Cherero Uso-machungwa

Spishi ndogo kiasi ya familia ya kasuku
Cherero uso-machungwa
Cherero uso-machungwa katika hifadhi ya Serengeti
Cherero uso-machungwa katika hifadhi ya Serengeti
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Nusufaila: Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo)
Ngeli: Aves (Ndege)
Oda: Psittaciformes (Ndege kama kasuku)
Familia: Psittaculidae (Ndege walio na mnasaba na kasuku wadogo)
Vigors, 1825
Jenasi: Agapornis
Selby, 1836
Spishi: A. fischeri
Reichenow, 1887

Cherero (au kasuku-mapenzi) uso-machungwa (kisayansi Agapornis fischeri) ni ndege wa kundi la kasuku katika familia Psittaculidae. Msambao wa asili ni mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria katika Tanzania.

Maelezo

hariri

Cherero uso-machungwa ni kasuku mdogo aliye kijani hasa na kuwa na urefu wa sm 14. Uso wake una rangi ya machungwa na domo ni jekundu kali. Kisogo ni njano-dhahabu na utosi una rangi ya zeituni. Kuna miviringo myeupe kuzunguka macho. Upande wa juu wa mkia una manyoya buluu au zambarau. Dume na jike wana muonekano wa nje unaofanana.

Ndege huyu hujenga kiota katika shimo la mti. Jike hutaga mayai matatu hadi manane lakini manne au matano ni kawaida. Rangi yao ni nyeupe. Jike huatamia mayai kwa muda wa takriban siku 23 na makinda huondoka kwenye kiota siku 38-42 baada ya kuanguliwa.

Msambao

hariri

Cherero uso-machungwa ni wa asili ya Tanzania: mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria, katika Hifadhi ya Serengeti na mpaka Arusha. Ikiwa hali ya hewa ni kavu sana huhama mpaka Rwanda na Burundi ili kutafuta hali nyevu zaidi. Ametambulishwa kwa Dar es Salaam na mazingira yake na kwa mahali pengi katika Kenya. Ndege hao wameonekana porini huko Puerto Rico na Florida, lakina labda ni matokeo ya ndege wa kipenzi waliotoroka, na hakuna uzazi uliorekodiwa. Katika Ulaya wanazaana katika eneo la Algarve, Ureno ya kusini.

Ndege walioachiliwa nje ya msambao wa asili mara nyingi ni mvyauso kutokana na cherero shingo-njano. Uso wao ni kijivu. Uvyausaji pia hutokea porini ambapo spishi hizo huingiliana, haswa ndani na karibu na Hifadhi ya Serengeti.

Mahusiano na watu

hariri

Kama cherero wengine, cherero uso-machungwa hufugwa duniani kote na watu wanaofurahi kuifanya. Ufugaji huu umesababisha rangi mpya ambazo hazitokei porini. Ndege zinazotokea nje ya msambao wao wa asili ni ama watorokaji ama vizazi wao. Ndege kama hao wanaweza kupatikana katika na karibu na Dar es Salaam, Mombasa, Nairobi, Naivasha na Isiolo na maeneo kuelekea kaskazini mashariki.

Ndege hawa wanaweza kujilisha nafaka anuwai, kama mahindi na mtama, mbegu za alizeti na matunda na wanaweza kutokea kwa makundi makubwa kiasi. Kwa hivyo wanaweza kuwa wasumbufu katika mashamba, k.m. katika maeneo ya Manyara mpaka Arusha. Jina la kieneo selengwa linatumika labda kwa spishi hiyo pia pamoja na cherero shingo-njano. Mnamo mwaka wa 2021 serikali ya Tanzania ilitangaza hatua za kudhibiti spishi hiyo, ingawa matumizi ya dawa za kemikali (kama inavyotumika dhidi ya kwelea domo-jekundu) ilikataliwa. Ilipendekezwa kwamba ndege hao wanapaswa kutegwa.