdogo. Akiwa na umri wa miaka 8, alianza kuigiza akiwa kanisani na baadaye shuleni.[1]

Yvonne Cherrie

Cherrie akishika tuzo yake ya Bab-Kubwa
Amezaliwa Cherrie Y. K. Salehe
19 Agosti 1981 (1981-08-19) (umri 43)
Dar es Salaam, Tanzania
Jina lingine Monalisa
Kazi yake Mwigizaji
mwongozaji wa filamu
mtayarishaji wa filamu
Miaka ya kazi 1998-hadi sasa
Ndoa Geoge Tyson (2001-2005)
Watoto Sonia Akinyi (2002).
Sean Abdulwahid Jr. (2007)

Maisha ya awali

Cherrie, alizaliwa katika hospitali ya taifa Muhimbili mjini Dar es Salaam, Tanzania na Susan Lewis (almaarufu Natasha), akiwa kama mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili aliojaaliwa kupata Bi. Lewis. Alianza kusoma shule ya chekechea huko mjini Luanda, Angola, na baadaye shule ya msingi ya Muungano ya Wilaya ya Temeke huko jijini Dar es Salaam kuanzia 1988 hadi 1994. Akabahatika kufaulu na kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya serikali ya wasichana Zanaki hadi mwaka 1998. Baada ya hapo alisoma katika chuo cha Uhazili Magogoni (ukatibu muhtasi-secretary). Mwaka wa 2002 alijiunga na British Council Tanzania ili kusomea zaidi lugha ya Kiingereza (Pre-Advanced Level) Mwaka wa 2003-2005 alijiunga na Wilnag Media Taining College huko mjini Nairobi, Kenya na kusomea masuala ya vyombo vya habari na kupata stashahada (Diploma in Mass Communication).

Kazi

Cherrie, pia ni mwigizaji wa jukwaani. Amepata kushiriki katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na tamasha la 18 na 19 la sanaa na utamaduni la Bagamoyo - katika Chuo Kikuu cha Sanaa cha Bagamoyo. Pia amewahi kutumbuiza katika jukwaa la ZIFF huko mjini Zanzibar mnamo 2002. Ambapo aliigiza kitabu cha Kirusi kiitwacho "Mkaguzi wa Serikali" (Gorvernment Inspector).[2]

Utumbuizaji wake mkubwa akiwa kama binti mdogo anayehangaikia kuliweka sawa penzi lake dhidi ya wapenzi wawili mnamo 1998 kupitia igizo la "Mambo Hayo" - ambamo alipata jina la Monalisa. Baadaye akarudia tena kazi yake ya uigizaji kwa kucheza uhusika wa jukwaani wa “Government Inspector” 2001 ikifuatiwa na “Zawadi ya Ushindi” 2002 kabla ya kuanza kuonekana tena rasmi katika filamu kibao.

Baada ya kutoka kwenye michezo ya televisheni filamu yake ya kwanza kucheza ilikuwa Girlfriend (2002) aliyocheza kama Zuwena kipenzi cha TID. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo rasmi wa mfululizo wa filamu kwani baada ya Girlfriend zikafuata Sabrina (2003),Dilemma (2004), She is My Sister 2006, Binti Nusa (2010), Network 2013.

Pia amepata kufanya igizo la jukwaani huko mjini Nairobi katika "Kenya National Theatre (KNT). Akiwa mjini Nairobi, amepata kutumbuiza jukwaani kwa kutumia vitabu vinavyotumika mashuleni nchini humo - ikiwa ni pamoja na kitabu cha KIU na A Man of the People mnamo 2003/2004. Pia alifanyakazi na Carib Theatre-UK akitumbuiza nchini Tanzania kuelimisha wanafunzi mradi ujulikanao kama TIE, yaani, Theatre in Education kwa miaka mitatu mfululizo.[3][4][5]

Utangazaji

TV

Cherrie, pia alifanya vipindi vya runinga kama vile Bongo Movies iliyokuwa ikioneshwa katika idhaa ya EATV. Awali alifanyakazi pia katika kipindi cha bahati nasibu maarufu kama Jackpot Bingo 1999-2001.

Redio

Alishawahi kufanya kazi na Radio One Stereo ya Tanzania mwaka 2001-2002 na kufanya vipindi mbalimbali ikiwemo Chombeza Time na Times FM Radio mwaka 2004-2005 akaacha kabla ya kurudi tena 2012 hadi sasa anafanya kipindi cha Filamonata kinachohusiana na masuala ya filamu na wasanii wa filamu wa Tanzania.

Maisha binafsi

Mwaka wa 2001 katika mwezi wa Agosti aliolewa na mtayarishaji/mwongozaji wa filamu kutoka nchini Kenya George Otieno Okumo (Tyson) na kubahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Sonia Akinyi (2002). Mwaka wa 2005 walitengana na 2012 akapewa talaka rasmi na mahakama. Mwaka wa 2007, alibahatika tena kupata mtoto mwingine wa kiume aitwaye Sean Abdulwahid Jr kutoka kwa baba mwingine aitwaye Abdulkarim Abdulwahid Abdulkarim.

Filamugrafia

Kama mwigizaji

  • Girlfriend
  • Sabrina
  • Dilemma
  • Jeraha la Ndoa
  • She is My Sister
  • Behind the Scenes
  • Where is God
  • Chanzo ni Mama
  • Black Sunday (ZIFF - 2010)
  • Binti Nusa 2 na 3
  • Payback
  • Nimeokoka
  • Cellular
  • Wrong Number
  • Wedding Pressure
  • Who is Smarter
  • Pastor Myambas Trial
  • 38 Weeks
  • Tell Me The Truth

Kama mwongozaji

  • Kaburi 1 (2007)
  • Chanzo Ni Mama (2007)
  • Binti Nusa 1. (2008)
  • Where is God (2009)
  • Binti Nusa 2 na 3 (2010)

Tuzo

  • Malkia wa Filamu za Bongo - Gazeti la Kiu 2007
  • Mwigizaji Bora Filamu wa Kike 2010 - Filamu-Central
  • Mwigizaji Bora Filamu wa Kike 2010 - ZIFF
  • Mwigizaji Bora Filamu wa Kike wa Muda Wote 2010 - Jarida la Bab-Kubwa

Uteuzi wa tuzo nchi za nje

  • Nigeria Entertainment - Tuzo Bora ya Waigizaji wa Afrika Yote kwa 2010 (Kateuliwa tu) - Nigeria
  • African Prestigious Awards - Msanii Bora wa Kike Afrika 2018 - Ghana

Viungo vya Nje

Marejeo

  1. "UJUE VILIVYO WASIFU WA YVONNE CHERRYL / MONA LISA (BIOGRAPH)". Bongo Film Database. Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  2. Michuzi Blog. "THE ZANZIBAR INTERNATIONAL FILM FESTIVAL AWARDS". MICHUZI BLOG. Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  3. donboye (2023-01-25). "Nigerian Entertainment Awards 2011 nominees". tooXclusive (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  4. Unknown (2015-04-02). "SWP: Full List of Nominees Tanzania Film Awards 2015, Dogo Maasai, Mdundiko, We Are Four Lead Nominations". SWP. Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  5. Monalisa (2011-01-16). "MONALISA AND THE TANZANIA FILM INDUSTRY: AHSANTE FILAMU CENTRAL". MONALISA AND THE TANZANIA FILM INDUSTRY. Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
  Makala hii kuhusu mwigizaji filamu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Yvonne Cherrie kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.