Abu Bakr

Abu Bakr (Kar.: أبو بكر‎‎ Abū Bakr al-Ṣiddīq; * 573 Makka kwa jina la ʿAbd Allah; + 23 Agosti 634 Madina) alikuwa khalifa wa kwanza wa Uislamu baada ya kifo cha mtume Muhammad. Alikuwa baba wa Aisha mke wake Muhammad.

Abu Bakr jinsi alivyomlinda mtume Muhammad dhidi ya watu wa Maka waliotaka kumtupia mawe - uchoraji wa karne ya 16 - Uturuki

Abu Bakr alikuwa kati ya wandani wa Muhammad walioshikamana naye tangu mwanzo na kungozana naye wakati wa hijra.

Baada ya kifo cha mtume alichaguliwa kiongozi mpya kwa msaada wa Umar ibn al-Khattab na Wakuraish. Abu Bakr akatumia cheo cha "mfuasi wa mtume wa Allah" (khalifatu-rasuli-llah) au khalifa.

Kati ya kazi zake za kwanza ilikuwa vita za riddah dhidi ya makabila ya Waarabu walioona ya kwamba baada ya kifo cha Muhammad hawakuwa na wajibu kwa kiongozi mpya. Wengine walikataa malipo ya zakat wengine walirudi kwa dini zao za awali.

Baada ya kushinda vita hizi Abu Bakr alituma jeshi lake dhidi ya Bizanti na Uajemi. Hapo kaskazini Waarabu walikutana na milki mbili kubwa zilizochoka baada ya vita ya miaka 30 kati yao. Zaidi ya hapo Wajemi walikuwa katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe. Jemadari Khalid bin Walid alishambulia Hira katika Mesopotamia na upande wa Bizanti jeshi la Waarabu likaingia katika Palestina.

Kwa upande wa dini Abu Bakr alimpa Umar bin Khattab kazi ya kukusanya mapokeo ya Korani. Kabla ya kuaga dunia alimtaja Umar kama mfuasi wake. Alikufa mwaka 634 mjini Madina akazikwa kando la Muhammad katika Masjid al Nabawi.